MADAKTARI wawili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Wambura Chacha na mwenzake bingwa wa upasuaji katika Kitengo cha Mifupa (MOI), Prof. Joseph Kahamba, jana walionja adha ya kuondolewa kwenye nyumba kutokana na deni la pango.
Madaktari hao ambao wanaishi katika nyumba namba 355 mali ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mtaa wa Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, walikumbwa na mkasa huo baada ya mwajiri wao, Muhimbili, kulimbikiza deni la miezi 15 linalofikia sh 9,738,000.
Mmoja wa madaktari hao, Profesa Kahamba ambaye alikuwepo wakati wa shughuli hiyo, alikiri kuwepo kwa limbikizo hilo la deni la pango, ambalo alidai kuwa haliwahusu wao, na kwamba ni tatizo la mwajiri wao ambaye ameshindwa kulipa kwa kipindi chote hicho.
“Nafikiri nyinyi waandishi mngekwenda kumuuliza mwajiri wetu, ndie anawajibika kulipa deni hili japo sisi ndio waathirika, na kama mnavyoona vyombo viko hapa nje vimenyeshewa na mvua, ni udhalilishaji kwa kweli,” alifafanua.
Meneja wa Kitengo cha Kukusanya Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga aliwaamuru madaktari hao kwa hiari yao kutoa nje vyombo vyao jambo ambalo waliliafiki na kutekeleza kabla ya kuamua kulipa deni hilo wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwanasenga alieleza kusikitishwa na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na uongozi wa Muhimbili kwa kipindi kirefu sasa bila utekelezaji.
“Hawa ni madaktari, wamefikia hatua ya kudhalilika namna hii, tumefanya jitihada zote za kutatua tatizo hili kwa kipindi kirefu sana, lakini uongozi wa Muhimbili umekuwa ukitoa ahadi ambazo hazitekelezeki na sheria inatutaka kumwondoa ndani ya nyumba mpangaji yeyote baada ya kushindwa kulipa kwa miezi mitatu tu,” alifafanua.
Kwa mujibu wa meneja huyo, hadi sasa Muhimbili inadaiwa na shirika hilo jumla ya sh milioni135.6 yakiwa ni malimbikizo ya malipo ya pango kwa vipindi tofauti.
“Hatua hii ni endelevu hususan kwa Muhimbili, haijawahi kutokea kulimbikiza deni kubwa namna hii, wamekuwa wakilipa vizuri sana huko nyuma, sijui kuna tatizo gani kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na meneja huyo, Dk. Chacha anadaiwa sh 4,674,000 na Prof. Kahamba ambaye anaishi juu ghorofani anadaiwa sh 5,064,000.
Baada ya kuona hali inawaendea vibaya kwa familia zao kwa kushinda nje, madaktari hao waliamua kukimbia benki na kulipa deni hilo kwa maelezo kuwa watamalizana na mwajiri wao.
Uongozi wa Muhimbili haukupatikana kutoa ufafanuzi wa kuchelewa kulipa deni hilo.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment