Friday 23 August 2013

‘RAY C’: Niliingia kwenye mihadarati bila kujijua

WINGU la utumiaji wa dawa za kulevya (mihadarati), kwa wasanii, limezidi kutanda hapa nchini huku wengine wakipoteza maisha kutokana na utumiaji wa dawa hizo na wengine kuamua kuachana nayo kabisa na kutoa ushuhuda.
Licha ya wasanii kupoteza maisha kutokana na matumizi hayo, wengine wamejikuta wakiishia mikononi mwa vyombo vya dola wakiwa katika harakati za kuyasafirisha nje ya nchi, kama ilivyotokea hivi karibuni kwa msanii anayejulikana kama Agnes Masogange.
Kutokana na matumizi hayo, ambayo yamewagusa wasanii wengi, akiwamo mwanadada aliyekuwa akitesa katika anga la muziki wa kizazi kipya, Rehema Chalamila ‘Ray C’, ambaye alipotea katika ‘game’ takriban miaka mitatu kutokana na athari za matumizi hayo, ameamua kufunguka na kumuomba Mungu aweze kumsaidia.
Ray C, mkali wa muziki wa kizazi kipya aliyekuwa katika upinzani mkali na mwenzake, JudithWambura ‘Lady Jaydee’, ameamua kusema kweli juu ya utumiaji wake wa dawa hizo ili aweze kupewa msaada wa kimatibabu.
Kuanza kutumia

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Clouds TV, Ray C anasema anajuta kutumia dawa hizo ambazo zimemfanya ashindwe kutimiza ndoto zake na kujikuta akipotea kwa muda mfupi, wakati mafanikio ndiyo yalikuwa yameanza kukolea.
Anasema, hajui aliingiaje katika dimbwi hilo, kwani kuna mpenzi wake ambaye alimfanya aanze kutumia bila yeye kujijua na alipogundua, ikawa vigumu kujitoa, kwani alikuwa akipata maumivu makali kuanzia miguuni na kumlazimu aendelee kutumia ili maumivu yaweze kukata.
“Mimi kwa kweli sijui niliingiaje katika matumizi hayo, lakini namlaumu sana X-Boyfriend wangu ambaye nilikuwa naye, maana yeye alikuwa anatumia mimi sijui na kunirubuni nikajikuta nimeanza kutumia na baadaye alikuja kuniambia, unajua unatumia nini, nikabaki nashangaa na ndipo akaniambia hizo ni dawa za kulevya, nilichanganyikiwa, ila sikuwa na namna ya kufanya,” anasema Ray C.
Aidha, Ray C anasema alipogundua mpenzi wake huyo si mtu mzuri kwake, aliamua kuchukua ‘maamuzi magumu’ ya kuachana naye, japokuwa alikuwa anampenda kwa dhati na kuwa na malengo naye.
“Yule kijana alikuwa mdogo na mimi nilimpenda sana, lakini mara baada ya kuona ananipeleka pabaya nikaamua kuachana naye,” anasema Ray C.
Madhara yake
Ray C anasema alipokuwa katika matumizi ya dawa hizo alikuwa anaona maisha ndiyo yake, kwani hata mama yake mzazi alipokuwa akimuomba fedha, alikuwa akimwambia hana huku roho ikiwa inamsuta, kwani mfukoni alikuwa na zaidi ya sh 1,000,000 lakini aliona vigumu kumpa mama yake na kwenda kununua dawa hizo.
“Ukweli ni kwamba, hizi dawa hazina faida yoyote bali ni tabu tupu kama nilizozipata mimi, maana mimi ni mfano hai, nilikuwa namnyima mama yangu fedha wakati ana shida na mimi nazipeleka kununua dawa, jamani Mungu anisamehe sana, maana hata roho ilikuwa inanisuta lakini sijali,” anabainisha.
Kutokana na kutumia dawa hizo kwa muda, hata alipoimba wimbo wa ‘Mama Ntilie’ alioshirikishwa na AT, anasema tayari alikuwa mwathirika wa dawa hizo, lakini alikuwa hajafikia hatua mbaya kama aliyokuwa nayo hivi karibuni, hadi Rais Jakaya Kikwete alipoamua kumpa sapoti ya matibabu.
Kuumwa kwake
Anasema mara baada ya kuona hali yake ya kiafya inadhohofika, aliamua kukimbilia nchini Kenya kwenda kufanyiwa matibabu na hali ilipomshinda na kuanza kuwa mbaya, aliamua kurejea nyumbani na kumweleza mama yake mzazi hali halisi.
“Hata nilipokuwa Kenya mwaka mmoja hivi, nilikuwa nafanya kazi zangu lakini huku nikiwa naumwa, nilipoona hali yangu inakuwa mbaya nikaamua kurudi nyumbani na kumweleza mama yangu na hapo tukaanza matibabu,” anasema.
Siku chache baada ya kurejea nchini, aliamua kuweka wazi kinachomsumbua na ndipo Rais Kikwete akaamua kumsaidia na kumtaka aende Hospitali ya Taifa Muhimbili akapatiwe matibabu, kwani dawa zipo na zinatolewa bure.
“Mara baada ya Rais wangu Kikwete, baba yangu kuniambia hivyo, tukafunga safari mimi, mama yangu na dada yangu, mpaka Muhimbili tukakutana na daktari ambaye alinisaidia vizuri mpaka sasa na kunipa moyo, japokuwa sitamtaja, nikapewa dawa, dakika kadhaa tu nikaona hali imebadilika japokuwa nilikuwa nasikia maumivu,” anabainisha.
Mara baada ya kufika Muhimbi, madaktari walimshauri kutosita kusema ukweli ili aweze kupewa matibabu na kupona kabisa na yeye aliweka wazi bila ya kuficha, kwani alitamani kupona siku hiyo hiyo.
Anasema akaanza kutumia dawa hizo ambazo anaendelea nazo hadi sasa na siku akiona uvivu kwenda Muhimbili, alikuwa akienda Hospitali ya Mwananyamala na kupatiwa matibabu kama kawaida bila ya kutozwa gharama yoyote.
Anawazungumziaje wengine?
Kuna usemi usemao, uking’atwa na nyoka, hata ukiguswa na nyasi unahisi ni nyoka, kwani Ray C anasema kwa sasa hata akiona na kusikia harufu ya moshi anaona ni kero, kwani anamshukuru Mungu kwa kumtoa katika dimbwi hilo huku akiwataka wasanii au watu wote wanaotumia dawa hizo waachane nazo mara moja na waende Muhimbili au Mwananyamala wakapate matibabu.
“Mimi ninajua kuna wasanii wenzangu wengi sana na watu wengine wanashinda maofisini na kuniga tai, nawaomba waachane na matumizi ya dawa hizo, kwani mimi najua vizuri madhara yake, na nina imani wale wanaotumia wamenisikia, mimi nimeweka wazi, watakwenda kupanga foleni ya ‘kufa mtu’ bila woga ili wapatiwe tiba,” anasema.
Licha ya kuwashauri watumiaji, anasema hata wauzaji wa dawa hizo ambao wanawaona wasanii ni watu wenye hela na kuwaharibu kiasi hicho, Mungu yupo na wao anawaona, kwani adhabu yao yeye ndiye atawapatia.
“Kuna watu wanarubuni wasanii kwa kuwa wanajua sisi tuna hela, kwa shoo moja mtu anajipatia milioni tano, wanaona tuna hela za bure, ila Mungu yupo na ipo siku, kwani wao wanaharibu watoto wa watu na sitaki kuwataja majina hapa, wanaendelea kupeta, kuendesha magari ya kifahari na kujenga maghorofa, wakati wenzao wanateseka, wengine wanatokwa udenda, siku ipo,” anasema huku akitokwa machozi.
Anavyozungumzia muziki kwa sasa
Ray C anasema muziki kwa sasa umekua na anatamani kurejea katika fani aliyobarikiwa na Mungu, kwani ana imani kubwa wapenzi na mashabiki wake bado wanamkubali.
Anasema siku za hivi karibuni, anatarajia kurekodi nyimbo zake si chini ya 30, ambazo amezitunga alipokuwa nyumbani akiendelea na matibabu ndani ya mwaka mmoja na wala hakuwa nje ya nchi kama watu wanavyodai.
“Mimi toka nilipoanza matibabu nipo kwa dada yangu naendelea na matibabu, nyumbani sikuwa na kazi, nilikuwa nafanya kutunga nyimbo tu, hivi sasa narudi tena jukwaani, kwani najua hakuna mwanamuziki ambaye namhofia kwa sasa,” anasema.
Mbali na kutowahofia wasanii, anasema, anamkubalia msanii anayekuja juu kwa kasi katika tasnia hiyo, Recho, kwani amemwakilisha vema kipindi chote alipokuwa amepotea katika ‘game’.
Anaongeza kuwa siku si nyingi atamaliza dozi na hapo ataanza kufanya mazoezi ya kurejesha mwili wake, kwani kwa sasa anajutia mwili wake, kwa kuwa amenenepa kupita kiasi na kuharibika ‘shape’ yake ya zamani.
Kauli yake kwa sasa
“Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa ‘second chance’, maana wenzangu Ngwair na Langa Mungu amewachukua na wao walikuwa katika dimbwi hilo, ila kwa nini mimi Mungu ameniepusha, najifikiria mara mbili, naona bado nahitajika kukitumia kipaji changu,” anasema.
Ray C anasema hakuna kitu ambacho yeye anazidiana na wenzake waliotangulia mbele ya haki, ila Mungu ndiye kila kitu.
“Mungu anajua na ameniponya na ameona kufa na kashfa hii si vizuri, na mimi nitamtumikia na kutoa kazi mpya hata nikifa watu waweze kusema, aliumwa akapona akarudi kwenye muziki halafu akafa, maana nilianza kujuta na kuona kama ni jini hivi.
Maana nilikuwa kama nina fuvu usoni na mama yangu akawa ananishangaa na kumuomba Mungu, kwani Ray C yule si wa sasa, mimi ni mpiganaji, nilianza kujitegemea nina miaka 17 na nikiwa na miaka 23 nilianza kujenga nyumba yangu mwenyewe, na ndoto zikazimika ghafla, Mungu nisaidie,” anaongeza.
Shukrani
Anatoa shukrani kwa Rais Kikwete, madaktari, ndugu, mama yake mzazi pamoja na rafiki zake wapya ambao walimthamini wakati anaumwa na si wa zamani ambao hata kumjulia hali ilikuwa shida.
Ray C alitamba na vibao mbalimbali vikiwamo, ‘Na Wewe Milele’, ‘Mahaba ya Dhati’, ‘Umenikataa’, ‘Sogea Sogea’ na vingine vingi.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment