Saturday 15 June 2013

Wakenya wizi wa NMB Mwanga jela miaka 67

WAKENYA wawili na Mtanzania mmoja wamehukumiwa kifungo cha miaka 67 jela baada ya kupatikana na hatia ya kula njama na kupora sh milioni 239 za benki ya NMB tawi la Mwanga, Kilimanjaro.
Mbali na uporaji huo, watu hao waliiba bunduki aina ya SMG mali ya Jeshi la Polisi nchini.
Wakenya hao ni Samwel Gitau Saitoti na Michael Joseph Kimani na Mtanzania Elizabert Msanze maarufu kwa jina la Bella aliyekamatwa na washitakiwa hao eneo la Njiro, mkoani Arusha Julai 2007.
Uporaji huo ulifanyika Julai 11, 2007 ambako sh 239,490,000 ziliporwa ikiwemo kuuawa kwa mmoja wa askari polisi PC Michael Milanzi aliyekuwa lindo.
Jopo la mahakimu watatu; Panterine Kente aliyekuwa kiongozi, Aziza Temu na John Nkwabi, liliwaachilia huru washitakiwa wengine wanne.
Walioachiwa huru ni ndugu watatu; Devota Elias Msenza, Ntibasana Elias Msenza na Julian Elias Msenza na mtu mwingine Calist Kanje baada ya kutowakuta na hatia katika mashitaka yote matatu.

Akisoma hukumu hiyo iliyoanza saa saba mchana hadi saa 9:30 jioni, hakimu Kente alitumia muda mwingi katika marejeo ya kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na kutupilia mbali ushahidi wa utambuzi wa baadhi ya washitakiwa wakati wa gwaride.
Hakimu huyo alizingatia hati ya ungamo la mshitakiwa wa kwanza Samwel Gitatu Saitoti ambalo alielezea jinsi walivyopanga tukio hilo na walivyotekeleza uporaji.
Katika hukumu hiyo, washitakiwa walihukumiwa miaka saba kwa kosa la kwanza ambalo ni la kula njama huku wakihukumiwa miaka 30 kila mmoja kwa kosa la uporaji na miaka 30 kwa kosa la wizi wa silaha.
Hata hivyo hakimu huyo alisema adhabu hizo zinaenda pamoja hivyo washitakiwa watatumikia kifungo cha miaka 67 jela.
Kabla ya hukumu hiyo, wakili wa serikali Tamali Mndeme aliomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.
Washitakiwa wengine katika shitaka la mauaji ya PC Milanzi ni Deodat William Temu (39), Emmanuel Mziray (36), Florian Kimati (37), askari aliyekuwa lindoni kwenye benki hiyo PC. 
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment