Tuesday, 23 July 2013

Waislamu wampongeza Lowassa kwa kuchangisha Sh. milioni 520

Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation (TIPF) imempongeza Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, (pichani) kwa kufanikisha kupatikana Sh. milioni 520, zikiwamo Sh. milioni 20 alizochangia mwenyewe kupitia harambee aliyoiendesha kwa ajili ya kuichangia Redio ya Kiislamu ya Iqra FM, iliyoko mkoani Mwanza.

Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Sheikh Saidi Godigodi, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa wanampongeza Lowassa kwa kuwa jambo alilolifanya ni zito kwa maendeleo ya Uislamu.

“Kwani Redio hiyo itasaidia sana katika kutoa elimu ya dini kwa watu mbalimbali watakaofikiwa na matangazo yake. Na hilo ndilo linalotusukuma kumpongeza na kumshukuru,” alisema Sheikh Godigodi.

Alimuomba Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), kuendelea na moyo aliouonyesha kwa Waislamu ili azidi kusaidia katika maeneo mengine kwa kuwa kutoa ni moyo.


Alisema viongozi wa aina ya Lowassa wasiokuwa na ubaguzi wa dini katika kuchangia maendeleo ni mfano wa kuigwa katika jamii. Kwa mujibu wa Sheikh Godigodi, kitendo hicho cha Lowassa kinadhihirisha wazi kwamba, tuzo waliyopewa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Musa Salum, na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited, Dk. Reginald Mengi, ilikuwa sahihi.

“Walistahili kufanyiwa jambo lile kwa kuwa ni watu wanaochangia sana maendeleo ya dini yetu bila ubaguzi,” alisema Sheikh Godigodi.

Alimpongeza pia Rais Dk. Jakaya Kikwete kwa juhudi zake za kuitangaza Tanzania kimataifa na kuiletea maendeleo makubwa kutokana na ziara zake alizozifanya nje ya nchi licha ya baadhi ya watu kuzibeza.

“Lakini ukweli ni kwamba, Watanzania sasa tunaona matunda yake, kama ziara za viongozi wakubwa duniani zilizofanywa nchini kwetu hivi karibuni na mikataba iliyosainiwa, tukianza na Rais wa China na hatimaye Rais wa Marekani,” alisema Sheikh Godigodi.

Aliwaomba Watanzania kudumisha amani nchini kwa kuwa pasipo amani hakuna maendeleo na kuwaomba pia kudumisha umoja na mshikamano walionao na kutokubali tofauti zao za kidini na kisiasa kuwafarakanisha.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment