Wednesday, 11 September 2013

Sheikh adaiwa kumbaka binti wa miaka minane

KIONGOZI wa msikiti wa Masjid Maftah ulioko Misufini katika manispaa ya Morogoro, Alhaj Abdul Wazir, maarufu kama Sheikh Koba, anashikiliwa kwa mahojiano mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka nane, mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Sabasaba.
Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, zilisema mtuhumiwa huyo, anadaiwa kutenda tukio hilo chumbani kwake, Septembatatu, majira ya saa mbili usiku, huko Mbuyuni katika manispaa ya Morogoro.
Mashuhuda wa tukio hilo wakizungumzia mazingira ya tukio hilo, walidai kuwa Alhaj Koba, amekuwa akiishi nyumba tofauti na mkewe na kwamba siku ya tukio mke wake alimtuma mtoto wa nduguye kupeleka chakula kwa mumewe, lakini alichelewa kurudi, hivyo kuamua kumfuatilia kujua kulikoni.
“Alipofika kwenye nyumba anayoishi mumewe, aligonga na kumuulizia binti huyo, lakini alielezwa kuwa alishaondoka eneo hilo, lakini mtoto alijitokeza na kudai alikuwa bado ndani ya nyumba hiyo, na alipohojiwa kuhusiana na uchelewaji wake, alikiri alikuwa amebakwa hivyo tukio hilo kuripotiwa polisi,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Polisi walithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo, na kwamba uchunguzi zaidi bado unaendelea ili kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.
Katika tukio jingine, kijana Typhory Singa, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa, mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Lipangalala na mkazi wa Liami Ifakara wilayani Kilombero.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Septemba nane mwaka huu, majira ya saa nane mchana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili mtuhumiwa aweze kuchukuliwa hatua.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment