MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilishindwa kutoa uamuzi wa kuifuta au kutoifuta kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara maarufu nchini, Abubakar Marijan (50), maarufu kama Papaa Msoffe na Makongoro Joseph Nyerere kwa sababu bado haijamalizika kuandaliwa.
Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi, Hellen Liwa, kwamba kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya mahakama yake kuitolea uamuzi wa ama ifutwe au la, ila akasema kuwa hataweza kufanya hivyo, kwa sababu bado uamuzi hajamaliza kuuandaa.
Hata hivyo Hakimu Liwa alimtaka Wakili wa Serikali, Leonard Chalo, atoe msimamo wa kesi hiyo imefikia katika hatua gani, ambapo alisema jalada halisi la kesi hiyo lipo polisi, hivyo upelelezi bado haujakamilika na akaomba kesi hiyo iahirishwe.
Aidha, Hakimu Liwa aliendelea kumweleza Wakili Chalo atambue kuwa washitakiwa hao wamekwisha kuchoka, ndiyo maana wamewasilisha ombi hilo la kuomba wafutiwe kesi hiyo, na kwamba upande wa Jamhuri kila mara kesi inapokuja mahakamani unadai upelelezi haujakamilika.
Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba siku hiyo mahakama itaona upande wa Jamhuri umefikia hatua gani ili ipange tarehe ya kutoa uamuzi wa ama kuwafutia kesi washitakiwa au la.
Septemba 11, mwaka huu, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, aliwasilisha pingamizi mahakamani hapo kuomba mahakama hiyo ilikatae ombi la wakili wa washitakiwa, Daud Malima.
Wakili wa washitakiwa hao aliiomba mahakama iwafutie kesi hiyo kwani ni ya muda mrefu na hadi sasa upelelezi bado haujakamilika.
Wakili Kweka alidai kuwa kwanza mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji ndiyo maana washitakiwa waliposomewa shitaka lao hawakutakiwa kujibu chochote na kwamba ni Mahakama Kuu peke ndiyo yenye mamlaka hayo.
Februari 13, mwaka huu, Wakili wa Serikali, Charles Anindo, aliiomba mahakama kumuunganisha Nyerere katika kesi hiyo ambayo awali ilikuwa ikimkabili Msoffe peke yake, ambaye alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 10, mwaka 2012.
Washitakiwa wote walidaiwa kumuua kwa makusudi Onesphory Kituli, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 19 kama kilivyorekebishwa mwaka 2002 na kwamba kosa hilo walilitenda Oktoba 11, mwaka 2011, nyumbani kwa marehemu Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment