Saturday 9 March 2013

Marekani yalaani kutekwa kwa Mhariri Kibanda

Ubalozi wa Marekani nchini umetaka kufanyike uchunguzi wa kina dhidi ya tukio la kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda.

Aidha, umetaka wahusika watakaokamatwa wafunguliwe mashitaka kwa kuwa mashambulizi dhidi ya wanahabari ni tishio kwa demokrasia.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, alijeruhiwa usiku wa kuamkia Jumatano ya wiki hii na watu wasiofahamika.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, amelaani mashambulizi hayo.

Pia balozi huyo ameeleza kufurahishwa na taarifa za uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya tukio hilo.

Akielezea kuhusu vyombo vya habari alisema  uhuru ni muhimu katika demokrasia na jukumu la waandishi ni kuelimisha jamii na kuiwezesha kutiririsha mawazo katika taifa.

Wakati huo huo, Chama cha Mapinduzi  (CCM)  kimesema kitendo cha kushambuliwa kwa Kibanda ni unyama usiokubalika ambao unapaswa kulaaniwa na Watanzania wote.

Taarifa ya chama hicho  iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, imeitaka serikali ihakikishe inawapata wahusika.

 “CCM tunaitaka Serikali kuhakikisha inawapata waliofanya unyama huo na kukomesha matukio ya namna hiyo,” imesema taarifa hiyo.

Kadhalika, chama hicho kimetoa pole kwa uongozi wa Jukwaa la Wahariri, Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari 2006, familia ya ndugu Kibanda, wanahabari na wadau wote wa habari nchini.

Kufuatia tukio hilo, jeshi la polisi liliunda timu ya maofisa 12 kwa ajili ya uchunguzi ambayo ilianza kazi jana.

Aidha wakati uchunguzi huo ukiendelea, majeruhi huyo anaendelea na matibabu yake huko Afrika Kusini.

Kibanda alivamiwa na watu wasiojulikana wakati akijiandaa kufunguliwa lango la kuingia nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
DPP aahidi kuwashughulikia waliomdhuru Kibanda

DPP KUSHUGHULIKIA WALIOMDHURU

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, ameahidi kuwashughulikia watu waliohusika kumdhuru Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Absolom Kibanda kwa kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Alisema vitendo vya kihalifu vimezidi kuongezeka nchini na ofisi yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupambana na vitendo hicho.

Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, alisema unyama aliofanyiwa Kibanda ni kielelezo kuwa vitendo hivyo vimeshika kasi na kuvuruga amani.

Alisema, ofisi yake licha ya kujitahidi kuchuja mashtaka mbalimbali lakini bado kasi imekuwa kubwa, licha ya kwamba kuna kesi zingine zinasubiri maamuzi kama watakuwa na hatia au hawana.

Feleshi alisema anasubiri watu waliomjeruhi Kibanda wakamatwe na kuahidi kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa kusimamia kesi hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine.

"Tukio lilompata Mhariri Absalom Kibanda limenisikitisha sana, huu ni mfano jinsi gani kasi ya kuongezeka makundi ya kulipizana kisasi ilivyokuwa kubwa hapa nchini," alisema DPP Feleshi.

"Leo wamemjeruhi Kibanda, hujui kesho atakuwa nani, yawezekana akawa profesa au mbunge na hata mimi, ni jambo la hatari sana," alisema Feleshi.

Alisema kama Kibanda alifanya kosa dhidi yao jambo jema wangemshtaki kwa Baraza la Habari (MCT) au MOAT, lakini unyama waliomfanyia haukubaliki katika nchi inayofuata ustaarabu.

Alisema hataona haya kumchukulia hatua mtu yeyote hata iwe inatokana na dini au kabila, anachokifanya ni kwa ajili ya maslahi ya umma na kwa mujibu wa sheria ya nchi.
"Kitu kikubwa ninachotaka ni amani ya nchi, sitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote anayevuruga amani kwa misingi yoyote ile," aliongeza kusema.

Wakati huo huo, Jukwaa la Wahariri(TEF) jana liliunda timu ya watu watano watakaochunguza tukio hilo ndani ya wiki mbili na kutoa ripito. Wajumbe wa timu hiyo ni watatu toka katika jukwaa, na wajumbe wawili mmoja toka Baraza la Habari Tanzania(MCT) na mwingine toka Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika(Misa Tanzania)
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment