Tuesday, 23 April 2013

Lema ailiza tena CCM



KWA mara nyingine tena Mahakama ya Rufaa nchini, imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na walalamikaji, Musa Mkanga, Agnes Mollel na Hapiness Kivuyo ya kutaka kupitia upya hukumu iliyomrejesha Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).
Walalamikaji hao ambao ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia kwa mawakili wao, Alute Mughwai na Modest Akida, walidai kutoridhishwa na hukumu hiyo iliyotolewa Desemba 21 mwaka jana.
Walikuwa wakidai kuwa kulikuwa na mapungufu katika hukumu hiyo, hivyo walilitaka jopo la majaji waliohukumu kesi hiyo kukubali kubatilisha uamuzi wao ili rufaa ya kesi namba 47/2012 waliyokuwa wamefungua isikilizwe upya.
Wakili Mughwai aliitaka mahakama ifutilie mbali hukumu hiyo kwa madai kuwa ilipingana kwa kiasi kikubwa na hukumu iliyotolewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Akitoa mfano wa kesi zingine mbalimbali zilizowahi kupatikana na mazingira kama kesi ya Lema, Mughwai alijikita katika kifungu cha 66(a) na (b), na 4(ii), ambavyo majaji walimwambia amevichanganya vibaya badala ya kufungua kila dai moja peke yake.
Hata hivyo wakili huyo alidaiwa kuwa kuna vifungu alikuwa anavisema kwa mdomo wakati hakuviweka katika maandishi.

Nao mawakili wa Lema, Method Kimomogolo, akisaidiwa na Tundu Lissu walitoa utetezi kuwa maombi hayo yaliletwa kinyume cha utaratibu, hivyo kutaka kuichanganya mahakama.
Walidai kuwa utaratibu uliotumika haukuwa sahihi, huku wakisisitiza kuwa kosa ambalo upande wa waleta maombi haukuonyesha kosa wazi, kwani kama lingekuwa dhahiri hakungehitajika kurasa 29 za maandishi kuelezea kosa hilo.
Kimomogoro alisoma kwa uangalifu sababu 11 kujibu hoja za wakili Mughwai na kwa umakini akilezea sababu za kutokuwepo kesi ya kujibu au sababu za kupitia hukumu hiyo upya.
Kimomogolo adai, “Hatukuona kama ni suala la msingi kwa kuwa suala lenyewe halikuwa wazi zaidi, hii ni kwa sababu msingi wa hoja ya kesi (locus standi) ni wa muhimu katika kuanzisha kesi zozote za kisheria katika mahakama.”
Kwamba kuna kesi ya kujibu au hakuna kisheria, alidai kuwa mahakama ilikuwa sahihi iliposema kuwa suala la hoja ya msingi wa uwepo wa kesi (locus standi) ni la umuhimu katika uendeshaji wa kesi kama hizo.
Aidha, pande zote mbili zilisema kuwa suala la walalamikaji kuwa wapiga kura walioandikishwa kupiga kura katika uchaguzi ambao matokeo yake yanalalamikiwa, vivuli vya vitambulisho vyao vya kupigia kura vimewekewa alama A( l-J).
“Ni kweli kwamba wakili Mughwai aliwasilisha vitambulisho vya kupigia kura kuthibitisha kuwa walalamikaji walikuwa ni wapiga kura walioandikishwa, hayo yalijiri mahakamani Aprili 6, 2011,” alisema Kimomogoro.
Aliongeza kuwa kwa bahati mbaya vitambulisho vya wapiga kura havikutolewa na kukubaliwa na mahakama kama ushahidi kwa kanuni za kimahakama na taratibu zake na hivyo katika kesi hiyo hakukuwepo na ushahidi kwenye kumbukumbu za mahakama na majaji walipomwomba Mughwai aionyeshe kama alifuata taratibu hizo hakuweza.
Hata hivyo pamoja na mivutano yote ya kisheria ya pande zote, jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Engela Kilewo akisaidiwa na Bernard Luanda na Salumu Masatti, waliyatulipia mbali maombi hayo ya kupitiwa upya kwa hukumu hiyo kwa misingi kuwa haikuwa na nguvu kisheria.
Baada ya hukumu hiyo, wakili Mughwai alisema kuwa anaikubali hukumu ya mahakama, huku Lissu akiwataka watu kuacha kutumika kufungua kesi.
Aliionya CCM iache kuwasumbua badala yake itumikie wananchi na isubiri uchaguzi mkuu 2015.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment