Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na uvamizi wa mashine za kuweka na kutoa fedha (ATM) zinazomilikiwa na Benki ya NMB na CRDB, katika kituo cha daladala cha Tabata Kimanga, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda Kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema ATM hizo zilizokuwa na zaidi ya Sh. 50,000,000. Hata hivyo, Kova hakutaja majina ya watuhumiwa kwa madai kwamba bado wapo kwenye upelelezi.
Kamanda Kova aliwaonya walinzi wote wa kampuni binafsi na wa Serikali wasiwe na tamaa ya kula hovyo haswa kula chakula ambacho hawajui kilipotoka kwa kuwa wanaweza kuwekewa dawa za kulevya.
Kauli hiyo inatokana na walinzi waliokuwa lindoni katika ATM hizo kunywa kahawa waliyopewa na mfanyakazi mwenzao ambayo inasemekana ilikuwa na dawa za kulevya zilizowapelekea kupitiwa na usingizi mzito mpaka waliposhituliwa na mfanyakazi mwenzao ambaye alienda kuwapokea lindo.
Pia alisema wamekamata mitungi ya gesi na nondo ambavyo vilitumika katika tukio hilo la kuvunjwa kwa mashine za ATM hizo.
Wakati huo huo, Kamanda Kova alisema Polisi inawashikilia watu 16 kwa kuhusika na matukio tofauti likiwamo kukamatwa kwa meno manane ya tembo na vipande 19 vya meno hayo vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. 30,000,000.
Katika tukio lingine, Polisi inawashikilia watu saba kwa tuhuma za wizi wa vipande vya shaba 650 yenye thamani ya Sh. 26,720,000 iliyokuwa ikisafilishwa kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuja bandari ya Dar es Salaam.
Aidha, Polisi imefanikiwa kukamata bastola mbili aina ya Glock 17 yenye namba LZD na usajili namba TZ CAR 98189 ikiwa na risasi 12 kwenye magazine.
Kamanda Kova alisema Jeshi la polisi limekamata pia SMG moja yenye namba 26081997 iliyokatwa kitako na mtutu ikiwa na magazine yake na polisi walipofanya msako kwenye nyumba ya watuhumiwa na kufanikiwa kukuta gari aina ya Suzuki Carry yenye namba za usajili T 289 BYL ambayo iliporwa Toangoma.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment