Majambazi ambao idadi yao haijafahamika wamevamia mashine za kuweka na kutolea fedha (ATM) zinazomilikiwa na Benki za NMB na CRDB, katika kituo cha daladala cha Tabata Kimanga, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuzivunja na kupora fedha zilizokuwamo.
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa majambazi hayo yalivamia mashine hizo majira ya kati ya saa 7 na 8 ya usiku wa kuamkia jana, baada ya walinzi wanaozilinda kuzidiwa na usingizi mzito.
Yanadaiwa kutumia vifaa mbalimbali vya kuchomea ili kufanikisha uhalifu huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi wa Jeshi hilo (ACP), Marietha Minangi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, alisema hadi jana hakukuwa na mtu yeyote aliyekamatwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Pastory Kiombya, alisema kabla ya kwenda kwenye eneo la tukio, alielezwa kwa njia ya simu na baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo kuwa majambazi hayo yalivamia mashine hizo baada ya walinzi kushikwa na usingizi mzito.
Alisema haijulikani kama usingizi uliwashika walinzi hao ulitokana na ama na kulishwa vyakula au kupuliziwa dawa za usingizi.
Alisema hali hiyo iliyowasibu walinzi hao, iligunduliwa na wenzao waliofika kuwapokea lindo jana asubuhi.
Kiombya alisema baada kupatwa na masaibu hayo, walinzi hao walipelekwa hospitali kwa uchunguzi.
Hata hivyo, alisema hadi jana jioni alikuwa hajui ni hospitali gani walikopelekwa walinzi hao.
Alisema baada ya kuelezwa hayo, alifika katika eneo la tukio, ambako aliwakuta baadhi ya maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi na wa Benki za NMB na CRDB wakifanya ukaguzi, ikiwa ni pamoja na kuwahoji baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo.
Naye Kamanda Minangi akielezea tukio hilo, alisema majambazi hayo hayakufanikiwa kupora fedha kwenye mashine hizo, baada ya jaribio lao la kuzivunja kuishia njiani.
“Hela zilikuwamo (kwenye ATM hizo). Lakini hawakuiba. Kwa sababu hawakumaliza (jaribio lao la kuvunja ATM hiyo),” alisema Kamanda Minangi.
Kwa mujibu wa Kamanda Minangi, haijajulikana kama kushindikana kwa jaribio lao hilo kulitokana na majambazi hayo kukurupushwa na watu au la.
Baadhi ya mashuhuda walisema kutokana na walinzi hao kuzidiwa na usingizi mzito, majambazi hayo yalifanya jaribio lao bila kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Walikutwa wamelala hadi saa 1 asubuhi,” alisema mmoja wa mashuhuda.
Hata hivyo, mashuhuda hao walisema jaribio la majambazi hayo kuvunja ATM hizo halikufika mwisho baada ya kukurupushwa na watu waliotokea eneo hilo.
Kamanda Minangi alisema majambazi hayo yalijaribu kuvunja ATM hiyo kwa njia ya kukata chuma kwa moto wa kuchomelea nondo.
Hata hivyo, alisema kama si kukurupushwa na watu, yawezekana jaribio lao lilishindikana kutokana na uimara wa mashine hizo.
Alisema majambazi hayo yalipoondoka, yaliacha vifaa mbalimbali katika eneo la tukio.
Baadhi ya vifaa hivyo, ni pamoja na mitarimbo na mitungi ya gesi vinavyosadikiwa kutumiwa na majambazi hayo kuvunja ATM hizo.
Alisema mbali na vifaa hivyo, pia lilikutwa gari dogo aina ya Toyota Corolla katika eneo hilo.
Hata hivyo, alisema hadi jana gari hilo lilikuwa halijajulikana kama lilitumiwa na majambazi hayo katika tukio hilo au la.
Alisema vifaa hivyo, pamoja na gari hilo, vyote vinashikiliwa na polisi na kwamba, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Tukio hilo limetokea miezi michache baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kusaidiana na maofisa wa Benki ya NMB kuwatia mbaroni watu watatu waliodaiwa kuiba Sh milioni 700 kwa nyakati tofauti.
Watuhumiwa hao walinaswa baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa benki na polisi kwenye saa 6.00 usiku wa Februari 10, mwaka huu na mtuhumiwa mmoja kubambwa akichukua fedha katika ATM ya NMB kwenye Tawi la PPF Plaza Mwanza.
Baada ya kunaswa kwa mtuhumiwa huyo, alisaidia kuwaelekeza polisi walipo wenzake, ambao walikutwa katika hoteli moja jijini Mwanza wakiwa wamejipumzisha.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mwanza, Christopher Fuime, alisema pia walikamata vifaa mbalimbali, ambavyo walikuwa wakitumia kwa ajili ya kufanyia uhalifu huo.
Vifaa vilivyokamatwa ni kadi za bandia 194 za kuchukulia fedha katika ATM za Benki ya NMB, kadi 36 za Benki za DTB, tatu zenye maandishi ya Download List na nyingine ikiwa ni kadi ya Visa ya Benki ya KCB.
Pia walikutwa na kadi ya Benki ya Amerikani, pia walikamatwa wakiwa na vifaa mbalimbali vya kielektroniki, ikiwamo kamera za siri tatu za kienyeji, ambazo zimetengenezwa kwa kufungwa betri za simu ya mkononi na pia walikamatwa na kifaa cha kutengenezea kadi bandia (Magnetic Card reader), mikebe mitatu ya rangi za kupulizia kamera za usalama katika ATM ili wasionekane wakati wa wizi wao, ‘printer’ pamoja na kifaa cha kuchomea vifaa vya umeme.
Aidha, Novemba 20, mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Lawrence Mafuru, alikaririwa akisema wizi kwa kutumia ATM ni tatizo linaloathiri wateja wengi wa benki nchini na limekuwa likiongezeka.
Mafuru alisema hayo katika Tawi la Corporate la Benki hiyo lililoko jijini Dar es Salaam wakati NBC ilipozindua kampeni ya huduma kwa wateja.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment