WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harisson Mwakyembe jana alishindwa kuwataja vigogo wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya nchini na badala yake akawataja watu waliofanikisha kupita kwa bidhaa hiyo haramu iliyokamatwa hivi karibuni nchini Afrika Kusini.
Waziri huyo pia alisimulia bidhaa hiyo ilivyopitishwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa waJulius Nyerere (JNIA), uliopo jijini Dar es Salaam na kukamatwa Afrika Kusini ikidaiwa kusafirishwa na wasanii wa hapa nchini.
Wengi wa watu waliotajwa kuwasaidia wauza ‘unga’ na wasafirishaji ambao hadi sasa hawajulikani, ni wafanyakazi wa uwanja huo katika idara mbalimbali.
Wafanyakazi wa uwanja huo waliotajwa kusaidia usafirishaji wa dawa walizokamatwa nazo Watanzania wawili Agnes Gerald “Masogange” na Melisa Edward nchini Afrika Kusini ni Koplo Ernest wa Jeshi la Polisi Tanzania, Zahoro Mohamed Seleman ambaye ni mbeba mizigo uwanjani hapo, Yusuph Daniel Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwa ambao ni maofisa wa usalama wa uwanja huo.
Hatua ya Dk. Mwakyembe kutangaza kuwataja hadharani vigogo wa dawa za kulevya ilisubiriwa kwa kiasi kikubwa na wananchi ambapo jana waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliingia katika Wizara ya Uchukuzi kuanzia saa 7:30 mchana hadi saa 8:40 wakati waziri huyo alipoingia na kutoa taarifa yake kwa umma.
Dk. Mwakyembe alisema baada ya serikali kupata taarifa ya kukamatwa kwa Watanzania Julai 5 mwaka huu katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini na kubaini wahusika walianzia safari jijini Dar es Salaam, waliamua kupitia mfumo mzima wa kamera za uwanja wa ndege wa JNIA (CCTV) na kubaini matukio yaliyohusika moja kwa moja na usafirishaji wa dawa hizo.
Alisema waliangalia mfumo wa kamera kuanzia saa 9:25 hadi 10:30 alfajiri ya Julai 5 na kubaini namna mkakati huo ulivyofanikishwa.
“Saa 9:28 alfajiri kamera zinamuonyesha kijana mbeba mizigo kwa jina la Zahoro akiwa anazunguka zunguka eneo la kuingia abiria mithili ya mtu mwenye miadi fulani, na kisha eneo jingine alionekana Issa akitoka nje ya jengo na kuingia tena huku akiongea na simu na hili haliruhusiwi,” alisema Mwakyembe.
Aliongeza kuwa wakati kamera zikimuonyesha Issa, pia alionekana Koplo Ernest akiranda randa eneo la uhakiki wa hati za kusafiria akiwa na dalili za kusubiri kitu na ilipofika saa 10:15 alfajiri waliingia watu watatu.
Aliwataja watu hao ni Agnes Masogange, Melisa Edward na Nasoro Mangunga wakiwa na mabegi tisa ambapo katika eneo hilo anaonekana tena Koplo Ernest akiwasaidia abiria kupanga mizigo na wakati huo huo mbeba mizigo Zahoro akisaidia kuweka vizuri mizigo ya kina Masogange na wenzake kabla ya kuizungushia karatasi za nailoni.
“Huu mtandao ni mkubwa na unahitaji uadilifu kwani baada ya shughuli hiyo tulimuona Yusuph akimuondoa mfanyakazi mwenzake yule Manyonyi na kukalia kiti cha mkaguzi wa mizigo na hili lilifanyika kwa dakika sita. Baada ya kufanikisha kazi hiyo akamwachia mwenzake jukumu alilokuwa nalo,” aliongeza Dk. Mwakyembe.
Alisema jambo jingine walilobaini ni kucheleweshwa kwa mbwa wa ukaguzi wakati mizigo hiyo ikipitishwa na kwamba ukaguzi wa kutumia mbwa ulifanyika wakati mabegi yenye dawa hizo yalipoingizwa katika sanduku la chuma na mbwa kunusa sanduku badala ya mabegi.
Aliongeza kuwa mkakati mwingine uliofanikisha hatua hiyo ni kwa Mangunga kuruhusiwa kusafiri siku hiyo hiyo licha ya kutokuwa na tiketi, na kwamba alilipa dola 60 kufanikisha safari yake ya dharura.
Uamuzi wa wizara
Kutokana na hali hiyo Dk. Mwakyembe alisema serikali imeiagiza Mamlaka ya Uwanja wa Ndege (TAA) kuwapiga picha watu wote watakaokamatwa na dawa za kulevya na kusambazwa katika vyombo vya habari, kampuni iliyomuajiri Nasoro imfukuze kazi mtumishi wake huyo na asikanyage uwanja wa ndege wa JNIA.
Waziri huyo pia alilitaka Jeshi la Polisi limkamate Zahoro na kumuunganisha na wenzake kujibu mashitaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya sura ya 95 ya mwaka 1996.
Dk. Mwakyembe aliitaka TAA kuwafukuza kazi wafanyakazi wake wanne ambao ni maofisa wa ulinzi uwanjani hapo na kisha wakamatwe na kufunguliwa mashitaka, huku Jeshi la Polisi likitakiwa kumchukulia hatua za kinidhamu Koplo Ernest.
Mbali na hatua hizo, pia Dk. Mwakyembe alisema serikali inaiagiza Idara ya Usalama wa Taifa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu Julai 5 mwaka huu, kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wa kubaini dawa hizo katika muda muafaka wa kukagua mizigo.
Wakati Dk. Mwakyembe akielezea hali hiyo kwa Tanzania, taarifa zilizopatikana na gazeti hili zinabainisha kuwa nchini Afrika Kusini mtandao huo ulijipanga kufanikisha upitishaji wa dawa hizo aina ya Cyrsatl Methamphetamine au “TIK” pasipo kubughudhiwa.
Taarifa zinaeleza baada ya Masogange na wenzake kufanikiwa kupita katika maeneo ya ukaguzi ya uwanja wa Oliver Tambo, Mangunga alifanikiwa kuondoka uwanjani hapo na mabegi matatu yenye jumla ya kilo 60 bila kujulikana.
“Masogange kilichomponza ni pale alivyokuwa anajiremba baada ya kuruhusiwa kupita katika vizuizi vyote. Kiuhakika hakukamatwa katika mashine bali ilikuwa ni ukaguzi usio rasmi uliofanywa na polisi. Nadhani huyu askari aliyewashika hakujua mpango huo,” kilisema chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment