Monday, 22 July 2013

Wachimbaji wamuua mfanyakazi wa Tanzanite One

MFANYAKAZI wa kampuni ya uwekezaji ya Tanzanite One, inayochimba madini eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro, Willy Mushi, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaoaminika kuwa ni wachimbaji wadogo baada ya kukutana mgodini chini ya ardhi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo alilosema lilitokea saa 6:00 usiku wa kuamkia jana na tayari ametuma timu ya upelelezi inayoongozwa na afisa upelelezi wa mkoa huo, kuchunguza zaidi tukio hilo.
Marehemu alipigwa risasi mbili kifuani upande wa kushoto alipoongozana na mfanyakazi mwenzake Kennedy Masimbaji kukagua eneo la mgodi unaoingiliana na migodi ya wachimbaji wadogo.
“Tulipofika kwenye mitobozano ambako kumepangwa mifuko ya viroba vya mchanga kutenganisha mgodi wetu na ile ya wachimbaji wadogo, ghafla tukashambuliwa kwa risasi ambazo zote zilimuingia marehemu kifuani na kufariki papo hapo,”
alisema Masimbaji
Mfanyakazi mwingine wa Tanzanite One, Leonard Paul alisema tukio hilo ni muendelezo wa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wachimbaji wadogo dhidi ya wafanyakazi wa mwekezaji pindi wanapokutana chini ya ardhi ambapo siku kadhaa zilizopita uongozi ulilazimika kusimamisha kazi kutoa fursa ya polisi kuchunguzi migogoro ya mitobozano.
“Serikali lazima sasa ichukue hatua kuzuia matumizi ya silaha za moto chini ya migodi,” alisema Paul.
Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Tumsifu Mushi, marehemu ameacha mjane na watoto wanne na taratibu za mazishi zinaendelea.


No comments:

Post a Comment