Thursday, 3 October 2013

Sheria ya kuwabana wanaoambukiza virusi kwa makusudi yalalamikiwa

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki amesema adhabu inayotolewa dhidi ya watu wanaowaambukiza wenzao kwa makusudi ugonjwa wa ukimwi bado inalalamikiwa kuwa ni ndogo, hivyo kuna haja ya kuangaliwa ili iongezewe ukali.

Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa madiwani na mameya kuhusu majukumu ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania(Tacaids), Sera ya Ukimwi na sheria za ukimwi.

Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiambukiza wenzao virusi vya ugonjwa wa ukimwi kwa makusudi na pale inapobainika adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano.

Hata hivyo, alisema adhabu hiyo inalalamikiwa kuwa ni ndogo.

Kairuki alisema Tacaids wataliangalia suala hilo na kupendekeza nini cha kufanya katika sheria hiyo na ofisi yake kuangalia kama kutakuwa na hoja ya msingi ili ifanyiwe kazi na wabunge kwani wao ndiyo wenye maamuzi ya mwisho katika suala hilo.

"Ki ukweli adhabu inayotolewa ni ndogo mtu anabainika kamuambukiza labda mtoto hata kama ni mtu mzima ugonjwa wa ukimwi halafu afungwe miaka mitano, ofisi yangu italiangalia hilo kwa kushirikiana na Tacaids," alisema.

Alisema kwa sasa kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa wanawake ni asilimia 6.2 na kwa wanaume ni  asilimia 3.8.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Fatuma Mrisho alisema mkakati ni kutoa mafunzo kwa mikoa yote na kwamba wameamua kuanza na mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa maambukizi ya virusi vya ukimwi yapo juu kuliko maeneo ya vijijini.

Alisema madiwani hao wataenda kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha wananchi wanaifahamu sheria ya ukimwi ili tatizo la maambukizi liweze kupungua
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment