Wakati serikali ikiendelea kupiga vita biashara ya dawa za kulevya nchini, meli moja iliyosajiliwa Tanzania imekamatwa nchini Italia ikiwa na shehena ya dawa hizo tani 30 zenye thamani ya Paundi milioni 50 sawa na Sh.bilioni 123 za Tanzania.
Meli hiyo ilikamatwa wiki iliyopita katika tukio lililozua kizazaa kikubwa baina ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo na watu waliokuwa ndani ya meli hiyo ambao waliamua kuilipua moto na kisha kujitosa baharini ili kujaribu kutoroka na kupoteza ushahidi.
Watu tisa waliokuwa ndani ya meli hiyo walichukua uamuzi wa kuilipua na kujitosa baharini baada ya kubaini wanafuatiliwa na maafisa forodha wa Italia kwa kutumia helkopita na boti kadhaa ziendazo kasi.
Moto mkubwa na moshi mzito vilionekana kutoka katika meli hiyo muda mfupi baada ya helikopta ya walinzi wa pwani wa Italia ilipokuwa ikizunguka angani kufuatilia kwa juu, huku boti ziendazo kasi zikiizingira.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa, baada ya kuona mambo yamekuwa magumu, watu hao waliokuwa katika meli hiyo yenye usajili wa Tanzania iliyotambulika kwa jina la Gold Star walijirusha baharini wakijaribu kutoroka ili wasikamatwe.
Hata hivyo, harakati zao hizo ziliishia mikononi mwa maafisa usalama wa Italia ambao waliwatia mbaroni.
Meli hiyo iliianza kufuatiliwa na maafisa forodha wa Italia siku kadhaa zilizopita wakati ikiwa inaelekea katika pwani ya Sicily baada ya kupata taarifa kuwa imebeba kiasi kikubwa cha dawa za kulevya (Hashishi) kabla ya jana kuamua kuivamia na kuizingira.
Helikopta ikizunguka angani, boti kadhaa ziendazo kasi ziliizingira meli hiyo na kisha maafisa forodha waliingia ndani na kufanya upekuzi.
Katika upekuzi huo ilibainika kuwa meli hiyo imebeba tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi ambazo nyaraka zinaonyesha kuwa zilipakiwa nchini Uturuki.
Maafisa wa Italia wamesema watu waliokuwamo ndani ya meli hiyo ni raia wa Misri na Syria na kwamba kabla ya kuitumia meli hiyo yenye urefu wa mita 82 na umri wa miaka 39, kwanza walilazimika kupata kibali cha kusafiria kutoka Tanzania ilikosajiliwa.
Boti za kuzima moto ziliitwa katika eneo hilo ili kuzima moto uliokuwa ukiwaka na baadaye meli hiyo ilichukuliwa hadi katika Bandari ya Syracuse katika pwani ya Sicily ambako watuhumiwa kwa sasa wanashikiliwa kwa mahojiano.
Msemaji wa Idara ya Forodha wa Italia, alisema meli hiyo ilikamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa za kiintelejensia kuwa imebeba dawa za kulevya, lakini hawakutarajia kama ingekuwa ni kiasi kikubwa kama kilichokamatwa na kwamba pia wameshtushwa na kitendo cha watuhumiwa kutaka kuilipua moto.
“Bila shaka lengo lao lilikuwa ni kutaka kupoteza ushahidi ili tushindwe kutengeneza kesi dhidi yao, lakini mpango wao ulishindwa na moto ulizimwa na dawa za kulevya tumefanikiwa kuzikamata” alisema na kuongeza: “Watu tisa waliokuwa ndani ya meli waliruka majini lakini hawakufanikiwa kufika mbali kwani pwani ilikuwa mbali hivyo waliokolewa na maafisa forodha na kisha kutiwa mbaroni,” alisema.
Hata hivyo, moto ulizimwa na meli hiyo imepelekwa bandarini ambako itafanyiwa upekuzi mwingine na watuhumiwa wanahojiwa na vyombo vya usalama vya Italia.
Kamanda wa Polisi Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema bado hajapata taarifa na kuahidi kufuatilia na kutoa taarifa wiki hii.
“Unavyoongea na mimi muda huu nipo nje ya nchi, lakini nashukru kwa taarifa nitafuatilia,” alisema.
Nzowa alisema kwa jinsi anavyopata ushirikiano kutoka kwa watu mbalimbali ni wazi kuwa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya watashindwa.
Katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai mwaka huu kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayohusiana na biashara ya dawa za kulevya yanayohusisha Watanzania kukamatwa nje ya nchi wakiwa na dawa za thamani ya mabilioni ya fedha.
Kufuatia kukamatwa kwa Watanzania hao ambao ilibainika kuwa baadhi yao walikuwa wakipitia katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hali hiyo iliilazimu serikali kupitia Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe kuingilia kati tatizo hilo.
Tukio la kwanza lilitokea Julai 5 mwaka huu baada ya wasichana wawili raia wa Tanzania waliokamatwa.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment