Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Lushoto Wilson Yona (35), amekiona cha moto kwa kile kilichodaiwa kushambuliwa kwa kupigwa vibao, mateke na ngumi na Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo, wakati akitekeleza wajibu wake kazini.
Tukio hilo la aina yake lilitokea saa 2:16 asubuhi ofisini kwa hakimu huyo, katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wakati akiwa anaandika hukumu za washtakiwa wengine.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Afisa Upelelezi mkoa wa Tanga, Azizi Kimatta, alisema hakimu huyo baada ya kupata maumivu alipewa fomu ya PF3 kwa ajili ya matibabu iliyotolewa na polisi Na. 5224 PC Hamis.
Akiongea na NIPASHE Jumapili, kuhusu mkasa huo, hakimu huyo alisema akiwa ofisini kwake Machi 22, mwaka huu, mkuu huyo wa upelelezi alimfuata na kuanza kumshambulia akimtuhumu kuwa hajui kufanya kazi yake vizuri.
Hakimu alidai kuwa pamoja na polisi kukataa kufungua jalada la kesi kwa madai ya kumlinda bosi wao, anakusudia kutumia njia nyingine ya kufungua kesi hiyo.
"Amenishambulia sana kwa ngumi, vibao na mateke utadhani mhalifu eti anadai kuna watuhumiwa nimewapatanisha na walalamikaji wakati suala la kupatanisha ni la jeshi la polisi.
“Nikamwambia sikutambui namfahamu mwendesha mashtaka wako mwambie aje nimfahamishe, na ndipo alipoanza kuniporomoshea kipigo kama mhalifu", alidai hakimu huyo.
NIPASHE Jumapili ilimtafuta mtuhumiwa anayejulikana kwa jina la Jumanne Juke na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantino Massawe bila mafanikio.
Hata hivyo, Afisa Upelelezi, Kimatta aliimbia NIPASHE kuwa suala hilo linaendelea kufanyiwa uchunguzi na polisi.
chanzo: nipashe
No comments:
Post a Comment