Dar es Salaam. Maandalizi ya kushambulia jengo la maduka la eneo la Westgate, Nairobi yalifanyika kwa miezi mingi.
Gazeti la New York Times la Marekani lilikariri vyanzo vyake ndani ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo jana vilivyosema kuwa mipango na mazoezi kwa ajili ya shambulizi hilo vilifanyika Somalia.
Magaidi kati ya 10 hadi 15 wa Al-Shabaab walivamia kwa silaha kwenye jengo la ghorofa nne la maduka na kusababisha vifo vya watu 67 kwa mujibu wa taarifa za Serikali ya Kenya na majeruhi 175. Magaidi watano walipoteza maisha kwenye tukio hilo.
Kitengo cha Mambo ya Nje cha Kundi la Al-Shabaab ndicho kilichokuwa na kazi ya kupanga shambulizi hilo.
Imeelezwa kuwa watekelezaji wa tukio la kigaidi walipitia mafunzo maalumu huko Somalia yaliyowawezesha kubaini michoro ya jengo pamoja na mbinu za kusafirisha silaha.
Utekelezaji
Gazeti hilo lilidai kuwa uratibu wa operesheni hiyo ulifanywa kwa uangalifu kwani wafuasi wa Al-Shabaab waliochaguliwa ni wale ambao walikuwa wanafahamu vyema Kiingereza na wenye uzoefu wa masuala ya kimataifa.
“Hawa jamaa pia waliandaa mchoro wa jengo hilo. Wakaandaa mkakati wa kupenyeza silaha ambazo walikuwa wamezileta kutoka Somalia,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.
Gazeti la New York Times, lilisema silaha zilizotumika kwenye uvamizi huo zilipenyezwa kupitia maeneo yalikuwa yakilindwa na askari wa kampuni binafsi za ulinzi.
Duru za usalama za Marekani zimeeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya askari walihongwa kutokana na kukabiliwa na ukata wa kutolipwa kwa wakati na waajiri wao.
Taarifa zinasema kuwa siku moja au mbili kabla ya uvamizi huo, inasemekana magaidi hao walipitisha kwa siri mikanda ya risasi kwa ajili ya kutumika kwenye bunduki zao aina ya `Short Machine Gun’ (SMG).
Baadhi ya wafanyakazi wa jengo hilo wanadaiwa kula njama na magaidi hao ili kufanikisha mpango wa kuingizwa kwa silaha hizo zilizotumika kwenye ugaidi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mmoja wa magaidi hao alikuwa amebeba nguo za kubadilisha ambazo angezitumia na wenzake kwa ajili ya kutoka nje ya jengo hilo pamoja na raia wakati wa kukimbia baada ya kufanya mauaji. Serikali ya Kenya imetoa orodha ya washukiwa wa shambulizi hilo wanaotoka Marekani na Uingereza.
Rais Uhuru Kenyatta alisema taarifa za kiusalama zimedokeza kuwa mashambulizi hayo yalitekelezwa na raia watatu kutoka Marekani na mwanamke mmoja wa Uingereza.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema imepokea taarifa za kuhusika kwa raia wake, lakini imesisitiza kuwa bado haiwezi kudhibitisha moja kwa moja mpaka pale itakapopata uhakika kwa njia ya vipimo vya kinasaba (DNA).
“Tunafahamu yaliyotokea Kenya, lakini hatuwezi kuthibitisha moja kwa moja kuhusika kwa raia wa Marekani, tunasubiri vipimo vya DNA pamoja na baadhi ya picha za kwenye mitambo ya CCTV... lakini tendo lililofanyika nchini Kenya ni la kinyama,” alisema ofisa mmoja wa usalama wa Marekani ambaye
hakutaka jina lake kutajwa alipohojiwa na New York Times.
Serikali ya Kenya imesema imedhibiti eneo zima la jengo na kuwaua baadhi ya magaidi hao ingawa nchi za Ulaya na Marekani zinaona kwamba kuna uwezekano baadhi ya wavamizi walifanikiwa kutoroka wakati wa kurushiana risasi.
chanzo:mwananchi
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment