Hali ya usalama kwa watu visiwani inazidi kutetereka, huku viongozi wa Kanisa Katoliki, wakizidi kushambuliwa.
Safari hii, Padre Joseph Mwang’amba wa Parokia ya Machui mjini hapa, amemwagiwa maji yanayoaminika kuwa tindikali.
Padre Mwang’amba, alishambuliwa na watu wasiojulikana jana saa 10:00 jioni, akiwa anatoka kwenye mgahawa wa ‘intaneti’ wa Sun Shine uliopo Mlandege.
Waliommwagia tindikali hiyo walitoweka na PadriMwang’amba kurudi ndani ya mgahawa huo kuomba msaada wa huduma ya kwanza, kabla ya kupelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema maji hayo yamemuathiri Padre Mwang’amba usoni, kifuani, mikononi, mapajani na kuchoma sehemu kubwa ya mbele ya nguo yake.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi kutoka Zanzibar, Mkadam, alisema Padre Mwang’amba ana tabia ya kwenda kwenye mgahawa huo mara kwa mara, kwa ajili ya kusoma na kutumia mtandao wa `intaneti’.
Alisema katika kwenda na kupata huduma hiyo mahali hapo, hakuna taarifa za kuwapo kutoelewana ama vitisho vya aina yoyote dhidi yake.
“Alipomwagiwa maji hayo, alikuja mwenyewe kituo cha polisi Mji Mkongwe kutoa taarifa, lakini polisi haikumhoji zaidi kwa sababu alitakiwa kukimbizwa hospitali kupata matibabu,” alisema na kuongeza kuwa hatahojiwa mpaka atakapopata nafuu.
Alisema wakati akifika polisi, hakuonyesha dalili za kuathirika hali ambayo ilikuwa tofauti baada ya kufikishwa hospitalini na kwamba hadi kufikia jana jioni, hakuna mtu aliyekamatwa.
Mkadam alisema Padre huyo anatoa huduma katika parokia ya Machui iliyoko eneo la Cheju mjini hapa.
Habari zaidi kutoka Zanzibar zilieleza kuwa Mwang’anda anahudumia kituo cha malezi ya vijana cha Cheju kinachoendeshwa na kanisa hilo.
Hili ni tukio la tano la kumwagia tindikali hapa Zanzibar katika mashambulio yaliyotokea kati ya mwaka jana na mwaka huu .
Katika tukio la kwanza Mkurugenzi wa Manispaa ya Zanzibar Rashid Ali Juma, alimwagiwa tindikali na baadaye Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alijeruhiwa na kemikali hiyo.
Wengine waliomwagiwa tindikali kwa nyakati tofauti ni Sheha wa Chumbuni, Mohamed Kidevu wakati mwezi Julai wasichana wawili wa Uingereza Katie Gee (18) na Kirstie Trup, walimwagiwa kemikali hiyo.
Wasichana hao waliokuwa wanajitolea kufundisha katika shule moja mjini hapa, walishambuliwa baada ya tukio la kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhili Suleiman Saroga.
Kwa upande wa mashambulio dhidi ya viongozi wa Kanisa Katoliki kujeruhiwa, Padri Mwang’amba ni mfululizo wa matukio hayo yaliyoanza na kushambuliwa Ambrose Mkenda, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi, wakati wa Sikukuu ya Krismasi, mwaka jana.
Tukio hilo lilifuatiwa na mauaji ya Padri Aloyce Mushi, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari mwaka huu, wakati akielekea kwenye ibada ya Jumapili saa 1:00 asubuhi.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment