UJIO wa Rais Barack Obama wa Marekani nchini, umezua machungu kwa baadhi Watanzania baada ya serikali kusihi abiria kutoka mikoani waahirishe safari za kwenda jijini Dar es Salaam.
Mbali ya hiyo, ujio huo pia umekuwa shubiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake kutokana na kuvurugika kwa shughuli za baadhi ya watu wanaojitafutia riziki.
Akizungumza kwenye kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa hewani na Radio Clouds FM, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe aliwataka watu wanaokaa nje ya Dar es Salaam wenye nia ya kwenda jijini humo kuahirisha safari zao.
Membe aliwataka waahirishe safari hizo katika kipindi ambacho Obama atakuwepo hapa nchini ili kuepuka usumbufu watakaoupata.
Alisema kuanzia leo taifa litapokea ugeni wa watu 2,700 kutoka mataifa mbalimbali duniani watakaohudhuria mikutano mitatu tofauti, ukiwemo ujio wa kihistoria wa Rais Obama na wake wa marais kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ugeni mwingine utatokana na wajumbe wa mkutano wa ubia wa wazi ‘Smartpartinership Dialogue’.
Rais Obama anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi na ujumbe wa watu 700, wakiwemo waandishi wa habari 200 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Membe, katika kipindi cha takribani wiki moja, Jiji la Dar es Salaam litakuwa na usumbufu mkubwa utakaozifanya baadhi ya barabara kufungwa na hoteli kubwa zitakuwa zimefurika wageni hao.
“Nawaomba wananchi wasio na ulazima wa kuja Dar es Salaam katika kipindi hiki kuahirisha safari zao, maana mji huu utakuwa na pilika nyingi sana, baadhi ya barabara zitafungwa, magari mengine hayataingia katikati ya jiji, hoteli nyingi zitakuwa zimefurika wageni, ulinzi utaimarishwa,” alisema Waziri Membe.
Tayari ulinzi umeimarishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo majengo marefu kwa kufungwa kamera ambazo zitakuwa zikirekodi matukio mbalimbali yanayoweza kutokea.
Kuhusu mkutano wa ubia wa wazi, Membe alisema lengo ni kujadiliana jinsi ya kutumia teknolojia katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuziletea nchi hizo maendeleo.
“Tunapozungumzia kuhusu Watanzania kuwa wanakabiliwa na umasikini, ni kweli. Lakini hali hiyo inatokana na uwezo wetu katika matumizi ya sayansi na teknolojia,” alisema Membe.
Alisema katika majadiliano hayo kutakuwa na makundi ya wataalamu wa fani za kila aina ambao watachambua kwa undani agenda mbalimbali na kuzipatia majibu kwa ajili ya utekelezaji wake hapo baadaye.
“Kutakuwa na makundi kama vile, la wataalamu wa gesi, madini na mafuta. Pia kutakuwa na kundi la sayansi na teknolojia, hususan katika upande wa kilimo na mengine, yote hayo yatakuwa na agenda zake,” alisema Membe.
Aliongeza kuwa baada ya wataalamu hao kumaliza majadiliano hayo, itatangazwa duniani kote kile kilichojadiliwa katika mkutano huo pamoja na maazimio yake.
Mandhari yabadilika
Baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kwa takriban wiki moja sasa yamekuwa kwenye pilikapilika kubwa ya usafi ikiwemo kuwafukuza wafanyabiashara mbalimbali kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.
Wafanyabiashara ndogo ndogo, wakiwemo mama ntilie, washona viatu, ni miongoni mwa walioonja shubiri ya kukamatwa au kutimuliwa kwenye maeneo waliyozoea kufanyia biashara.
Katika hatua nyingine, watu waliokuwa katika kituo cha mabasi ya Posta Mpya jana jioni walikuwa katika wakati mgumu baada ya gari la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii lenye namba DFP 8132 aina ya Toyota Land Cruiser, Pick Up, kupita katika eneo hilo na kumwaga dawa ya kuua mbu na wadudu wengine.
Baada ya gari hilo linalomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupita na kumwaga dawa, wananchi wengi walianza kukohoa huku wakifikicha macho kutokana na dawa hiyo kuwawasha machoni.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi yao walisema ingawa suala la kupata mgeni ni la faraja kwa mwenyeji, lakini kwao limekuwa tofauti huku wakilaumu utaratibu wa kuboresha mazingira kwa sababu ya ugeni.
Wamachinga wazungumza
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jana kwa sharti la majina yao kuhifadhiwa kwa sababu za kiusalama, wauza magazeti na wamachinga, walisema kuanzia jana wametangaziwa kuondoka katika maeneo yao ya biashara.
Walilaani hatua hiyo na kueleza kwamba inashangaza na kuwaweka katika hali ngumu kimaisha wakati siku zote wamekuwa wakifanya kazi zao bila tatizo na wala kumbughudhi mtu.
“Uongozi wa kituo cha Mwenge umetuamuru kuondoa meza zetu za magazeti na kutofanya kazi hii hapa tangu leo kwa ajili ya ujio wa Obama, wanasema tunasababisha uchafu.
“Hili si sawa kabisa kwani magazeti ni kitu muhimu kwa umma, na siku zote tunafanya biashara hii hadi Ikulu, sasa kwa nini watusumbue?” alihoji muuuza magazeti mmoja na kuongeza kuwa gazeti halina uchafu, hivyo hali hiyo haileti usawa hata kidogo.
Mwingine alieleza kuwa baada ya kuhoji sababu ya wao kuondolewa, ndipo walipoambiwa kwamba ni kutokana na ujio wa Rais Obama, na wakaelezwa kwamba wataruhusiwa kuendelea na biashara yao baada ya kiongozi huyo kuondoka.
Mwingine alisema hatua ya kuwaondoa ni kudhalilisha vyombo hivyo vya habari ambavyo vimekuwa vikihabarisha jamii kila siku na kueleza kwamba haijawahi kutokea wakafanyiwa hivyo.
“Baada ya wao kutuambia, sisi tulitii amri na kuondoa meza zetu na kuyashika magazeti mikononi, lakini waliobaki waliondolewa kwa nguvu,” alisema muuza magazeti mwingine.
Tanzania Daima ilipomtafuta msimamizi wa kituo hicho cha mabasi cha Mwenge, aliyejulikana kwa jina moja la Kessy ili kuzungumzia suala hilo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya kiganjani kwa mara kadhaa iliita bila majibu.
Kikwete ashitakiwa kwa Obama
Katika hatua nyingine, kamati ya kuwalinda waandishi wa habari barani Afrika (CPJ), imemwandikia barua Rais Obama ikimuomba amuulize Rais Jakaya Kikwete juu ya kukandamizwa kwa uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.
Barua hiyo ya Juni 25 iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ, Joel Simon na nakala yake kutumwa sehemu mbalimbali ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), inamtaka Obama ajue na azungumzie masuala mbalimbali ya unyanyasaji kwa vyombo vya habari, na waandishi nchini Tanzania.
Sehemu ya barua hiyo kwa Obama imeandikwa; “Katika mikutano yako na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, tunaomba kwamba mjadili umuhimu mkubwa wa uhuru wa habari kwa maendeleo ya kiuchumi na demokrasia, kwani CPJ ina kumbukumbu ya kupanda kwa vitisho na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari nchini Tanzania.”
Mandela afunika ziara ya Obama
Habari kutoka jijini New York, Marekani zinasema kuwa safari ya Rais Obama nchini Afrika Kusini imejikuta ikiwekewa kiwingu na hali ya afya ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela ambaye amelazwa katika hospitali ya Pretoria karibu wiki tatu sasa.
Obama aliyeanza jana safari yake ndefu ya barani Afrika katika nchi za Senegal, Afrika Kusini na Tanzania ziara yake imefunikwa na taarifa za maendeleo ya afya ya Mandela.
Wafuatiliaji wa mambo barani Afrika wanasema kuwa kutokana na utete wa afya ya kiongozi huyo maarufu duniani, Rais Obama alipaswa kuahirisha ziara yake kwani atashindwa kutawala vyombo vya habari iwapo Mandela atafariki wakati akiwa katikati ya ziara hiyo.
Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Ikulu ya Marekani imeeleza kuwa Rais Obama hataweza kwenda hospitalini kumjulia hali Mandela (94) kutokana na hali yake ya kiafya kuwa mbaya.
Akiweka sawa kuhusu hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Maite Nkoane Mashebane alibainisha kwamba Obama alipenda kumjulia hali Mandela, lakini hataweza kuonana na kiongozi huyo wa zamani wa Afrika kusini kutokana na afya yake kuzidi kuzorota.
Kwa mara ya mwisho kukutana kwa Obama na Mandela ilikuwa mwaka 2005, wakati ambao Mandela alikwenda Washington na Obama alikuwa ameteuliwa kuwa seneta. Wawili hawa walipata nafasi ya kuzungumza kwa muda mrefu.
Tangu mwaka huo Mandela hajawahi kuonana na Obama uso kwa uso hata alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani kwa mara ya kwanza mwaka 2008.
Kutokana na afya yake kuwa tete, jana Mandela alifanyiwa maombi ya ‘mwisho mwema’ na Askofu mkuu wa kanisa la Kianglikana la mjini Cape Town, Afrika Kusini, Thabo Makgoba.
Maombi hayo yamefanywa wakati familia ya Mandela imekutana nyumbani kwake huko Kunu, huku hali yake ya afya ikizidi kuzorota hospitalini, Pretoria.
Maombi hayo yalitolewa baada ya askofu huyo kumtembelea Mandela hospitalini ambako kiongozi huyo wa zamani amelazwa baada ya kuugua mapafu.
Katika hali ya kutia wasiwasi majaliwa ya Mandela, kuna taarifa kuwa wajukuu wa rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini wameanza kukutana nyumbani kwake kijijini katika Jimbo la Eastern Cape, ambako viongozi wa kitamaduni pia wamealikwa huku helikopta za jeshi zikionekana zikipaa karibu na nyumbani kwa Mandela
No comments:
Post a Comment