MKAZI wa Tarime, Bhoke Ghati, amempiga hadi kumuua binti yake Neema Ghati (14) kwa madai ya kutoroka nyumbani.
Neema aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Mazoezi Buhemba mjini Tarime, alifikwa na mauti hayo jana wakati akiadhibiwa kwa madai ya kutoroka nyumbani kwa siku nne.
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya alisema mama wa mtoto huyo anashikiliwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa kamanda huyo na baadhi ya majirani wa Bhoke, Neema alirejeshwa nyumbani na Wasamaria waliomwacha na mama yake huyo baada ya kukutwa mitaani, akihofia kurudi kwao.
Mashuhuda hao walilieleza gazeti hili kwamba baada ya mtoto huyo kukabidhiwa kwa mama yake alimtoroka tena akikwepa adhabu.
Ilidaiwa kuwa baada ya Bhoke ambaye ni mjamzito kumkamata mtoto huyo alianza kumpiga hadi kupoteza maisha kisha kuanza kulia akiomba msaada kwa majirani ambao walipiga simu polisi.
Baada ya askari polisi kufika, walimkamata Bhoke na kumpeleka kwenye kituo cha polisi bomani huku mwili wa mtoto huyo ukipelekwa kwenye hospitali ya wilaya kwa ajili ya kuuhifadhi.
No comments:
Post a Comment