Dar es Salaam. Mwili wa mwanafunzi wa Tanzania aliyefia nchini China, Leonard Peter Tambalu aliyekuwa akisoma Chuo cha Huazhong Agriculture, mjini Wuhan sasa utawasili leo ukitokea Addis Ababa, Ethiopia.
Awali, habari zilizopatikana juzi zilidai kuwa mwili huo ungeletwa nchini jana, lakini kutokana na kuunganisha ndege, ilibidi kulala Addis Ababa.
Tambalu aliyekuwa Ofisa Kilimo Mwandamizi wilayani Iramba, Mkoa wa Singida, alifikwa na mauti Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ndege wa Beijing akijiandaa kupanda ndege kuja nchini.
Habari zilizopatikana jana kutoka Beijing, China zilisema mwili wa Tambalu uliondoka Beijing jana Aprili 9 saa 5:59 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kwa ndege namba ET605 iliyotua Addis Ababa saa 2:59 asubuhi. Baadaye ndege itakayochukua mwili wa Tambalu, itaondoka Addis Ababa leo saa 4:30 asubuhi kwa ndege namba ET805 inayotarajiwa kufika Dar es Salaam saa 7:25 mchana.
Hivi karibuni, Katibu wa Umoja wa Wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali Mji Wuhan (Wtasa), Hamphrey Sikauki alisema Tambalu alifariki na mwili wake ulikuwa unafanyiwa uchunguzi na maofisa wa Serikali ya China wakishirikiana.
Wakati huohuo, Jane Tumainieli, aliyekuwa mke wa Mnadhimu Mkuu Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Tumainieli Kihwelu atazikwa leo nyumbani kwake Mbezi Louis.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment