Tuesday, 16 April 2013

Akimbilia polisi akiogopa kukeketwa


MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Chiringe, Sikujua Pius (16), amelazimika kukimbia kwao na kwenda kujisalimisha Kituo cha Polisi Bunda akiogopa kukeketwa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mwanafunzi huyo alisema Machi 21, mwaka huu majira ya jioni baada ya kutoka shuleni na kula chakula, aliitwa chumbani na kaka yake na wifi yake aitwaye Mwajuma na alipoingia walimkamata na kumlaza chali wakimlazimisha wamkekete kwa nguvu.
Alisema baada ya kuona hivyo alipiga kelele na kufanikiwa kuwaponyoka, lakini walimkamata tena na kumvuta ndani na baada ya muda baba yake alifika akawataka wamuachie.
“Waliniachia huku wakinitukana kuwa hawawezi kuishi na mimi kama sijakeketwa,” alisema.
Alifafanua kuwa baada ya kuona hali hiyo aliamua kukimbilia Kituo cha Polisi Bunda ambako alitoa taarifa na kuchukuliwa na ofisa mmoja wa polisi ambaye anamhifadhi hadi sasa huku jitihada za kuwatafuta watuhumiwa wa tukio hilo zikiendelea, kwani walitoroka baada ya polisi kufika nyumbani kwao.
“Naomba polisi iwakamate wahusika wa tukio hilo na wafikishwe mahakamani, vinginevyo nitasoma kwa shida,” alisema.

Alisema yeye na mdogo wake wamekuwa wakiishi kwa kaka yao baada ya mama yake kuachana na baba yake miaka mitatu iliyopita.
Kwa upande wake Jeshi la Polisi limeeleza kuwa wanaendelea kuwasaka watuhumiwa hao ili waweze kuwafikisha mahakamani huku wakifanya jitihada za kumsaidia mwanafunzi huyo ili aweze kumaliza masomo yake.
“Tunajaribu kutafuta uwezekano wa kumpeleka kwenye mashirika yanayolea watoto walio katika matatizo kama haya, nadhani Tarime kuna shirika kama hili, bado tunafanya uchunguzi ili tuweze kujua mahali pa kumpeleka,” alisema ofisa mmoja wa polisi.
Vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike vimeshamiri mkoani Mara kutokana na jamii kutobadili mila, ambapo inasadikiwa kuwa mwaka jana watoto 4,000 walitarajiwa kukeketwa kutoka katika wilaya za Tarime, Bunda, Serengeti na Butiama, huku jitihada mbalimbali zikifanywa na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment