MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma imetupilia mbali mashitaka yaliyokuwa yamefunguliwa na serikali dhidi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) kwa madai ya kumtukana Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Eliezel Luvanda alitupilia mbali mashitaka hayo kutokana na hati ya mashitaka dhidi ya mbunge huyo kuwa na upungufu.
Luvanda alisema kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 132 (20) hati hiyo haikuwa na maelezo ya kutosheleza kuonesha ni lugha gani iliyodaiwa kuwa ni ya matusi aliyotumia mshitakiwa huyo dhidi ya Pinda.
Awali akisoma hati hiyo, Mwendesha Mashitaka, Hariet Lopa alidai kuwa Juni 24 mwaka huu akiwa katika Manispaa ya Dodoma, Mbilinyi aliweka ujumbe wenye lugha ya matusi dhidi ya Waziri Mkuu Pinda kinyume cha sheria.
Kabla ya hakimu kutoa hukumu hiyo, wakili na mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lisu, aliwasilisha utetezi wake mbele ya mahakama hiyo akiitaka kuitupilia mbali kesi hiyo kwa vile hakuna matusi yanayotajwa yakidaiwa kutolewa na mbunge huyo dhidi ya Pinda.
Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 132 (20), hati hiyo haikuwa na maelezo ya kutosheleza kuonesha ni lugha gani iliyotumika na ni matusi gani, hivyo haiwezi kuwa kesi ambayo inaweza kuendelea kusikilizwa.
Lissu alidai kuwa maneno yanayodaiwa yangesababisha uvunjifu wa amani hayakutajwa katika hati hiyo huku akihoji upande wa mashitaka unataka Sugu ajitetee kwa shitaka lipi.
Aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa kama hati hiyo ya mashitaka iliyopelekwa mahakamani hapo itaendelea kutumika, itakuwa imekiuka sheria, hivyo akaitaka mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo.
Hakimu Luvanda alipomtaka mwendesha mashitaka wa serikali kujibu hoja ya Lissu, alishikilia msimamo wake na kuiomba mahakama kuendelea kuisikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa ni mpya, hivyo makosa ambayo yapo yatafanyiwa marekebisho wakati shauri likiendelea.
Hata hivyo Lissu alipinga kauli ya mwanasheria wa serikali kwa madai kuwa hati ya mashitaka ni chafu na imeandaliwa ovyo, hivyo mahakama kukubali kuendelea kusikiliza kesi hiyo ni kosa na hivyo ni vyema ikatupiliwa mbali.
“Mheshimiwa hakimu naomba kesi hii itupiliwe mbali kwa kuwa hati ya mashitaka ni chafu na ni ya ovyo. Naomba itupiliwe mbali na mtuhumiwa aachiwe huru,” alisema Lissu na kuongeza kuwa wapo tayari hata kesho kuendelea na kesi hiyo ikiwa serikali itaandaa hati sahihi.
Hata hivyo, baada ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka alidai wataendelea na upelelezi na ukikamilika wataandaa hati mpya.
Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo, Lissu alisema mahakama hiyo imetenda haki na kama upande wa mashitaka haukuwa umeridhika na hukumu hiyo, ujipange upya na kupeleka hati ya mashitaka.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) alisema hata hivyo kufutwa kwa kesi hiyo hakumaanishi mteja wake hawezi kushitakiwa tena, kwani bado Waziri Mkuu Pinda anaweza kwenda polisi kutoa maelezo kama anaona kweli ametendewa kosa hilo.
Kwa upande wake, Sugu baada ya kuachiwa huru alisema kuwa anachoshauri ni Pinda kujitafakari upya juu ya kauli zake anazozitoa hasa kuhamasisha watu kupigwa.
Awali, Sugu alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma kuwa aliweka ujumbe mfupi katika mtandao wa kijamii ambao ulikuwa unamtusi Waziri Mkuu Pinda.
Hata hivyo, alikuwa akipelekwa katika kituo cha polisi cha kati kwa mahojiano na jana ilikuwa ni mara ya kwanza kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment