Monday 11 March 2013

Ukweli kuhusu masaibu ya Kibanda


WAKATI hali ya Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Absalom Kibanda ikiendelea kuwa tete, ukweli kuhusu afya yake na masaibu yaliyompata umejulikana, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Habari kutoka nchini Afrika Kusini kwenye Hospitali ya Milpark anakotibiwa, zinasema kuwa majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana ni makubwa na yatamwacha na ulemavu wa kudumu.
Taarifa kutoka kwa watu walio karibu na Kibanda hospitalini hapo, zinasema kuwa mishipa yote inayozunguka jicho lake la kushoto imevunjika na jicho hilo limesambaratika lote na madaktari sasa, wameamua kuling’oa kabisa.
Madaktari wanne wanaomfanyia uchunguzi na kumpatia tiba Kibanda, wanasema kuwa jicho hilo limesambaratishwa na risasi na atawekewa jicho la bandia ambalo hata hivyo halitaweza kuona.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali wa madaktari, kuna madhara kidogo kwenye ubongo wake na kiasi fulani cha damu kimechuruzika kwenye sehemu hiyo ya ubongo.
“Ubongo umedhurika kidogo na madaktari wanampa dawa ya kuyeyusha damu kwenye ubongo. Madaktari wanasema tusiogope, wanaweza kuidhibiti hali hiyo, lakini kipaumbele chao cha kwanza ni jicho. Wakishamaliza jicho ndipo watashughulikia ubongo,” ilisema taarifa hiyo.

Habari zaidi kuhusu afya ya mhariri huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), zinasema kuwa jana alifanyiwa upasuaji kwa saa nne kwa ajili ya kutengeneza upya sura yake, kuweka vizuri paji la uso, na kurekebisha mfumo wa meno.
Pia alifanyiwa upasuaji wa jicho la kushoto na taarifa mbaya ni kwamba madaktari wameshindwa kuliokoa, hivyo wameling’oa.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa TEF, Neville Meena, ilisema kuwa madaktari wamechukua hatua ya kitatibu baada ya kuwa tayari jicho hilo lilikuwa limepondeka kwa ndani hivyo lisingeweza tena kuona. Atawekewa jicho la bandia la plastiki ambalo hata hivyo halitakuwa likiona.
“Jambo la kumshuruku Mungu ni kwamba kwa ujumla upasuaji huo uliochukua saa 5 na dakika 30 umefanyika kwa ufanisi mkubwa, na ulikuwa ukiongozwa na madaktari bingwa watatu. Wawili kati yao ni wataalamu wa kichwa na mmoja ni mtaalamu wa macho,” alisema Meena.
Katika upasuaji huo, hakukuwa na madhara ya ndani katika kichwa chake, hivyo kiko salama. Sura yake imejengwa upya kutokana na majeraha ambayo yalikuwa yametapakaa baada ya 
kupigwa na watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa habari hizo, changamoto kubwa waliyokutana nayo madaktari waliomfanyia upasuaji ni kurejesha katika sehemu yake baadhi ya mifupa midogo inayozunguka jicho, pia kurejesha taya la kushoto ambalo lilikuwa limeathiriwa na tukio la kupigwa kwake. Hata hivyo hatimaye walifanikiwa.
Ripoti kamili kuhusu upasuaji huo inatarajiwa kutolewa leo.
“Tuendelee kumwombea Mwenyekiti wetu Kibanda ili Mungu amponye. Kwa niaba ya Bodi ya Wakurungezi ya Jukwaa la Wahariri, kwa mara nyingine tunampa pole Kibanda pamoja na familia yake na tunamtakia uponyaji wa haraka,” ilisema taarifa hiyo.
Kabla ya upasuaji wa jicho jana, juzi Kibanda alifanyiwa upasuaji kutengeneza upya sura yake, kuweka vizuri paji la uso, na kurekebisha mfumo wa meno.
Upasuaji huo ulifanyika baada ya kupungua kwa majeraha na uvimbe katika sehemu mbalimbali za mwili wake, hususan kichwani na usoni.
Upasuaji huo pia unazingatia matokeo ya uchunguzi uliofanywa kwa zaidi ya saa 48 na jopo la madaktari wanne na kubaini madhara ya awali aliyoyapata mwanahabari huyo nguli.
Kuhusu jicho lake la kushoto ambalo lilijeruhiwa kwa kiasi kikubwa, madaktari walisema wangetoa uamuzi kuhusu aina ya upasuaji ambao wangeufanya baada ya kubaini hali halisi wakati watakapokuwa wakijenga sura yake ambayo iliharibiwa kwa majeraha.
“Wakati akipelekwa kwenye chumba cha upasuaji, Kibanda alikuwa akilalamikia maumivu kutokana na kidonda kilichopo kwenye mguu wake wa kushoto, kidonda hicho pia ni matokeo ya unyama aliyofayiwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya TEF.
Wakati Kibanda akiendelea na matibabu, jana Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ambao wako Afrika Kusini kikazi, walimtembelea kumjulia hali hospitalini hapo.
Katika salamu zake, Rais Kikwete alisema serikali itawasaka hadi kuwatia nguvuni wahusika wa tukio hilo la utesaji na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Jinsi alivyoshambuliwa

ngawa uchunguzi wa shambulio dhidi ya mhariri huyo umeanza, duru za uchunguzi zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kundi lililohusika kuwa lile liliomteka, kumtesa na kisha kumtelekeza kwenye Msitu wa Mabwepande, Dk. Steven Ulimboka.
Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, aliyeongoza mgomo wa wanataaluma hao, aling’olewa meno, kucha, kupigwa kichwani - staili ya utesaji ambayo pia imetumika kwa Kibanda.
“Ukiangalia jinsi alivyoteswa Kibanda, hakuna tofauti na Ulimboka. Tofauti yake kidogo ni kwamba kwa Kibanda walitumia muda mfupi sana, kama dakika tano hivi. Lakini yote kwa yote, hawa ni watu hatari na ni wataalamu,” alisema mtoa habari wetu kutoka Jeshi la Polisi.
TMF watoa ruzuku kuchunguza
Katika hatua nyingine Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), umesema utatoa ruzuku ya fedha kuwawezesha waandishi wa habari kufanya habari za uchunguzi kubaini chanzo cha ukatili aliofanyiwa Kibanda.
Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura katika taarifa yake alisema kuna kila sababu ya kuchunguza tukio hilo ambalo ni mfululizo wa matukio yanayopunguza uhuru wa vyombo vya habari nchini na kuwajengea woga wa kufanya kazi zao.
“Kwa vyovyote vile na kwa sababu zozote, wanaotoa vitisho kwa waandishi na kuwafanyia vitendo vya kikatili ni maadui wa uandishi wa habari za uchunguzi. Ni kwa msingi huu, TMF ipo tayari kutoa ruzuku ya chapuchapu na kuungana na wadau wengine wa habari kuchunguza kilichomtokea Kibanda,” alisisitiza Sungura katika taarifa hiyo.
Alisema TMF katika awamu ijayo, itaandaa mpango mkakati unaolenga kuwalinda waandishi wa habari wanaofanya habari za uchunguzi, ikiwemo kufikiria uwezekano wa kuwawekea bima ya kazi kwenye mazingira hatarishi.
Kibanda alivamiwa na kushambuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake saa 6.15 usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita, maeneo ya Goba Kunguru, Mbezi Beach, Kata ya Kawe, jijini Dar es Salaam.
Tayari Jeshi la Polisi limeunda tume, huku Jukwaa la Wahariri, nalo limeunda timu maalumu kuchunguza na kubaini waliohusika na tukio hilo.
chanzo:daima


No comments:

Post a Comment