Tuesday 20 August 2013

Ponda kama sinema

Mkurungenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), amemfutia mashtaka ya uchochezi Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, yaliyokuwa yanamkabili.

Jana saa 2:00 asubuhi viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Hellen Riwa, upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kusudio la kutokuendea na mashitaka kutoka kwa DPP.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, aliwasilisha hati hiyo akidai kuwa DPP ameona hana nia ya kuendelea kumshtaki Sheikh Ponda na ameomba mahakama kumfutia mashtaka hayo.

Wakati mahakama ikimfutia kiongozi huyo mashtaka, viunga vya mahakama hiyo vilizungukwa na askari polisi waliokuwa na sare za jeshi hilo na wengine kiraia ili kuimarisha ulinzi.

Hata hivyo, baada ya Sheikh Ponda kufutiwa mashtaka aliondoka mahakamani hapo chini ya ulinzi na alipakiwa kwenye helkopta ya Jeshi la Polisi kwenda mkoani Morogoro ambako alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka mapya.

Mjini Morogoro, shughuli mbalimbali zilisimama kwa muda kufuatia Sheikh Ponda kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.


Sheikh Ponda alipandishwa mahakamani na kusomewa mashitaka matatu ambayo ni kutotii amri halali ya mahakama, kutoa maneno ya uchochezi yenye nia ya kuharibu imani za dini za watu wengine pamoja na kufanya uchochezi dhidi ya wananchi na serikali.

Kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, jeshi la polisi liliimarisha ulinzi maeneo yote ya jirani na mahakamani hapo kwa askari wa vikosi vyote ikiwamo mbwa pamoja na gari la maji ya kuwasha. 

Shekh Ponda aliwasili mahakamani hapo saa 5:26 asubuhi kwa helikopta ya Jeshi la Polisi akiwa amesindikizwa na maofisa wa polisi kutoka Dar es Salaam waliovaa kiraia.

Kabla ya kuwasili kwa helkopata hiyo, polisi iliimarisha ulinzi katika viwanja vya Gymkhana ambako ndipo helikopta hiyo ilitua na kisha kupelekwa mahakamani kwa kutumia gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser nyeusi iliyokuwa na namba T 007 BQC.

Aidha, ulinzi mkali uliimarishwa kwenye mahakama hiyo ambako kulikuwa na gari tatu aina ya Land Rover Defender zikikuwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambao walikuwa na silaha za moto, mabomu ya machozi, mbwa na pia kulikuwa na gari lenye maji ya kuwasha huku barabara inayokatisha mahakamani hapo ikifungwa.

Hali hiyo ilisababisha ofisi zilizo jirani na mahakama hiyo ikiwamo ofisi ya mkuu wa wilaya, hazina ndogo, ofisi ya madini, ofisi ya ukaguzi pamoja na posta kusimamisha kazi kwa muda.

Akisomewa mashitaka hayo akiwa amekaa kutokana na kudai kuwa na maumivu ya jeraha kwenye bega, Wakili Mkuu wa Serikali Kanda ya Morogoro, Bernard Kongola, alidai kuwa Sheikh Ponda alitenda makosa hayo matatu Agosti 10, mwaka huu majira ya jioni katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro.

Katika shitaka la kwanza, Ponda anadaiwa kutotii amri halali ya mahakama ya kutokutenda kosa lolote wakati anatumikia kifungo cha nje na shitaka la pili anadaiwa kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini kwa kutoa maneno “Serikali iliamua kupeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa Mtwara ni Waislamu.”

Shitaka la tatu linalomkabili Sheikh Ponda ni kushawishi na kutenda kosa na anadaiwa kuwa alitoa maneno ya ushawishi ambayo ni “Ndugu zangu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani zinaundwa na Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) ambao ni vibaraka wa CCM na serikali; na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha fungeni milango na madirisha ya misikiti na muwapige sana.”

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Sheikh Ponda anayetetewa na mawakili Bartholomew Tarimo na Ignas Punge, alikana mashtaka yote na hivyo upande wa mashtaka kupinga dhamana kwa madai kuwa Sheikh Ponda anatumikia kifungo cha nje na kwamba hakutakiwa kufanya kosa, hata hivyo anakabiliwa na makosa mengine.

Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Punge ulishindwa kuwasilisha maombi ya dhamana kwa madai kuwa kuomba dhamana kuna hatua nyingi, hivyo kwa sasa wanaandaa utaratibu wa kumpatia dhamana mteja wao na ombi hilo litawasilishwa mahakamani hapo.

Upande wa mashitaka umedai kuwa upelelezi umekamilika na kesi hiyo itatajwa Agosti 28, kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Mshtakiwa alipandishwa tena helikopta ya polisi na kurudishwa rumande katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam. 

Hata hivyo, kabla ya kuondolewa mahakamani hapo, baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wake walisimama mbali na gari lililombeba Sheikh Ponda na kuanza kusema ‘takbir, takbir’.

Katika mashitaka yaliyofutwa jana, akiwa kitandani katika wodi Taasisi ya Mifupa (MoI), Jumatano iliyopita, Ponda alisomewa  mashtaka ikidaiwa kuwa alifanya makosa sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Juni 6 na Agosti 11, mwaka huu mshtakiwa alihamasisha vurugu zilizopelekea uvunjifu wa amani.

Kosa la pili ambalo lilikuwa katika hati ya mashtaka Sheikh Ponda alidaiwa kufanya makosa sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar; na kesi yake ilipangwa kutajwa tena Agosti 28, mwaka huu.

Mapema Agosti 10, mwaka huu Sheikh Ponda alijeruhiwa mkoani Morogoro baada ya kuhutubia mhadhara wa Sikukuu ya Idd El Fitri ulioandaliwa na wanazuoni wa dini ya Kiislamu mkoani humo.

Inadaiwa kuwa Sheikh Ponda alijeruhiwa bega la kulia kwa risasi iliyopigwa na polisi katika harakati za kumkamata baada ya mhadhara huo.

Inadaiwa kuwa wafuasi wake walimpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, lakini baadaye walimhamishia katika hospitali ambayo haikufahamika.

Kesho yake alipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya kuhamishiwa Moi.

Imeandikwa na Hellen Mwango na Jacqueline Yeuda Dar na Ashton Balaigwa, Morogoro
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment