Majambazi wawili wamempora raia mwenye asili ya Kiasia fedha ambazo kiwango chake hakijafahamika, baada ya kumjeruhi mkononi kwa risasi.
Tukio hilo lilitokea maeneo ya Upanga Sea View karibu na ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam jana majira ya saa 9 alasiri.
Watu walioshuhudia tukio hilo, waliliambia NIPASHE kuwa majambazi hao walifika katika eneo hilo, huku kila mmoja akiwa amepanda pikipiki na kuziegesha karibu na kituo cha mafuta cha Puma kinachotazamana na ofisi za shirika hilo.
Mashuhuda hao, ambao walikuwa wakiendelea na shughuli za ujenzi, walisema wakati wakiendelea na shughuli yao, ghafla walisikia sauti ya mlio wa risasi na kudhani kwamba, kulikuwa na kunguru aliyepigwa 'shoti' ya umeme. Walisema mara baada ya mlio huo, waliwaona majambazi hao wakikimbia huku wakiwa wamebeba mkoba mkononi na kuelekea eneo la Ocean Road walikotokea.
Mashuhuda hao walisema majambazi hao walipotoweka, walimwona mtu aliyeporwa akiwa ndani ya gari lake kwenye msongamano barabarani akipiga kelele kuomba msaada.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, majambazi hao walifyatua risasi, ambayo ilivunja kioo cha gari na kupenya na kutoboa kidole cha mkono cha mtu huyo.
Walisema dakika chache, askari polisi walifika eneo hilo na kumsikiliza mtu huyo na baadaye likaja gari la kubeba wagonjwa na kumchukua na kisha kumpeleka hospitali.
Hata hivyo, walisema hawakujua ni hospitali gani aliyopelekwa mtu huyo kwa kuwa waliogopa kusogelea eneo hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi jana, mara zote ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment