Friday, 26 July 2013

Vipato vya wasanii, umaarufu na dawa za kulevya

MATUKIO ya wasanii na vijana mbalimbali wa Kitanzania kukamatwa na dawa za kulevya ndani na nje ya nchi, yameendelea kutikisa huku kukikosekana jawabu la hatima yake.
Katika siku za nyuma, matukio haya yalikuwa kama uvumi tu, lakini kwa sasa si siri tena na majina yamekuwa yakitajwa waziwazi, huku mengine yakihusishwa na mizigo ya dawa yenye uzito na gharama kubwa sana, kiasi cha kutia shaka juu ya walioko nyuma ya biashara hizi.
Inatia shaka, kutokana na ukweli kwamba si rahisi kwa wasanii hawa kujitwisha mizigo hii ya mabilioni na kuanza kuzunguka nayo pande mbalimbali za dunia, bila kuwa na mkono mnene unaowatetea na kuwapa uhakika wa usalama wao.
Kama alivyosikika akisema Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, hivi karibuni, ni wazi biashara hii imezungukwa na vigogo wakubwa, ambao kutokana na ushawishi wao, imekuwa ni rahisi kuwaingiza wasanii na vijana wengi katika mtego huu.
Akizungumzia hivi karibuni nchini China, wakati wa ugeni wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana na ujumbe wake, Balozi wa Tanzania nchini humo aliyehamishiwa Ujerumani kwa sasa, Philip Marmo, anasema kwamba kuna vijana zaidi ya 100 wa Kitanzania waliomo kwenye magereza mbalimbali nchini China kutokana na biashara hii haramu.
Anaongeza kwamba, wengi wa vijana hawa, tayari wamekwisha kuhukumiwa kunyongwa, ingawa kutokana na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na China, wengi wamebadilishiwa vifungo vyao na kuwa vya maisha, huku vikiambatana na kazi ngumu.
Ripoti za aina hii haziko katika nchi ya China tu, bali mataifa mbalimbali duniani na kumekuwa na ripoti nyingine za kimataifa zikiitaja Tanzania kama lango kuu la biashara hii haramu ya dawa za kulevya.

Ni bahati mbaya kwamba, katikati ya wingu zito la dawa hizi za kulevya, wasanii wa Kitanzania wamejikuta kwenye mzingo tata wa kubebwa na kokoro hili.
Wasanii wamebebwa na kokoro hili katika mazingira mawili, kwanza wao wenyewe kuhusika moja kwa moja katika matumizi yake na pili kuyabeba kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kuyauza.
Orodha ya wasanii ambao wamekuwa wakihusishwa na matumizi ya dawa za kulevya, huku wengine vifo vyao vikihusishwa na kadhia hii ni ndefu sana.
Hili pia haliwaachi wale ambao wanatajwa kuyasafirisha kutoka eneo moja hadi jingne.
Majina ya wasanii kama Albert Mangweha ‘Ngwair’ na Langa Kileo waliotutoka hivi karibuni na wale waliokamatwa wakibeba dawa hizo kama Agnes Gerald ‘Masogange’, Binti Kiziwi na wengine ni ushahidi tosha wa hili.
Itoshe kusema kwamba, katika kasi ya biashara hii ya dawa za kulevya inayoendelea sasa, wasanii wamejikuta wako katikati ya muhimili wa kuathirika na kwa kweli, baadhi wako katika wakati mgumu kwa sasa.
Hata hivyo, maswali yanayobaki kuwa magumu katika vichwa vya wengi ni kwa nini kwa sasa majina ya wasanii na vijana maarufu (celebrities), ndiyo yamekuwa yakigonga vichwa vya habari katika biashara hii haramu?
Je, ni kwa kuwa wanaweza kutumia umaarufu wa majina yao kuaminika na kupita katika vizingiti na vizuizi mbalimbali? Au ni kwa kuwa wana uhitaji mkubwa sana wa fedha kuliko watu wengine?
Lakini, maswali mengine magumu ya kujiuliza katika hili ni je, wasanii wetu hawawezi kabisa kuishi kwa kutegemea kazi zao za sanaa bila kuingia kwenye mitego ya dawa hizi haramu? Je, ni kwa kuwa wanataka kuishi maisha ya mafanikio kwa njia za mkato?
Maswali haya yanakosa majibu ya moja kwa moja, lakini kwa hakika yanahitaji kupatiwa majibu ya kina ili kuweza kutibu tatizo hili, ambalo kwa sasa linaonekana kuwa sugu na kutishia mustakabali wa vijana wengi nchini.
Hata hivyo ukweli mchungu ambao mtu yeyote akiunganisha nukta kadhaa na kufanya utafiti mdogo anaweza kupata majibu ni kwamba, wasanii wengi na hata vijana wameingiwa na tamaa ya kutaka mafanikio ya haraka pasipo kusota wala kufanya kazi kwa bidii.
Hata wale wanaofanya kazi, wanataka mafanikio ya haraka sana na yasiyolingana na mikakati (input), wanayoweka hali ambayo inawafanya waingie kwenye mikakati ya ‘njia za panya’ ambayo mwisho wa siku, wengine wanajikuta kwenye mzinga wa dawa hizi za kulevya.
Kunaweza kuwa na sababu nyingine nyingi, kama umaskini wa kipato na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, lakini kwa wasanii ambao tayari wana kazi zinazoweza kuwaingizia kipato, hili la kuishi maisha ya kuigiza na yasiyo na uhalisia wa vipao vyao linaweza kuwa sababu kuu.
Nilishawahi kueleza katika moja ya makala zangu kwamba, kati ya wajibu mkuu walionao wasanii kwa sasa ni kuhakikisha kila fedha wanayoipata kupitia kazi zao inazaa fedha nyingine.
Nilieleza kwamba, inawezekana kabisa kutokana na mazingira yaliyopo sasa, kazi za sanaa zikawa zinaingiza kipato kisicholingana na kazi zao.
Hata hivyo, hicho kidogo kinachopatikana kama kikiwekezwa katika miradi mingine, kinatosha kabisa kubadili hali iliyopo na kuwa bora zaidi.
Nilitoa mifano ya baadhi ya wasanii wakubwa wa Marekani na baadhi wa hapa nchini, ambao wamekuwa wakijiingiza katika fani nyingine kama za uigizaji filamu, uuzaji wa mavazi yao, kufungua maduka na kadhalika katika kutanua mianya ya mapato.
Nilihitimisha kwa kutoa wito kwa wasanii kwamba kwa sasa wengi wao fedha wanazozipata zimeongezeka tofauti na ilivyokuwa zamani. Malipo ya maonesho na kazi zao yameongezeka. Urasimishaji wa sekta ya sanaa umeanza rasmi hivyo hawana budi kuwa chachu ya uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, ni vema nikatanua mjadala sasa kwa kuangalia tatizo jingine sugu linalozunguka vipato vya wasanii, hivyo kuwafanya kuingia kwenye vishawishi vya kufanya shughuli haramu za kuwaingizia vipato, hasa zile za kusafirisha dawa za kulevya, nalo si jingine bali lile la kuishi maisha yasiyorandana na vipato vyao halisi.
Ni wazi, wasanii wote wa Tanzania hawatoki mbinguni, bali wanapatikana miongoni mwa familia za kati au duni kabisa, ambazo nyingi zinawategemea katika kupata mkate wa kila siku na kuendesha maisha.
Kwa maana hiyo, hata maisha ya kila siku wanayoishi, lazima yafanane na vipato vyao na zaidi familia zao zilivyo. Kinyume chake ni lazima kusaka vyanzo vingine vya mapato ambavyo vinaweza kuwa halali au vinginevyo.
Hapa, ndipo huwa kunaleta shaka na utata, hasa wengi wetu tunapotazama kazi za wasanii na maisha yao ya kila siku wanayoishi. Tunafikia hatua ya kuhoji ni kwa vipi hasa wanaweza kuweka mizania halisi ya mapato yao na matumzi yao?
Si vema kuhoji mapato na matumizi ya mtu binasfsi, lakini inapofikia hatua lawama za kundi la wasanii za kupata mapato kidogo zikiongezeka huku wakionekana kila uchwao kwenye starehe za gharama sambamba na kuwepo kwa taarifa za wao kuingia kwenye shughuli haramu kama za dawa za kulevya, lazima tuanze kuhoji ili kupata majibu sahihi ya nini kinaendelea.
Tunalazimika kuhoji, maana kuna tatizo kubwa hapa linalohitaji kuwekwa sawa na lisipowekwa sawa ni maafa zaidi mbele.
Tatizo lenyewe ni la wasanii kuwa na matumizi makubwa yasiyooana na vipato vyao.
Ni tatizo hili la wasanii kuishi maisha yasiyorandana na uhalisia wao, ndilo limewalazimisha baadhi yao kutumia kila mbinu, kuhakikisha wanaweza kuishi ‘kimaigizo-igizo’. Mbinu hizi ndizo zimewafikisha kumezwa na lindi la dawa za kulevya.
Kama nilivyoeleza awali, wasanii wanaingia kwenye lindi la dawa za kulevya katika njia mbili. Kwanza, ni matumizi yake na pili ni usafirishaji wake kutoka kona moja hadi nyingine ili kupata fedha za haraka, kutoka kwa wafanyabiashara wa ‘dili’ hizi haramu.
Ukweli ni kuwa, katika hali ya kawaida, binadamu yeyote anahitaji kupata mahitaji yote ya muhimu katika maisha. Wanasayansi wanayataja mahitaji hayo kuwa yanaangukia kwenye mavazi, nyumba, chakula, mapenzi na kadhalika.
Hata hivyo, upatikanaji wa mahitaji haya na yale mengine ambayo yamepewa jina la anasa (ziada), hutegemea zaidi uwezo binafsi wa binadamu husika, vinginevyo kama kipato ni kidogo, hakuna jinsi, unaweza kuyapata labda kwa kutumia njia za panya na haramu.
Kwa vijana na wasanii wengi suala la kutaka maisha ya gharama kubwa kuanzia vyombo vya usafiri, mavazi, mitoko ya usiku, vifaa wanavyotumia na kadhalika ni jambo la kawaida sana.
Haishangazi kwa vijana na wasanii wengi kukesha maeneo mbalimbali ya klabu za usiku kwa matumizi makubwa ya fedha huku wengine wakiishi katika ufahari ambao kwa mazingira ya kawaida ya Tanzania si rahisi kuyamudu na kuyaishi kwa muda mrefu.
Suala hapa si kuvipata vitu hivyo vya gharama, suala ni je, uwezo wa kuvipata vitu hivyo unatoka wapi? Utadumu kwa muda gani? Na kwa vipi mtu ataweza kuishi maisha yasiyorandana na jamii inayomzunguka?
Maswali haya ndiyo yanapaswa kuwa dira kwa wasanii na vijana wa kisasa, ambao ndoto ya kutaka kuishi maisha ya juu na yasiyofanana na vipato vyao halisi, ndiyo yanayosababisha kuangukia kwenye shughuli haramu na za kutisha.
Kwa ujumla, kuwa maarufu ni jambo moja lakini kuweza kuumiliki na kuuishi umaarufu ni jambo jingine tofauti. Hapa ndipo tatizo lipo kwa vijana na wasanii wetu wengi.
Maana, wanaamini umaarufu ni kuwa tofauti na wengine na kuishi maisha ya gharama kuzidi wengine. Haiwezekani, maana tuko Tanzania hii hii na kipato chetu ni hiki hiki.
Wasanii na vijana wakifika mahali wakatambua kwamba hakuna jinsi wanaweza kuishi maisha yasiyooana na vipato vyao na zaidi jamii inayowazunguka, wataweza kuepuka mitego ya kuingizwa kwenye wimbi la dawa za kulevya.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment