Saturday 17 August 2013

Wanaotafsiri filamu za nje marufuku

BODI ya Filamu Tanzania, imetoa miezi sita kwa watu wanaotafsiri filamu za nje hapa nchini kuacha mara moja kwani ni kinyume na sheria.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa bodi hiyo, Joyce Fissoo, alisema wanatoa miezi sita kwa watu wanaofanya kazi ya kutafsiri filamu za nje kuacha mara moja na ni kinyume cha makosa ya hatimiliki.
Fissoo alisema atakayekaidi amri hiyo atachukuliwa hatua kali na ikiwemo kufunguliwa mashitaka.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwepo kwa Watanzania wanaofanya kazi ya kutafsiri filamu hizo maeneo mbalimbali nchini.
Watu hao, wamekuwa wakizichukua filamu hizo kwenye mitandao na kuziingiza maneno ya Kiswahili na kuziuza huku zikiwa hazina nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Tanzania Daima ilifanikiwa kufika maeneo ya Mtoni Mtongani, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambako ndiko kuna mitambo inayodurufu filamu hizo na kukuta biashara hiyo ikiendelea, huku watu wakizigombania kununua.
Walipoulizwa wafanyabiashara waliokuwepo maeneo hayo, ambao huzichukua filamu hizo na kuzipeleka sokoni, kama hawaoni kuwa ni makosa kufanya biashara hiyo, walijibu wanatambua, lakini wakahoji mbona serikali wanawaacha, hivyo biashara hiyo iko poa.
Uchunguzi ulibaini majina ya watu wanaotafsiri filamu hizo, kuwa ni Juma Shine maarufu kama Dj Maki, Juma Kani na mwingine anayejulikana kwa jina moja la Rufufu, ambao walipotafutwa, hawakuweza kupatikana mara moja.
Tanzania Daima ilibisha hodi kwenye ofisi za TRA kupata ufafanuzi kutokana na biashara hiyo, lakini wahusika hawakuwa radhi kujibu kwa wakati huo na kutaka kuachiwa taarifa kwa maandishi na kuahidi kujibu baadaye
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment