Gaidi Samantha Lewthwaite maarufu kama ‘mjane mweupe’ raia wa Uingereza anayedaiwa kuhusika katika tukio la shambulizi la kigaidi jijini Nairobi, Kenyamwezi uliopita, amezua tafrani kubwa baada ya kuzuka uvumi kuwa ameonekana katika benki moja jijini Dar es Salaam.
Mjane mweupe ni gaidi anayehusishwa na tukio la ugaidi kwenye kituo cha biashara cha Westgate jijini Nairobi Septemba 14, mwaka huu na anatafutwa na vyombo vya usalama vya Kenya na polisi wa kimataifa (Interpol) kwa udi na uvumba.
Gaidi huyo anadaiwa kuwa ndiye aliyeongoza katika mashambulizi hayo yaliyoua watu 67 na kujeruhi zaidi 200 katika kituo hicho na kufanikiwa kutoroka kwa kujifanya kuwa mmoja watu waliokuwa wakijiokoa.
Kutokana na kutoroka kwa gaidi huyo, vyombo vya usalama katika nchi za Afrika Mashariki vimekuwa macho kufuatilia watu ambao wanahisiwa kuwa wanahusika na shambulizi hilo linalodaiwa kusukwa na kutekelezwa na mtandao wa kigaidi wa al Shaabab kwa kushirikiana na Al Qaeda.
Kufuatia hali hiyo, mwanamke mmoja raia wa Uingereza, jana alikamatwa na Jeshi la Polisi Tanzaniabaada ya kutiliwa shaka akifananishwa na gaidi huyo mtukutu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata ambazo pia zimesambazwa katika mitandao ya kijamii, mwanamke huyo alikamatwa katika benki ya Exim tawi la Tower jijini Dar es Salaam baada ya wafanyakazi wa benki hiyo kumtilia shaka.
Chanzo cha habari kutoka katika benki hiyo kilieleza kuwa mwanamke huyo shombe alifika katika ofisi za benki hiyo makao makuu kuomba tenda ya kusafisha jengo.
Mwanamke huyo ambaye Jeshi la Polisi bado halijataja jina lake, alifika katika benki hiyo Jumatatu ili aonane na meneja, lakini aliambiwa aende kesho yake yaani juzi.
Habari zinasema kuwa baada ya kufika makao makuu ya benki hiyo, aliambiwa meneja hayupo, ndipo alipoibua hoja mpya na kuwaambia wafanyakazi wa benki kuwa angelipenda kufungua akaunti kwenye tawi la benki hiyo.
Baada kukubaliwa aliambiwa awasilishe nyaraka za kumtambulisha, lakini akadai ni raia wa kigeni na hana nyaraka zozote na alipoulizwa anakaa wapi, alidai kwenye nyumba za kupanga za Uhuru Heights.
Wafanyakazi wa benki hiyo baada ya kuona maelezo yake hayajitoshelezi, walitoa taarifa polisi wanaolinda jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jirani na benki hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Polisi walifika eneo hilo na kumkamata mwanamke huyo na kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi na alipofanyiwa uchunguzi, ilibainika alivaa lenzi kwenye macho na pia usoni alikuwa amejipaka vitu ambavyo vilikuwa havionyeshi vizuri uso wake.
Kufuatia hali hiyo, polisi walimwamuru anawe uso na baada ya kufanya hivyo, sura yake ya Kishombe ikapotea na kubaki kama Mzungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Manongi, alipolizwa kuhusu tukio hilo, alisema hakuwa na taarifa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alithibitisha kukamatwa kwa mwanamke huyo katika benki ya Exim baada ya kutiliwa shaka na wananchi.
Alisema baada ya kumfanyia uchunguzi, ilibainika kuwa siyo gaidi kama ilivyokuwa inahisiwa, badala yake na ana mume ambaye yupo jijini Dar es Salaam.
“Huyu mwanamke ni raia wa Uingereza, alipokamatwa alikutwa amevaa hijab na kimsingi wananchi ndiyo waliomtilia shaka, lakini siyo gaidi kama yule anayetuhumiwa kufanya ugaidi jijini Nairobi, Kenya,” alisema Kova. Kamishna Kova alisema mwanamke huyo aliachiwa baadaye baada ya kubainika kuwa ameolewa na mume wake yupo Dar es Salaam.
Alisema kilichowafanya wananchi wamtilie wasiwasi ni uvaaji wake wa nguo ambao uliwafanya wahisi huenda anafanana na gaidi wa tukio la Kenya.
Kamishna Kova alipongeza wananchi kwa jinsi wanavyokuwa makini katika suala la ulinzi na usalama wa nchi yao kwa kuwashuku watu ambao hawawaelewi na kuwataka kuendelea kushirikiana na jeshi hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi, DCP Thobias Andengenye, alitoa taarifa kuwa jeshi hilo litamsaka gaidi Samantha Lewthwaite anayedaiwa kupitia mpaka wa Namanga mkoa wa Arusha kabla ya kwenda kufanya tukio Nairobi ili kumzuia kufanya uhalifu zaidi.
Andengenye alikuwa akihojiwa katika kipindi cha kipima joto kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV kilichokuwa kikijadili Watanzania wamejifunza nini katika kuchukua hatua juu shambulio la ugaidi lililotokea Nairobi.
Andengenye alisema Jeshi la Polisi limejipanga kumsaka gaidi huyo ili asije akatenda uhalifu zaidi na kwamba ufuatiliaji wa mwanamke huyo hautafanywa kwenye mipaka bali hata ndani ya nchi.
No comments:
Post a Comment