FILAMU mpya ya nguli wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba, inayojulikana kwa jina la ‘Love and Power’ itaanza kusambazwa kuanzia Aprili 12 mwaka huu.
Filamu hiyo iliyozinduliwa Aprili 7 katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam ikiendana na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufariki dunia kwa nguli huyo, tayari imeanza kuwa gumzo kubwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo, mdogo wa Kanumba, Seth Bosco, ambaye ni msimamizi wa Kampuni ya Kanumba The Great, aliwashukuru Watanzania waliokuwa wamejitokeza.
Alisema siku ya juzi hawezi kuisahau katika maisha yake kutokana na kuzinduliwa kwa kazi ya kimataifa iliyofanywa na Kanumba kabla ya kufariki dunia Aprili 7, mwaka jana.
“Kanumba alikuwa na ndoto za kuikomboa nchi yetu katika tasnia ya filamu, nafikiri naye Mungu anajua ni kwanini kamchukua, hivyo yatupasa kushukuru kwa kila jambo,” alisema Bosco.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wasanii nyota kutoka Ghana, Ama Abebrese, Ama Mc Brown na aliyekuwa Meneja wake wa Kimataifa, Prince Richard na wasanii mbalimbali wa filamu wa hapa nchini.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka jana nyumbani kwake Sinza – Vatican jijini Dar es Salaam, huku kifo chake kikihusishwa na msanii mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment