Monday, 30 September 2013

Mlinzi afumaniwa na denti…apata kichapo yu mahututi!

Yupo baba mmoja mtu mzima ambaye kazi yake ni ulinzi katika shule ya sekondari. Huyu ni mlinzi wa amani shuleni na kazi yake ni kulinda wanafunzi pamoja na mali zao na zile za shule. Lakini anapokiuka miiko ya kazi yake na kufanya kinyume, hakika huyo siyo mlinzi tena bali mhalifu.
Mlinzi pamoja na majukumu yake katika shule anapaswa kuangalia usalama wa wanafunzi na kuhakikisha wanazingatia maadili mema ya shule. Lakini mlinzi huyu huyu anapoharibu wanafunzi badala ya kuwalinda, kuwaonya na kuwaweka katika mstari mzuri wa maadili, huyu ni mhalifu anayestahili adhabu.
Baba huyu,, amewahi kufanya kazi hiyo katika shule kadhaa na kote huko amekuwa akihamishwa kutokana na tabia yake ya kuwalaghai kimapenzi wanafunzi wa kike. Lakini si unajua siku za mwizi ni arobaini? Kote huko alikohamishwa alikuwa akikanusha kujihusisha na tabia hiyo chafu.
Kivumbi ni katika shule alikohamishiwa hadi yanamkuta makubwa ambayo huenda yakampotezea maisha kwani hivi sasa yuko taabani baada ya kichapo cha nguvu kutoka kwa raia wenye hasira kali.
baba huyu mtu mzima kabla ya kichapo cha hivi majuzi, alishawahi kukutwa katika mazingira ya kutatanisha na mwanafunzi wa kike wa shule ya kutwa, hali ambaye ilisababisha bibi wa mwanafunzi amfungulie mashtaka.
Ajabu ni kwamba siku aliyopata kichapo, ndiyo siku kesi yake ilikuwa ianze kusikilizwa mahakamani. Katika kesi hiyo, inasemekana mkewe aliuza eneo la shamba ili apate fedha za kumtolea dhamana.

Lakini kutokana na tabia hiyo ya kuwarubuni wasichana wa shule kimapenzi kuendelea, ikabidi awekewe mtego ili akamatwa na ushahidi.
Inaelezwa kuwa bibi yake na binti huyo baada ya kuona mjukuu wake anarudi usiku wa giza huku akiwa ananukia pombe akiwa na nguo za shule, aliamua kuweka mtego kwa kuwaweka watu wamvizie mjukuu wake anarudi saa ngapi na anakuwa na mtu gani.
Siku ya siku jamaa(mlinzi) akamtoa outing denti huyo wakaenda kujichana na ilipofika usiku wa saa nne hivi akawa anamrudisha kwa bibi yake. Kumbe umewekwa mtego wa watu wawavizie kisha wawakamate.
Jamaa alipokaribia karibu na nyumbani kwa binti, ndipo kikundi cha watu kilipojitokeza na kumweka chini ya ulinzi. Fikiria mlinzi anawekwa chini ya ulinzi kwa kubambwa na mwanafunzi wakiwa wote wamelewa chakari.
Jamaa akajaribu kutoroka ambapo alikimbilia kwenye ofisi ya kijiji iliyokuwa jirani kabisa na nyumbani kwa binti yule. Bahati Mwenyekiti alikuwa pale ofisini akisuluhisha tatizo la familia fulani. Jamaa akajitosa ndani.
Lakini kutokana na kelele za raia ambao wanamfahamu na walishamuonya hasa katika kesi iliyokuwa mahakamani, walivunja mlango wa ofisi na kumtoa nje, kisha kuanza kumtandika, kumbonda kwa mawe, huku wengine wakizishughulikia sehemu zake nyeti kwa kuzichoma sindano na ukatili mwingine.
 Mlinzi yule alipigwa vibaya hata kudhani kuwa amepoteza maisha. Ndipo polisi walipoitwa na walipofika wakitaka kumbeba akatoa sauti…”niokoeni jamani…niokoeni”. Watu wote walishangaa kwani walishajua jamaa kapoteza maisha.
Ndipo polisi wakamchukua na kuondoka naye na inaelezwa walimpeleka hospitali kwa matibabu, ili baadaye aweze kufunguliwa mashtaka kuhusiana na tukio lenyewe. Hadi juzi jamaa alikuwa mahututi.
Mpenzi msomaji, ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo. Si unajua msemo, ‘asiyesikia la mkuu, mbele huvunjika guu?’. Alionywa mara kadhaa lakini hakutaka kusikia, ona sasa yamemkuta ya kumkuta na bila shaka kilema cha maisha kimemfika kutokana na tabia yake mbaya iliyokwenda kinyume na maadili ya kazi yake.
Badala ya kuwa mlezi mzuri na mlinzi wa mali za shule, yeye amekuwa mharibifu na matokeo yake yamemfika ya kumfika.
Tabia hii ya watumishi wa shule kuharibu wanafunzi imekuwa ikipigiwa sana kelele ambapo baadhi ya walimu nao ni vinara wakubwa. Tena hawa ndiyo hata huwatia mimba ambazo huwafukuzisha shule wanafunzi na wengine huzitoa kwa njia mbalimbali ili wasijulikane.
Huu ni ukatili mbaya sana dhidi ya wanafunzi, kwanza huwadumaza kisaikolojia na pia huwaharibia elimu ambayo ni msingi wa maisha yao baadaye. Jamii ya eneo lilikotokea tukio hilo, bila shaka iko makini na nyendo za watumishi wa shule zinazowazunguka na pia inafuatilia mienendo ya wanafunzi.
Hii inatokana na ukweli kwamba jamii imeshaelewa umuhimu wa elimu kwa watoto wao na kwamba vikwazo vya aina yoyote vinavyojitokeza kama hilo la wanafunzi kurubuniwa kimapenzi ni lazima hupambana navyo

No comments:

Post a Comment