Wakati vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi vikiendelea kushika kasi nchini, mwanasaikolojia ameeleza kwamba vinachangiwa na hasira za muda mrefu kiasi cha kuwafanya watu kukata tamaa.
Aidha, mwanasaikolojia huyo, Dk. Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameeleza pia kwamba kukata tamaa huko (frustration) kunachangiwa na hali ya wananchi kutonufaika na rasilimali za nchi yao kwa kipindi kirefu.
Alisema hasira za muda mrefu kwa wananchi dhidi ya vyombo vya dola hususani Jeshi la Polisi pamoja na uvunaji wa rasilimali usiowanufaisha, unachangia 'uasi' wa wananchi unaosababisha kujichukulia sheria mkononi.
“Kila tukio (la kujichukulia sheria mkononi), lina maana yake. Ukiangalia kule Liwale ni korosho, Loliondo ni ardhi, Mtwara ni gesi, mauaji ya polisi kama kule Ngara na Rufiji ni hasira dhidi ya kutotendewa haki na vyombo vya dola na yote hii ni hasira za muda mrefu,” alisema.
Alisema kwenye maeneo kama Mtwara au Liwale, wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa
kuwa wameona hawanufaiki na rasilimali zinazowazunguka.
Dk. Mkumbo alisema hasira hizo zinaibuka zaidi kwa sababu wananchi wanahangaika kujitafutia ajira kama usafiri wa boda boda, lakini katika hali ya kushangaza vyombo vya dola vinachangia kuminya ajira hizo, jambo linaloamsha hasira.
“Kwamba ajira hakuna, halafu watu wamehangaika hadi wamejiajiri au wamelima, lakini bei waliyoahidiwa hawaipati kwa hiyo wanaona njia pekee ni kupambana na wale wanaozuia malengo au mafanikio yao,” alisema.
Dk. Mkumbo alisema ili kumaliza hali hiyo, ni lazima wenye mamlaka watimize wajibu wao kikamilifu.
Kauli hiyo ya Dk. Kitila Mkumbo inakuja wakati ambao matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yamekithiri nchini.
Katika matukio ya hivi karibuni, ni lile la mwishoni mwa mwaka jana lililosababisha askari wawili wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera, kuuawa na wananchi wenye hasira kali.
Mauaji hayo yalifanyika baada ya wananchi hao kuvamia na kukichoma moto kituo cha polisi cha Mugoma wilayani humo kufuatia askari hao kudaiwa kumpiga risasi fundi wa pikipiki.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea mchana wakati askari kadhaa wa kitengo cha usalama barabarani walipofika kwa fundi pikipiki huyo na kutaka kuichukua pikipiki aliyokuwa akiitengeneza kwa madai kuwa ilikuwa na makosa.
Habari zilisema kuwa fundi huyo aligoma na kueleza kuwa asubiriwe mwenye pikipiki ili kuepuka kudaiwa chombo hicho cha usafiri.
Baada ya mvutano wa muda mfupi, askari hao walifyatua risasi na kumpiga fundi huyo mguuni na kifuani, hivyo kusababisha kifo chake.
Tukio hilo liliwapandisha hasira wananchi na kuwafukuza askari hao waliokimbilia katika kituo hicho cha polisi na ndipo waliamua kukichoma moto hatua iliyosababisha askari waliokuwamo kutoka na kukimbia kila mmoja na muelekeo wake.
Hata hivyo, Koplo Paschal alianguka wakati akijinusuru, hivyo kuvamiwa na wananchi waliokuwa na zana mbalimbali za jadi ambazo walizitumia kumshambulia na kumuua papo hapo.
Wananchi hao pia wanadaiwa kumfuata askari mwingine anayetajwa kwa jina la PC Alex aliyekuwa amekimbilia kwenye nyumba ya mwananchi mmoja na kumtoa kwa nguvu na kisha kuanza kumshambulia hadi kumuua.
Katika tukio hilo, nyaraka mbalimbali ziliteketea vikiwamo vizibiti kama pikipiki na baiskeli zilizokuwa kituoni hapo.
Mapema mwezi huu, raia walivamia kituo cha polisi Kawe jijini Dar es Salaam na kuharibu mali pamoja na nyaraka kituoni hapo baada ya watu wanasadikiwa kuwa ni wanajeshi waliotuhumiwa kumuua dereva wa bajaji, Yohana Cyprian kupelekwa kituoni hapo.
Tukio hilo lilisababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wakishinikiza polisi wamwachie mtuhumiwa ili wamuue.
Katika tukio hilo, watu 12 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
MTWARA
Tukio la Kawe lilitokea wiki kadhaa baada ya polisi mkoani Mtwara kulazimika kupiga mabomu ya machozi kutwa nzima katika kata ya Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani kutawanya wananchi walioizingira nyumba ya diwani wa kata hiyo, Mohamedi Chehako, kwa madai ya kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.
Wananchi hao waliokuwa na hasira walichoma moto Mahakama ya Mwanzo na kuvunja vioo vya nyumba za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na ya Mohamed Said Sinani ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara.
Wakiwa katika mahakama ya mwanzo, polisi walizingirwa na vijana waliokuwa wamebeba mawe na kufunga barabara zote za kuingia na kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi na eneo la Soko Kuu, licha ya kufyatua hewani mabomu ya machozi.
Hayo yalitokea huku mkoa wa Mtwara ukiwa umeshuhudia maandamano na mapigano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, kutokana na msimamo wa wananchi kupinga uamuzi wa serikali wa kutaka kuisafirisha gesi asilia kutoka mkoani humo na kuipeleka Dar es Salaam kwa njia ya mabomba.
DUMILA
Tukio la Mtwara lilitokea siku ambayo vurugu kubwa zilikuwa zimezuka katika eneo la Dumila mkoani Morogoro baada ya wananchi kuchoma moto nyumba na kupasua vioo vya magari na hivyo kuzuia magari yote yanayotumia barabara hiyo, kwa madai kuwa wanapinga agizo la Mkuu wa Wilaya hiyo la kuwanyang'anya ardhi wakulima na badala yake kupewa wafugaji.
Vurugu hizo zilisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa.
KIBITI
Tukio lingine ni lile la wananchi wenye hasira kuvamia kituo cha Polisi Kibiti Wilayani Rufiji na kuleta vurugu kubwa kufuatia raia mmoja kufa kwa kile kilichodaiwa kipigo cha polisi.
Vurugu hizo zilitokea baada ya kijana Hamis Mpondi aliyedaiwa kupigwa na polisi kufariki wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Muhimbili.
Wananchi hao waliteketeza nyumba za askari polisi hao zilizopo jirani na kituo hicho, licha ya juhudi za polisi kuwatawanya kwa mabomu.
Aidha, wananchi hao walifunga barabara kuu ya Kilwa iendayo mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara kwa mawe, magogo na kuchoma matairi umbali wa kama kilometa moja kutoka kituo cha Polisi Kibiti.
MWANZA
Tukio jingine ni lile la mkoani Mwanza, ambako Polisi walazimika kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waendesha bodaboda waliokuwa wakiwalazimisha askari wawaachie wenzao waliowakamata kwa makosa mbalimbali.
Ghasia hizo ziliibuka wakati polisi wa usalama barabarani na kikosi maalumu cha ukaguzi wa magari walipofanya doria kukagua leseni na uhalali wa madereva hao wanaofanya shughuli za kusafirisha abiria.
Vurugu hizo zilianza baada ya polisi kuwakamata waendesha bodaboda wapatao 26, ambao walitozwa faini za papo kwa papo kulingana na makosa yao, huku wengine wakiendelea kushikiliwa.
Hatua hiyo iliwafanya waanze kujikusanya kutoka sehemu mbalimbali na kuandamana hadi eneo kulikokuwa limetengwa kwa ukaguzi huo katika mtaa wa Mission.
Baada ya kufika eneo hilo, walianza kuwarushia mawe askari hao, huku baadhi yao wakiendesha pikipiki kuzunguka eneo hilo na kuzuia magari kupita hali iliyozua tafrani.
Baada ya kutokea hivyo, askari hao walilazimika kuwaita askari wengine ili kuwakabili vijana hao.
Vurugu hizo zilizodumu kwa saa tatu, zilisababisha kufungwa kwa barabara iendayo Uwanja wa Ndege na katika eneo la Pasiansi, huku baadhi ya abiria wakilazimika kuteremka katika daladala na kukimbia ovyo na wengine kulala katika mifereji ya maji machafu baada ya milio ya risasi na mabomu ya machozi kuanza kurindima.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment