Monday 5 August 2013

Wazazi wanaowabagua watoto ni wasaliti wakubwa!

 “Mzazi anapobagua watoto kutokana na hali zao kimapato.”

 hebu leo wasikie baadhi ya wasomaji waliochangia mada hiyo kama ifuatavyo;-

…huyo kijana awe mvumilivu kwani hakuna marefu yasiyo na ncha. Mungu atamfungulia milango ya Baraka atabarikiwa kama wenzake hao wenye kipato. Asimchukie mama yake, amheshimu tu. (Stela wa Dar).
….Hapo dogo ashtakie kwa Mungu huku akichapa kazi kwani ipo siku atatenda miujiza. Kwa kuwa si mama mzazi aachane naye asije kumuathiri kisaikolojia(Msomaji Dar).
….Jamani, kubagua watoto kwa hali yoyote ile siyo vyema hata Mungu hapendi, ndiyo maana akatupa watoto katika hali tofauti…ni kama mtihani kwa wazazi. Inabidi tuwaweka katika mtizamo sawa ili wasijisikie vibaya. Mfano, watu wa mkoa fulani. Usione kila mwaka wanaenda kwao ile ni kwenda kutathmini nani ana nini, kakwama wapi tumsaidie. Hapo mambo yanakwenda vyema na kubaguana hakutakuwapo.(mama Lulu, Kitunda).
... Huyu mzazi ni mbaguzi sawa na wale wanaobagua watoto bila sababu. Anampenda mtoto fulani hata kama ana tabia mbaya na kuwachukia wengine.
Mifano ipo ya ukweli. Tukirudi kwa huyu mzazi anayekimbilia wenye uwezo hajui kwamba kuna kwako leo na kesho kwangu? Zikijaisha kwa hawa halafu akapata huyu asiye nacho atarukia tena upande wa pili? Watoto umezaa wewe unabagua kisa fedha! Wazazi wengine hamnazo kweli.(Willy Kwanga, mji mpya Majohe Ukonga).
Mpenzi msomaji, hao ni baadhi ya wachangiaji wa kisa hicho ambapo mama anayetajwa anapendelea watoto wake ambao wamejaliwa kimapato. Lakini huyu ambaye ni mtoto wa dada yake aliyekwisha kutwaliwa mbele za haki, anamtenga kisa hana uwezo kifedha.

Mimi nilidhani atakuwa karibu na huyu asiye nacho na kumpa mwelekeo wa kujiinua ili angalao akimbizane na wenzake, lakini kinyume chake anamtenga mbali naye. Ama kwa hakika, huyu siyo mama mlezi mwenye uchungu na watoto wa wanawake wenzie. Kama alivyouliza msomaji mmoja hapo juu, kwamba mama huyo “hajui kwamba kuna kwako leo na kesho kwangu?”
Ni jana tu nilikuwa nikiongea na baba mmoja akimsikitikia kaka yake ambaye hivi sasa anafanya vituko visivyotakiwa katika maisha haya. Kaka yake huyu ni mzee mstaafu ambaye japokuwa anao watoto, lakini hapo anapoishi ameanza kuuza eneo kimya kimya tena bila hata kumshirikisha mkewe na watoto.
Kibaya zaidi, fedha anazopata hafanyi nazo kitu chochote cha maana bali anampelekea mwanamke mmoja ambaye na mumewe na watoto, lakini inavyoonekana mama huyo na mumewe walishakubaliana wamchune mzee huyu, jambo ambalo wamefanikiwa sana.
Kila akipata fedha iwe za kupewa na watoto, kodi za nyumba au kuuza eneo, yeye mbio humpelekea mwanamke huyo wanazifaidi. Wazee wenzake wa mtaani wanamtizama na kumuonea huruma lakini wafanyeje?
Ndipo mdogo wake aliposikia taarifa hizo akawa anasikitika sana kwa kuniambia; “Vituko vya kaka yangu vinanisikitisha sana…hataki kukubali kuwa ameshazeeka huku akipiga miaka 70….Ni ajabu marehemu mama yetu alikuwa anampenda kuliko watoto wote. Akimchukulia kwamba atakuwa na mafanikio makubwa sana huko aendako.
Ni sawa alipata kazi nzuri hadi akastaafu. Lakini vituko anavyofanya na uzee huu ni aibu kubwa… Sasa anatuonea wivu sisi ambao tulidharaulika zamani lakini sasa tuna heshima zetu wakati yeye anasemwa ovyo mitaani,” anamaliza kusema mzee huyu anayekaribia miaka 67.
Mpenzi msomaji, nimehusisha maelezo ya mzee huyo kuonyesha jinsi ubaguzi wa watoto ulivyokuwa tokea zamani. Hata watoto wenye akili, tabia njema nyumbani, baadhi ya wazazi waliweza kuonyesha ubaguzi wa wazi. Wengine waliwaletea zawadi wale wanaowapenda na kuwaacha wengine.
Nakumbuka mama yangu, akiwa mzaliwa wa pili akitanguliwa na kaka yake, baba yao(babu), aliwabagua na kumpelekea mjomba shule ati kwa sababu ni mwanaume na kumwachisha mama darasa la pili eti ni mwanamke na atakwenda kuolewa hivyo hana faida. Ebo! Hayo yalikuwa makosa makubwa kutomwendeleza mwanamke, makosa ambayo serikali yetu imeyasahihisha kwa kiwango kikubwa hivi sasa. Mtoto wa kike anathaminiwa kielimu sawa na mtoto wa kiume.
Hata kasumba ya upendeleo wa watoto unaofanywa kati ya baba na mama katika baadhi ya familia huonyesha wazi aina ya ubaguzi wa mtoto fulani kuliko mwingine, huku zikiwapo sababu zake mbalimbali.
Kwa mfano, yupo atakayemtenga mtoto kwa sababu anamdadisi na kutoa siri zake iwe kwa baba au kwa mama. Mwingine atabaguliwa na mmoja wa wazazi kutokana na tabia yake mfano mwizi, mdokozi, haambiliki anapokanywa na kadhalika.
Hali kama hii siyo sahihi kabisa. Kama mzazi/wazazi wanapaswa kuwa kidete na watoto wao katika kuwalea sawa na kuwapa miongozo sahihi inayokubalika katika kuwajengea mazingira salama na tabia njema.
Wazazi wanapaswa kuwasaidia watoto kujiona wamoja na wanaostahili malezi sawa na sahihi pasipo upendeleo. Ubaguzi wa watoto na hasa unapofanywa bayana na wazazi hupelekea chuki, mifadhaiko kama ambavyo anateseka kijana anayebaguliwa na mama yake mdogo.
Huyu hasikitiki sana kwamba hana kipato kikubwa kama wenzake, la hasha. Anachosikitika, kama nimemuelewa vyema ni kwamba kwanini mama yeke huyo mdogo anapokuja kutembelea watoto wake, yeye hamjulii hali, walau kujua anaendeleaje au ana tatizo gani?
Mama huyu anasahau kwamba kila mtu hazina yake iko mbinguni. Na kila mtu Mungu anao utaratibu wa kumpa kile alichomwandaliwa tokea akiwa tumboni mwa mama yake.
Ndiyo maana kijana huyu hapaswi kusikitika sana bali achape kazi kama alivyoshauriwa pia na masomaji wetu hapo juu, na naamini iko siku Mungu atamuinua kimapato, hata hao wanaomdharau waje kumwangukia. Si unajua tena malipo ni hapa hapa duniani?Wazazi wanaowabagua watoto kwa namna yoyote ile ni wasaliti wakubwa!
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment