MFANYABIASHARA, Heaven Kassia (44), mkazi wa Bahari Beach jijini Dar es Salaam, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kwa kosa la kuwagonga kwa gari makusudi watu sita kutokana na kile kinachodaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Juni 30, mwaka huu, katika baa iitwayo Kilongawima Resort wakati mtuhumiwa akiwa na rafiki yake wa kike aitwaye, Jovita Njunwa ambaye pia ni mfanyabiashara.
Kova alithibitisha kuwa mfanyabiashara huyo akiwa katika baa hiyo na rafiki yake huyo wa kike, meza ya pembeni walikuwepo watu sita, ambapo baadaye Njunwa alihama kutoka katika meza yake na kwenda kukaa nao.
Kwa mujibu wa Kova, baada ya Njunwa kuhamia meza hiyo ilizuka tafrani kubwa kati ya Kassia na watu hao sita, kiasi cha kuanza kurushiana maneno makali yenye ishara ya kumgombea mwanamke huyo.
Alisema kuwa wakati huo Kassia alikuwa akidai kuwa rafiki yake amekwisha mgharamia Njunwa fedha nyingi, hivyo kuwataka wanaume hao wamwache bila maelewano.
Kova alisema kitendo hicho kilisababisha Kassia kuwasha gari lake lenye namba za usajili T 546 BXX aina ya Toyota Hilux na kuondoka kwa mwendo wa kasi kuelekea katika ile meza ya wanaume hao na kuwagonga kwa nguvu kiasi cha kuwasababishia majela sehemu mbalimbali za miili yao.
Aliongeza kuwa watu hao walivunjika miguu, mbavu na kuumia vichwani, hivyo kukimbizwa katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako wamelazwa wakiwa mahututi.
Kova aliwataja majeruhi hao kuwa ni Solomon Kirato, Peter Marwa, Yahaya Albert, Noah na wengine ambao majina yao hayakufahamika.
Kwa mujibu wa Kova, mtuhumiwa amekamatwa na uchunguzi unaendelea kuhusu kosa hilo la kutaka kuua kwa makusudi pamoja na kosa la kujaribu kujiua baada ya tukio hilo.
Alisema kuwa mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya jalada kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
No comments:
Post a Comment