Friday, 16 August 2013

Mkwara wa Mwakyembe Airport wajibu,mtu akamatwa na pipi 86 na misokoto 34 ya bangi

 
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akiwaonyesha waandishi wa habari picha ya mtuhumiwa wa dawa za kulevya, Leonard Jeremiah Monyo, jijini Dar es Salaam jana.
Mkwara wa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuhusu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kufanya uchochoro wa kupitishia dawa za kulevya, umeanza kuzaa matunda baada ya mtu mmoja kukamatwa akiwa na pipi 86 na misokoto 34 ya bangi.

Kukamatwa kwa dawa hizo kumekuja saa kadhaa baada ya Dk. Mwakyembe, kufanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo na kubaini kuwa JNIA kufanywa uchochoro wa kupitishia dawa za kulevya tatizo siyo ukosefu wa vifaa bali ni wafanyakazi wenyewe waliopewa dhamana ya kuusimamia.

Waziri Mwakyembe alifanya ziara hiyo juzi alfajiri na mtuhumiwa wa kusafirisha dawa alikamatwa siku hiyo hiyo saa 2:15 usiku.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alimtaja aliyekamatwa kuwa ni Leonard Jeremiah Monyo ambaye alikamatwa juzi katika uwanja huo akisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroen kwenda Italia kupitia Zurich, Uswisi.

Alisema mtu huyo ambaye ni raia wa Tanzania, alikamatwa katika uwanja huo baada ya kufanyiwa ukaguzi na wanawake wawili ambao ni wafanyakazi wa JNIA kubaini kuwa alikuwa amezificha dawa hizo katika begi lake.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Deusdedit Kato, alisema mtuhumiwa huyo alipokuwa anataka kupita getini, mashine maalum za kukagulia zilibainisha kwamba alikuwa na kitu, na hivyo askari waliokuwapo hapo walimtilia shaka na kumweka pembeni kisha kumkagua na kumkuta na dawa hizo. 

Kato alisema kuwa mpaka sasa bado hawajajua thamani ya dawa hizo ambazo watazipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kupata uthibitisho zaidi iwapo ni dawa za kulevya au la.

Kwa mujibu wa Kato, mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na Polisi na kwamba  muda wowote kuanzia jana walitarajia kumfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu  mashtaka baada ya kupata majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, NIPASHE lilipozungumza  na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Victor  Manyele, kwa njia ya simu jana kujua iwapo amezipokea na kuzipima, alisema kwa utaratibu yeye hawezi kutoa majibu kwa vyombo vya habari isipokuwa anakabidhi kwa aliyempelekea.

Dk. Mwakyembe alisema kuanzia sasa wizara yake itaanzisha utaratibu wa kutangaza na picha zao kuchapishwa katika vyombo vya habari watu au mtu atakayekamatwa na dawa za kulevya katika viwanja vya ndege vya nchini.

Aliongeza kuwa pia mtu au watu watakaokamatwa wakisafirisha dawa za kulevya kupitia viwanja vya ndege vilivyopo nchini kwenda nje au kuingia nchini, watapigwa marufuku kusafiri katika viwanja vya ndege vilivyopo Tanzania.

Alisema wafanyakazi wa uwanja huo waliofanikisha kukamatwa kwa mtu huyo aliagiza uongozi wa TAA kuwapandisha vyeo na kuwaongezea mshahara.

Dk. Mwakyembe alipoulizwa hatua ya kuwataja majina wafanyakazi wa TAA waliofanikisha kukamatwa kwa mtu huyo kama hakuhatarishi usalama wao, alisema hakuna haja ya mtu kuogopa na kama anaogopa basi aache kazi.

“Tuache utaratibu wa kuogopa, hakuna mtu ambaye ana mkataba na Mungu wa kuishi milele,” alisema na kuongeza kuwa sakata la dawa za kulevya kilo 150 zilizokamatwa Afrika Kusini zikitokea Tanzania atalitolea maamuzi hivi karibuni.

Alisema haiwezakani kuwa na Taifa la kuogopana kwani hali ikiwa hivyo itafikia wakati hata kuku atakuwa anaogopwa kwa hofu ya kwamba atadonoa watu.

Dk. Mwakyembe juzi alipofanya ziara katika uwanja huo na kupewa taarifa kwamba yupo ofisa mmoja aliyechukuliwa hatua kutokana na sakata la dawa za kulevya alisema hiyo ni sawa na utani kwa sababu kwa mujibu wa picha zilizorekodiwa katika mitambo (CCTV) iliyopo uwanjani hapo siku dawa hizo kilo 150 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 zilipopitishwa Julai 5, mwaka huu kwenda Afrika Kusini, ni wengi wanaostahili kuchukuliwa hatua.

Alisema hatua atakazochukua itakuwa ni historia na kama wapo watu waliozoea kupitisha dawa za kulevya katika viwanja hivyo labda watafute njia nyingine ya kusafirisha kama ya punda.

Alisema haiwezekani dawa za kulevya kupitishwa kirahisi katika uwanja huo wakati kuna vyombo mbalimbali vya serikali kama Usalama wa Taifa, Polisi, TAA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na nyingine na wanalipwa mshahara na serikali.

NIPASHE ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti taarifa za kukamatwa kwa wasichana wawili raia wa Tanzania waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oriver Tambo uliopo eneo la Kempton Park, Afrika Kusini wakiwa na dawa hizo aina ya Crystal Methamphetamine.

Waliokamatwa ni Agnes Jerald (25), Melisa Edward (24), ambao wameshtakiwa Afrika Kusini.
Wanawake hao walikamatwa wakiwa na dawa hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’ na baadaye walikabidhiwa polisi na kufunguliwa mashtaka.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 wamekamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.

Wiki moja baada ya tukio la wasichana hao, Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong.

Matukio hayo yanatokea wakati wakuu wa uwanja wa ndege wa JNIA zinakopitishwa wakiwa hawana cha kusema juu ya uharamia huo unaotokea kwenye kitovu cha mawasiliano cha nchi

No comments:

Post a Comment