Wednesday 10 April 2013

Mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari anaswa


MFANYABIASHARA maarufu mkoani Kilimanjaro, Adrian Tilika Mariwa (38) amenaswa na makachero wa Jeshi la Polisi akihusishwa na mtandao wa wizi wa magari yanayodaiwa kuibwa nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita, magari hayo yalisafirishwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ikiwamo DRC kupita hapa nchini.
Moita alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alinaswa na polisi nyumbani kwake eneo la Kiboriloni akiwa na magari matatu yakiwa yamebandikwa namba bandia na kwamba sasa yapo mikononi mwa polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Alisema kuwa Mariwa alikamatwa Aprili 8 mwaka huu, saa 12 jioni baada ya askari wa doria katika maeneo ya kiboriloni kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwapo kwa magari hayo nyumbani kwake.
Moita aliyataja magari yaliyokamatwa ni aina ya Mitsubishi Fusso lililokuwa na namba bandia za usajili T 130 AUN, Ford Ranger lenye namba T 130 AWN na Vitara lenye namba za usajili T 518 BJP.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa mtandao wa wezi wa magari katika miji ya Arusha na Moshi umeshamiri kutokana na kuwapo kwa baadhi ya askari wanaoshirikiana na wahalifu hao.
Ushahidi huo unatokana na ukweli kwamba baadhi ya askari wamewahi kukamatwa na magari ya wizi.
Baadhi ya madereva wa magari ya wizi yanayodaiwa kumilikiwa na askari hao wakiyatumia kama teksi bubu, waliliambia gazeti hili kuwa hufichwa wakati wa operesheni ya kusaka magari ya wizi ambayo hufanywa na makachero wa upelelezi kutoka makao makuu ya jeshi hilo wakishirikiana na wale wa kimataifa (interpol).
Walidokeza kuwa magari hayo baada ya kuingizwa nchini, hufichwa katika maeneo ya Mailisita wilayani Hai, Majengo na Rau mjini Moshi ambako huchakachuliwa ‘cheeses’ namba zake na kuwekewa za bandia ambazo ni nadra kutambulika.
Akizungumza na Tanzania Daima hivi karibuni, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz ambaye kwa sasa yupo likizo alisema zaidi ya magari matano ya wizi yalikamatwa kutoka nchi jirani ya Kenya wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi wa nchi hiyo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment