Thursday, 4 July 2013

`Hakuna mashine za kutambua dawa za kulevya Uwanja wa Ndege Z`bar`

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Fereji, amesema mashine za ukaguzi katika Uwanja wa Ndege  wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, hazina uwezo wa kutambua dawa za kulevya zinazosafirishwa ama kuingizwa nchini.
 
Alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni, Jaku Hashim Ayoub wakati wa kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani mjini hapa.

Alisema hatua hiyo imesababisha msafirishaji au muingizaji kukamatwa akiwa tayari katika chumba cha kuondokea abiria baada
ya kukaguliwa mizigo na kuruhusiwa.
 
Alisema mashine zilizopo zina uwezo wa kutambua vifaa vya vitu hatari kama vile visu na silaha nyingine.
 
“Katika siku za hivi karibuni, tumeanza kushuhudia matukio mbalimbali ya wasafirishaji wa dawa za kulevya wakikamatwa tayari wakiwa katika chumba cha kuondokea baada ya kukaguliwa mizigo na kuruhusiwa kuendelea na safari,” alifafanua.
 
Alisema hiyo ni changamoto katika suala zima la vita dhidi ya dawa za kulevya katika maeneneo ya viwanja vya ndege na wizara yake itaendelea kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
 
Mwakilishi huyo alitaka kufahamu sababu za wasafirisha wa dawa za kulevya kukamatwa wakiwa tayari katika chumba cha kuondokea baada ya kukaguliwa mizigo na kuruhusiwa na maafisa wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar.

No comments:

Post a Comment