Monday, 15 April 2013

Wakuu wa shule waagizwa kuwanyang’anya simu wanafunzi


Serikali imewaagiza wakuu wa shule za sekondari nchini kuchukua hatua kali dhidi ya wanafunzi watakaobainika kumiliki simu za viganjani na kuwanyang’anya na kisha kuziteketeza kwa moto au kuzitupa chooni.
 
Agizo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanika katika kijiji cha Totowe wilayani chunya.
 
Alisema sheria haiwaruhusu wala kuwapa haki wanafunzi kumiliki simu wakiwa shuleni, hivyo mwanafunzi anayekwenda na simu shuleni anakuwa amevunja sheria na taratibu za shule ambazo zinamzuia kumiliki na kutumia masomoni.
 
“Nawaagiza walimu kuwa ukimwona mwanafunzi ana simu na kuitumia nyakati za masomo, mnyang’anye na kuichoma moto au kuitupa chooni kwa sababu wakati mwingine simu hizo wanakuwa wamenunuliwa na wapenzi wao na hivyo kuwafanya washindwe kusoma vizuri na matokeo yake wanafeli mitihani, sisi Wizara ya Elimu hatujaruhusu na wala hatufanyi hayo mambo,” alisema Mulugo. 
 
Alisema akitokea mzazi akalalamika au kumsumbua mwalimu kutokana na kunyan’anya mwanae simu akiwa shuleni, maofisa watendaji wa vijiji na mitaa wamchukulie hatua za kumkamata na kumpeleka Polisi ili afikishwe mahakani.
 
Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songwe wilayani Chunya, alisisitiza kuwa wanafunzi wakiachwa bila kudhibitiwa nidhamu zao, ndio cha kushindwa kusoma na kupata matokeo mabovu kwenye mitihani ya kitaifa na baadae kuharibikiwa kimaisha.
 
Alisema vijana ambao hawadhibitiwi nidhamu wawapo shuleni ndio wanaoshindwa kufanya vema masomo yao na baadaye kuwa mzigo kwa taifa kutokana na kujihusisha na mambo ya hovyo kama vile maandamano yasiyo na tija, utumiaji wa dawa za kulevya na uhalifu mwingine kwenye jamii.
 
Aidha, Mulugo aliwataka walimu kuanza kutembeza bakora kwa wanafunzi watukutu ili kuhakikisha nidhamu ya wanafunzi inarejea mashuleni na kuwafanya watoto warejee kwenye masomo badala ya kujihusisha na mambo ya hovyo.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment