JESHI la Polisi limemuua mtuhumiwa wa ujambazi , Lembris Taiko, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30-35, maarufu kama Dk. Mbushi, wakati wa majibizano ya risasi, tukio lililotokea nyumbani kwa mtuhumiwa huyo Mtaa wa Onjaftian Sokon One.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa, Liberatus Sabas, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tano asubuhi ambapo mtuhumiwa huyo anayefahamika kama Jenerali au Muarusha alikutwa na silaha aina ya bastola aina ya Bereta, ikiwa na risasi moja ambayo ilikuwa imefutwa namba zake.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu na jeshi hilo kutokana na kuhusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha uliotokea Agosti 26, 2012 ambapo alishirikiana na wenzake kupora bastola na kumjeruhi polisi mguuni kwa risasi.
Kamanda Sabas alisema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ukisubiri ndugu zake waweze kuutambua.
Alisema jeshi hilo linaendelea kumtafuta mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa huyo, aliyefahamika kwa jina moja la Swalehe, maarufu kama Baba Amir ili aeleze mahusiano yake na mtuhumiwa huyo.
Akielezea namna walivyoweza kumnasa mtuhumiwa huyo wa ujambazi, Kamanda Sabas alisema kuwa siku ya tukio majira ya saa moja asubuhi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watuhumiwa watatu wa ujambazi wameingia kwenye nyumba ya Swalehe.
“Mara baada ya kuizingira polisi walijaribu kuingia ndani na kuwataka watu wote waliokuwa ndani ya nyumba hiyo wajisalimishe. Ghafla ilifyatuliwa risasi kutoka ndani kupitia ukutani na kumkosa askari mmoja, hali iliyowalazimu polisi kujibu mapigo na kufanikiwa kumuua mtu mmoja aliyekuwa akifyatua risasi kwa kutumia bastola,” alisema Kamanda Sabas.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment