Dar es Salaam. Polisi Makao Makuu Kitengo cha Makosa ya Jinai Rasimali Watu, juzi ilimhoji Amir Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha kwa kile walichodai kuwa mtu huyo ni rafiki mkubwa wa Sheikh Kondo Bungo anayetafutwa polisi.
Taarifa kutoka kwenye vyanzo vya polisi Makao Makuu zilieleza kuwa Bungo anatafutwa na polisi kwa kile walichodai alitoa maneno ya uchochezi katika Mkutano wa Waislamu uliofanyika Viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Advocate Nyombi, kutoka Kitengo cha Upelelezi Makao Makuu alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, simu yake ilikuwa haipatikani.
Chanzo chetu kilidokezwa kuwa baada ya mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, Polisi walipanga kumkamata Bungo kwa wakati maalumu na siyo eneo lile ili kuepusha vurugu ambazo zingeweza kutokea endapo angetiwa nguvuni.
“Kundecha aliitwa jana (juzi) na kuhojiwa kwa saa kadhaa na kumtaka amlete Bungo ambaye ni mtu wake wa karibu, “ alisema mtoa habari huyo kuongeza kuwa: “Asipofanya hivyo kwa muda aliopangiwa basi atakamatwa yeye hadi hapo atakapo patikana Bungo.”
Katika hatua nyingine, Polisi Kanda Maalumu inamshikilia Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa m Kitengo cha Utafiti wa Mimea kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi fundi ujenzi, Fadhili Mkachino.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 10 alasiri maeneo ya SalaSala Benako wilayani Kinondoni.
Alisema Mkachino akiwa na mafundi wenzake wakijenga nyumba moja ya Khadija, ndipo profesa huyo alitokea na kuwataka kusisitisha mpango huo mara moja kwa kile alichodai ni eneo lake.
“Kabla ya mafundi hao hawajafanya chochote ghafla Profesa huyo alitoa bastola na kumpiga risasi mbili tumboni Mkachino ambaye alikuwa kiongozi wa mafundi hao na kumsababishia maumivu makali,” alisema Kamishna Kova.
Kova alisema kitendo cha kumpiga risasi mtu ni kosa la jinai na kwamba ni jambo lisilokubalika katika jamii. Alitoa wito kwa wenye silaha kuwa wavumilivu wakati wote.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment