Wednesday, 26 June 2013

SMZ yataka Wazanzibari wanaoishi Bara wasitishwe

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud, amewataka wasomi, wanasiasa na viongozi kuacha kuwatisha wananchi wanaoishi Tanzania bara kuwa watafukuzwa kama Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavujika.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia makadirio na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachofanyika Chukwani mjini hapa.

Alisema  baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiingilia  mchakato wa rasimu ya mabadiliko ya Katiba kama kuwatisha ikiwamo kusema Wazanzibari watafukuzwa Bara kama Muungano utavujika.

Alisema muhimu viongozi na wasomi kuwapa nafasi wananchi watoe maoni yao kwa uwazi na siyo mwafaka kuanza kuwatisha.

Othman alisema Wazanzibari wanaoishi Bara ni wachache kuliko Wakenya, Waganda ama Wanyarwada na wanaiishi wakati wao hawamo katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kwa upande wake,  Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, Nassor Salim Ali, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar, kuacha tabia ya kuwasemea wananchi aina ya mfumo wa Muungano wanaoutaka kwa kuwa Katiba ni jambo la wananchi na siyo jukumu la vyama vya siasa.

Aidha, alisema wananchi wa Tanzania Zanzibar, bado wanaupenda Muungano kwa sababu umefanikiwa kujenga misingi ya amani na umoja wa kitaifa baina ya pande mbili za Muungano.

Aliwataka viongozi wa kisiasa kuacha tabia ya ndumilakuwili.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment