Wednesday, 11 September 2013

SMZ: Tutaifutia usajili meli iliyobeba bangi Italia

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekuja juu ikisema itawafungulia mashtaka wamiliki wa meli ya mizigo ya Kampuni ya Gold Star iliyokamatwa juzi ikiwa na tani 30 za bangi nchini Italia ikipeperusha bendera ya Tanzania na kuifutia leseni kwa kulichafua jina la Tanzania kimataifa.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar, alisema kuwa SMZ imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya meli hiyo kubeba dawa hizo za kulevya kinyume cha  kibali cha usajili wake.

Omar alisema  meli hiyo ilisajiliwa kwa madhumuni ya kubeba mizigo, lakini Kampuni hiyo imekiuka masharti ya Sheria ya Usajili wa Meli na ile ya Umoja wa Mataifa zinazozuia meli kubeba dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa kitendo cha meli hiyo kubeba dawa hizo huku ikiwa na bendera ya Tanzania imeidhalilisha Tanzania hivyo lazima ichukuliwe hatua.

Hata hivyo, alisema ni mapema kuzungumzia lini wataanza mchakato wa kufungua mashtaka kwa kuwa tukio lenyewe lilitokea juzi, hivyo lazima kuwapo na vikao vya watendaji wakuu watakaozungumzia uamuzi huo.

Alisema meli hiyo ilisajiliwa Oktoba 15, mwaka 2011 nchini Dubai katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Meli za Kimataifa Zanzibar, hivyo kisheria ni mali ya Tanzania, lakini wamiliki wake siyo raia wa Tanzania.

Alisema wamiliki wakuu wa meli hiyo ni Marshal Irend waliopo visiwa vya Caribbean, lakini jina la mmiliki pekee halijaweza kufahamika.

Omar alisema katika meli hiyo kulikuwapo na mabaharia tisa, saba wakiwa ni raia wa Syria na wawili waIndia.

Alifafanua kuwa mabaharia hao kwanza watashitakiwa nchini Italia na SMZ itapata muda wa kusikiliza utetezi wao  ili kufahamu kama hao ndiyo waliopakia dawa hizo au mmiliki wa meli hiyo ndiye aliyepakia ili waweze kumpata mtu wa kumshitaki.

Alisema baada ya kupata ushahidi huo, SMZ itawafungulia mashitaka Mahakama Kuu ya Zanzibar. Alisema mzigo wa dawa hizo zilizokamatwa katika meli hiyo haukutokea Tanzania, na  kwamba meli hiyo haifanyi kazi zake katika nchi za Afrika Mashariki bali katika Bahari ya Mediterranean.

“Ningependa Watanzania wajue kuwa ile meli siyo ya Tanzania, bali Tanzania inamiliki kisheria tu kwa kuwa ilisajiliwa katika moja ya ofisi za Tanzania zilizopo Dubai, sisi tunawafadhili tu,” alisema Omar.

Aliwataja mabaharia hao waliokuwa kwenye meli hiyo kuwa ni Ahmad Balkis, Hani Othman, Abdul Ramadhan Jalloul, Ahmad Dalileh, Bachar Alfran, Shadi Suleiman, Mustafa Jumaa, raia wa Syria na Anuj Chauhan na Munishwa wa India.

Katika kipindi cha kuanzia  Julai mwaka huu, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya biashara ya dawa za kulevya  yanayowahusisha Watanzania.

Watanzania hao wamekuwa wakikamatwa kwa nyakati tofauti nje ya nchi wakiwa na dawa hizo zenye thamani ya mabilioni ya fedha.

Ilibainika kuwa baadhi yao walikuwa wakipitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa na dawa hizo na kuilazimu serikali kupitia Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuingilia kati.

Tukio la kwanza lilitokea Julai 5, mwaka huu baada ya wasichana wawili raia wa Tanzania kukamatwa nchini Afrika Kusini wakisafirisha dawa hizo zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8

Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa hizo aina ya Cocaine na Heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6, akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea jijini Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hongkong.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara hiyo haramu ndani na nje ya nchi na kwamba.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na biashara hiyo ya dawa hizo.

Katika kipindi hicho,  Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na kuharibu taswira ya nchi katika duru za kimataifa.

 Sakata la meli hii linaibuka baada ya lile la Julai mwaka jana ambalo meli za mafuta za Iran zilizua kizaazaa baada ya kubainika kuwa zilikuwa zikipeperusha bendera ya Tanzania kwa lengo la kufanikisha biashara ya nishati hiyo.

Kwa mujibu wa sheria, upande wa Tanzania Bara serikali inaweza kutoa usajili wa meli inapobainika umiliki wake ni wa raia wa Tanzania kwa asilimia 50 tofauti na Zanzibar ambako hata Mtanzania akiwa na asilimia moja meli inaweza kusajiliwa na kupeperusha bendera ya Tanzania.

Baada ya kuibuka kwa meli hizo za mafuta, SMZ  iliibuka na kutoa taarifa kuwa sheria ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (Maritime Authority – ZMA) iliyoundwa kwa sheria Namba 3 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na kazi nyingine inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Usafiri wa Bahari Zanzibar ya mwaka 2006 (Zanzibar Maritime Transport Act 2006).

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa SMZ wa kipindi hicho, Hamad Masoud Hamad,  aliwasilisha taarifa yake kwa Baraza la Wawakilishi Julai 2, mwaka jana akithibitisha kusajiliwa kwa meli 10 za  Zanzibar ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania, lakini siyo za Iran ila zimetokea Malta na Syprus
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment