Thursday 17 October 2013

Mamaye Ufoo Saro atolewa risasi tano, Mtaalam aeleza kwa nini muuaji aliua

Mwili wa Anastazia Saro, mama mzazi wa mtangazaji na mwandishi wa kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Jumapili iliyopita, ulifanyiwa uchunguzi jana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), na kukutwa na risasi tano.

Anastazia aliyeuawa wakati akisuluhisha ugomvi kati ya binti yake Ufoo na mzazi mwenzie, Anthery Mushi, alikutwa na risasi hizo katika sehemu kadhaa za mwili wake.
Mushi mbali na kumuua Anastazia, pia alimjeruhi kwa risasi Ufoo kisha kujilipua mwenyewe na kufariki dunia papo hapo.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Allelio Swai, Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya Anastazia wakati akizungumza  muda mfupi kabla ya mwili huo kutolewa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, na kupelekwa Kibamba kwa ajili ya ibada ya mazishi tayari kusafirishwa kwenda Machame kijiji cha Shari kwa ajili ya mazishi leo.

Swai alisema kuwa katika uchunguzi wa mwili huo ambao hata hivyo, hakumtaja daktari aliyeufanya, baadhi ya ndugu wa marehemu walihudhuria.

Swai alifafanua kuwa risasi hizo zilikutwa katika maeneo ya mapafu, maini na tumbo.

Kwa mujibu wa Swai mwili huo ulitakiwa kufanyiwa uchunguzi mapema asubuhi, lakini ulichelewa kutokana daktari huyo kuwa na majukunu mengine, walilazimika kusubiri kwa muda.

Mwili wa mama huyo uliondolewa hospitalini hapo saa 7:30 mchana baada ya kukamilika kwa taratibu zote.

Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo na kuondoa risasi hizo, alikataa kuzungumza chochote zaidi ya kusema: “Siwezi kulizungumzia jambo hili kwa kuwa nimeshakamilisha nilichotakiwa kukifanya.”

Baadhi ya ndugu wa marehemu Anastazia waliokuwapo eneo hilo na walioshuhudia uchunguzi wa mwili, walisikika wakisema kuwa kitendo alichokifanya Mushi ni cha kinyama kutokana na kutumia risasi nyingi kumuua ndugu yao.

Wakati huo huo, Ufoo hataweza kushiriki mazishi ya mama yake kutokana na matibabu anayoendelea kuyapata, hospitalini hapo.

Swai aliiambia NIPASHE kuwa walimtaarifu Ufoo juu ya mipango ya mazishi ya mama yake na kwamba naye ametoa ruhusa ili mama huyo azikwe hata kama yeye (Saro) hataweza kuhudhuria mazishi hayo kutokana na hali yake.

“Niliongea na Ufoo ili kumfahamisha kuhusu mipango ya mazishi naye alitutaka tuendelee na mipango hiyo hata kama yeye atashindwa kumzika mama yake, lakini cha msingi alituomba tuhakikishe kuwa mama yake anazikwa salama,” alisema Swai.

MWANASAIKOLOJIA AMZUNGUMZIA MUSHI

Wakati hayo yakijiri, Mhadhiri Mwandamizi katika mambo ya Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Kitila Mkumbo, amesema kulingana na taarifa za mauaji ambazo amekuwa akizisoma kwenye vyombo vya habari juu ya mauaji hayo yalivyofanyika, ni dhahiri muuaji alikuwa amefikia ngazi ambayo hasingeweza kuacha kufanya unyama huo.

Alisema mtu huyo  alikuwa amejiandaa kufanya tukio hilo kwa muda mrefu kimkakati na kimaandalizi.

Alifafanua kuwa mhusika wa tukio hilo alikuwa ameshafikia katika hatua ya mwisho ya maamuzi inayoitwa tafsiri ya akili ambayo huwa ni vigumu kwa mtu kujizuia kutenda jambo.

Alisema kuna hatua tatu ambazo ni stress (msongo wa mawazo), depression (sonona) na tafsiri ya akili ambazo mtu anaweza kuzipitia kabla hajachukua maamuzi.

“Kuna kitu kinaitwa fluctuation, lazima kilitokea kati yake na familia hiyo siyo bure, lakini angekuwapo yeye mwenyewe angetueleza, sisi hatuwezi kujua,” alisema Dk. Mkumbo.

Dk. Mkumbo alisema kuwa sehemu aliyokuwa anafanya kazi marehemu Mushi (Darfur) siyo kigezo kikubwa cha kuamua kufanya tukio lile japokuwa watu wengi wanaoishi katika mazingira ya kuona maiti za watu huwa ni wepesi kuua.

Alisema hicho siyo kigezo cha marehemu kufanya kitendo hicho kwa kuwa hakuna mwanadamu asiyeogopa kifo.

Kuhusiana na iwapo wanajeshi wanaotoka katika operesheni za kijeshi nje ya nchi kama wanapatiwa ushauri (councelling), Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Erick Komba alisema: “Mafunzo anayopata mwanajeshi yanalenga kumjenga na kumpa uwezo wa kuyakabili mazingira mbalimbali ndani na nje ya nchi kimaumbile na kisaikolojia,” alisema.

Meja Komba alisema mwanajeshi ana uwezo wa kuishi kwenye mazingira yoyote kwa kipindi kirefu kijasiri.

“stress management-(jinsi ya kubaliana na msongo) inafanyika vizuri kwa kufanya michezo mbalimbali kwa pamoja ambayo inaimarisha fiziki (ukakamavu),”

Aliongeza kuwa maisha ya mwanajeshi ni ya umoja na ushirikiano, kitu ambacho kinamfanya ayakabili mazingira yake vizuri, na kuweza kutekeleza majukumu ya jeshi kiufasaha na kiuweledi. 

Alisema kwa kipindi wanapokuwa katika operesheni mbalimbali za ulinzi wa amani pamoja na mambo mengine wanapewa ushauri.

HALI YA UFOO YAZIDI KUIMARIKA
Ofisa Habari wa  MNH, Aminiel Aligaesha, alisema jana kuwa hali ya Ufoo inaendelea vizuri kulinganisha na siku za nyuma.

Alisema kwa sasa yupo katika jengo la matibabu ya moyo na kueleza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya daktari anayemuhudumia, Ufoo anahitaji mapumziko zaidi.

“Kwa sasa Ufoo haitaji kuonana na mtu, anahitaji kupumzika zaidi kama daktari alivyoniambia na kwa kifupi yupo katika wodi ya kawaida tu,” alisema Aligaesha.

SIMANZI YATAWALA KUAGA ANASTAZIA
Mwili wa marehemu Anastazia uliagwa jana katika Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibwegele Kibamba Shule kabla ya kuelekea kijiji cha Shari Wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro kwa mazishi.

Waumini na wanakwaya ya Uinjilisti wa Kanisa hilo waliangua vilio baada ya jeneza la mwili wa marehemu ambaye alikuwa mwanakwaya na mweka hazina wa kanisa kufika kanisani hapo.

Kadhalika, ibada iligubikwa machozi na simanzi, hali iliyosababisha kusimama kwa muda.

Mchungaji wa Kanisa hilo, Magret Shekolowa, aliwaeleza waumini hao kuwa na moyo wa subira hasa katika kipindi hiki na kuwataka kuacha kulia badala yake waiombee Tanzania kwani kumekuwa na matukio mengi ya mauaji ya kinyama.

Akitoa salamu za rambirambi Mkurugenzi wa ITV, Joyce Mhavile, huku akitokwa na machozi ya huzuni alisema: “Jana nilikwenda kumuona Ufoo akaniomba nitoe salama za mwisho nisimame kwa niaba yake, nami nasema poleni sana.”

Marehemu alizaliwa mwaka 1957 huko Mbulu mkoani Arusha na alifariki juzi baada ya kushambuliwa kwa risasi tano na Mushi.


 Chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment