Wednesday, 17 April 2013

Msafara wa mbunge wanusurika kutekwa


MBUNGE Viti Maalumu, Susan Kiwanga (CHADEMA), na ujumbe wa benki ya NMB Kanda ya Mashariki, wamenusurika kuvamiwa na watu wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi katika kijiji cha Mbingu wilayani hapa.
Kunusurika huko kulikotokana na wasamaria wema kuwashtukia watua hao majira ya saa 8 mchana na kutoa taarifa kituo cha polisi Mbingu waliofanikisha kuwanasa kabla viongozi hao waliokuwa shule ya msingi Mtyangimbole iliyo kijiji cha Ikule na shule ya msingi Kitete, iliyo kijiji cha Mkangawalo, kata ya Mngeta, kutoa msaada wa madawati 78.
Mbele ya mbunge Susan ambaye pia ni Mwenyekiti wa  CHADEMA mkoani Morogoro aliyeamua kupita kituoni hapo kuwashuhudia watu hao, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mbingu, Adriano Mayo, aliwataja waliokamatwa kuwa ni Shomari Miraji (29) mkazi wa Kibaha Mwendapole, Shukuru Bakari (33), mkazi wa Mlandizi, Abdalah Ally (33), mkazi wa  Dar esSalaam na Stumai Shaban (30) mkazi wa Bagamoyo.
“Baada ya mahojiano walikiri kuwa kuna baadhi ya matukio waliyafanya,” alisema polisi huyo.
Hata hivyo, Mayo alimwambia mbunge huyo kuwa kituo hicho hakina jengo la kuhifadhia wahalifu, ofisi, silaha, vifaa vya usafiri kama gari kwa ajili ya doria katika barabara hiyo na fedha za hamasa juu ya upatikanaji taarifa za kihalifu.

Mbali na mkuu huyo wa kituo kutoa malalamiko na adha dhidi ya uduni wa mazingira ya kazi, ofisa mtendaji wa kijiji hicho Salum Sadala alimwomba mbunge huyo kukisaidia kijiji hicho upatikanaji wa fedha shilingi mil.6 kukamilisha jengo la kituo hicho cha polisi kijijini hapo ambalo liko katika hatua ya mwisho ya ujenzi naye Susan aliahidi shilingi 200,000 mwezi ujao.
“Mbunge tumekwama kukamilisha jengo hili na kituo cha polisi ili tuimarishe usalama; ni kiasi kisichozidi shilingi mil.6 tunahitaji; tunaomba popote ufikapo tusaidie kupata mfadhili maana hali ya sasa kwa wananchi si nzuri kuwabana michango,” alisema Sadala.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment