MHARIRI wa zamani wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kuwa hakuwahi kupata taarifa ya malalamiko kutoka Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu makala iliyochapishwa Novemba 30, 2012.
Makala hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Waraka maalumu kwa askari wote’ iliandikwa na mshtakiwa wa kwanza, Samson Mwigamba, katika safu yake ya ‘Kalamu ya Mwigamba’ katika gazeti hilo.
Akitoa utetezi jana mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Waliarwande Lema, Kibanda alidai kuwa toka makala hiyo itoke hakuwahi kuitwa, kupewa onyo wala kulalamikiwa na Idara ya Habari (Maelezo).
Kibanda pia aliieleza mahakama hiyo kuwa Idara ya Habari (Maelezo) wao kama wasajili wa magazeti wangeona makala hiyo ina makosa, msajili ama angefungia gazeti, angeandika barua ya wito au kutoa onyo hatua ambayo hufanyika ndani ya siku moja au mbili.
“Nilikaa zaidi ya wiki mbili ndipo nikaitwa polisi, lakini sikuwahi kuitwa na idara hiyo ili kujieleza, ama kupewa onyo kutokana na makala hiyo,” alidai.
Pia alidai kuwa makala hiyo ilikuwa ni maoni ya mwandishi yaliyoeleza haki ya wananchi kuandamana, kuishi na haki ya polisi kuwalinda raia na mali zao.
Kwa upande wa mshitakiwa wa kwanza Mwigamba, alijitetea kwa kuieleza mahakama hiyo kuwa si kweli kwamba makala hiyo ilishawishi askari kutotii amri ya wakubwa wao bali aliandika kutoa maoni kwa askari wasivunje haki ya kikatiba kwa raia, haki ya kukusanyika na haki ya kuishi.
Kibanda, Mwigamba na Theophil Makunga wanakabiliwa na kesi ya uchochezi dhidi ya askari wa majeshi ya ulinzi kwa kuchapisha makala kwenye gazeti la Tanzania Daima yenye maneno yanayodaiwa kuwashawishi askari wasiwatii viongozi wao.
Washitakiwa hao wanatetewa na wakili Nyaronyo Kicheere, Isaya Matambo na John Mhozya, wanaowatetea Mwigamba na Kibanda na Imam Daffa kwa niaba ya Makunga.
Kesi hiyo itaendelea tena Septemba 23, mwaka huu kwa mshitakiwa wa tatu Makunga kujitetea na upande wa washitakiwa kupeleka mashahidi
No comments:
Post a Comment