Friday, 13 September 2013

Membe abipu urais

Tetesi kwamba Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa na nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 zimezidi kukolea baada ya kuwaambia viongozi wa chama chake na wapiga kura wake wa Jimbo la Mtama kuwa hatagombea tena nafasi ya ubunge katika jimbo hilo kwa kuwa atakabiliwa na majukumu ya kitaifa na kimataifa.

Waziri Membe alirudia kauli hiyo wiki iliyopita wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa (Nec) wa wilaya ya Lindi Vijijini. 

Waziri huyo aliwahi kutoa kauli hiyo takribani mwaka mmoja uliopita akiwa jimboni kwake.

Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akitajwa tajwa kuwa ana nia ya kuwania nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ametoa kauli hiyo wakati ambao Rasimu ya kwanza ya Katiba mpya Ibara ya 94 kifungu cha 2(a) inakataza wabunge au madiwani kuteuliwa kuwa mawaziri au naibu mawaziri.

Ibara hiyo inaeleza kuwa: “Watu wafuatao hawatakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa Mawaziri au Naibu Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Wabunge wa Bunge la Tanzania Bara, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar au madiwani kutoka washirika wa Muungano.”

Membe alisema amechukua uwamuzi wa kutogombea tena nafasi hiyo ya ubunge ili apate muda wa kupumzika, baada ya kulitumikia jimbo lake la Mtama kwa kipindi kirefu cha miaka 15.

Membe alikaririwa na vyombo vya habari akiwaeleza wananchi wa Jimbo la Mtama kuwa  mwili wake umechoka na hivyo anahitaji kupumzika ubunge.

Alisema uongozi ni kazi ngumu, hivyo kama binadamu huchoka, hivyo anahitajika kupata mapumziko na kupisha nguvu mpya itakayoweza kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo. Kadhalika, katika mkutano huo Membe hakuwa tayari kufafanua majukumu ya kitaifa na kimataifa yatakayomkabili ifikapo mwaka 2015  ni yapi. 

Kulingana na siasa za Tanzania, majukumu ya kitaifa ambayo mwanasisa anaweza kuzungumzia ni kati ya nafasi mbili, moja urais au makamu wa rais ambao huchaguliwa kwa pamoja katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge.

Aidha, katika mkutano huo Membe aliwasisitizia wajumbe, wanachama na wananchi wa Jimbo la Mtama kuwa muda wa uchaguzi utakapofika wahakikishe wanamweka mbunge atakayeshirikiana nao katika kuongeza maendeleo ya jimbo na siyo kurudisha nyuma.

Aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba  wakati utakapofika wahakikishe wanaweka nguvu mpya kwenye jimbo lao kwa kuchagua mtu atakayefanya kazi ya kuwatumikia.

NIPASHE lilimtafuta Waziri Membe kufafanua juu ya uamuzi huo mzito aliouchukua una maana gani, lakini hakupatikana licha ya kupigiwa simu yake ya kiganjani na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms). 

Hata hivyo, mmoja wa watendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Ushirikiano wa Kimataifa, alilieleza gazeti hili kuwa Waziri huyo yuko nje ya nchi kikazi.

Ingawa Membe hajawahi kukiri wala kukanusha kugombea urais mwaka 2015, lakini aliwahi kusema kuwa muda wa kufanya hivyo bado na kwamba atatangaza ikiwa ataoteshwa na Mungu.

Baadhi ya makada ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakitajwa kwamba wana nia ya kuwania urais kuchukua nafasi ya Rais Jakaya Kikwete ambaye atamaliza muda wake kikatiba mwaka 2015. 

Wanaotajwa ni Membe, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Naibu Katibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mstaafu, Dk. Asha-Rose Migiro.

Wakati wa Mkutano wa 12 wa Bunge uliloahirishwa wiki iliyopita baadhi ya wabunge walimpigia debe la wazi Spika Anne Makinda, kwamba anazo sifa za kuwania urais mwaka 2015.

Waliompigia debe kwa kummwagia sifa Makinda ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki, aliyesema Makinda ni tishio kwa wanaowaza urais mwaka 2015.
chanzo:nipashe
 

No comments:

Post a Comment