Tuesday, 9 April 2013

Ridhiwani adaiwa kuikoroga UVCCM


MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, anadaiwa kuandaa mpango wa mapinduzi ya uongozi ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Tanzania Daima limedokezwa.
Habari za ndani ya umoja huo zinasema kuwa mtoto huyo, Ridhiwani, ameanza mpango wake huo kwa kumwingilia Mwenyekiti wa UCCM, Juma Khamis Sadifa, katika utekelezaji wa majukumu yake.
Ridhiwani ambaye amekuwa akijipenyeza katika siasa za chama hicho kwa kutumia mgongo wa baba yake, anatajwa kuwa kinara wa mkakati mchafu unaolenga kutaka kumwondoa tena mwenyekiti wa UVCCM kwa mbinu zile zile alizozitumia kumwondoa mwenyekiti aliyepita, Yusuf Massauni.
Chanzo chetu kilisema kuwa Ridhiwani ambaye vilevile ni mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM taifa, anadaiwa kuwa msukaji wa mkakati wa kuwang’oa katika nyadhifa zao Sadifa, Makamu wake, Mboni Mhita na Katibu Mkuu wa UVCCM Martine Shigella.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya viongozi wa juu wa umoja huo, walieleza kuwa mwenyekiti wao kwa mamlaka aliyo nayo kikatiba, alifanya mabadiliko ya kawaida katika Idara ya Oganaizesheni ya jumuiya hiyo, kwa kumwondoa aliyekuwapo, Sofia Juma.
Baada ya Sofia kuondolewa katika wadhifa huo, alipeleka mashtaka kwa Ridhiwani kulalamika, na kwamba Ridhiwani alianza kumtumia ujumbe mfupi wa simu Sadifa, kumkemea kwa kitendo hicho na kumwamuru amrejeshe.

Habari zaidi zinabainisha kuwa, Sadifa alimwambia Ridhiwani kuwa si vizuri kujibizana naye kwa simu, hivyo kumtaka afike ofisini.
“Alipofika ofisini alikuta Sadifa amewaita wakuu wote wa idara, na alipokaribishwa aseme alitoa shutuma nyingi kuhusu utendaji wa mwenyekiti wetu, akisema ni mbaya,” kilisema chanzo hicho.
“Sadifa alimjibu Ridhiwani kuwa: umezoea kunipiga vita, uliandaa watu wa kunipokea kwa mabango, Mwenyekiti wa CCM ni baba yako si wewe, Rais wa Tanzania ni baba yako si wewe, na nilichokifanya kuhusu mabadiliko nimefanya kwa mujibu wa katiba.
Mimi ni Mwenyekiti wa UVCCM na mjumbe wa Kamati Kuu, kuanzia leo nakuamuru usije tena hapa ofisi za UVCCM, upaone kama kituo cha polisi,” alisema.
Baada ya majibizano hayo, inadaiwa kuwa Ridhiwani aliahidi kumshughulikia Sadifa kwa kupeleka malalamiko kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, akimwomba amwondoe madarakani kwa kuwa ana umri mkubwa, jambo ambalo ni aibu kwa chama na kwamba hana akili timamu.
“Kabla ya hatua zozote kuchukuliwa, Zakia Meghji alipata taarifa hizo na kuonya kuwa kitendo hicho kisifanyike, kwani Wazanzibari watakasirika sana na kufikiri kuwa Wabara hawapendi kuongozwa na Wazanzibari, kwani walimwondoa Yusuf Masauni kwa vigezo hivyo hivyo,” alisema mtoa taarifa.
Inadaiwa kuwa baada ya Ridhiwani kugonga mwamba kwa utaratibu huo, aliamua kumtumia, Salum Hapi, kuwafungulia mashtaka Sadifa na Mhita kuwa katika uchaguzi wao walishinda kwa rushwa ili wahojiwe na kamati ya maadili ya chama hicho leo asubuhi.
Hapi alikuwa mgombea wa Makamu Mwenyekiti na sasa ni mfanyakazi katika Kampuni ya uwakili ya RGK ya Ridhiwani Kikwete.
Alipotafutwa kuthibitisha mgogoro huo kwa simu jana jioni, Sadifa hakukubali wala kukanusha bali alisema kwa kifupi kuwa: “Hizo habari unazoniuliza si muda wake kuzizungumza, acha niende nikasikilize yale niliyoitiwa kesho.”
Aliongeza kuwa: “Kanuni za chama haziniruhusu kusema sasa, nikimaliza kuhojiwa huko ndipo nitasema kimejiri nini. Hata kama una mpango wa kumtafuta makamu wangu usimtafute kwa kuwa msemaji wa jumuiya ni mimi, lakini ni kweli kesho tutahojiwa.”
Ridhiwani hakupokea simu yake ya kiganjani, kwani iliita muda wote bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment