Friday, 18 October 2013

Simanzi mazishi ya mamaye Ufoo Saro!!!!

Simanzi ilitanda katika familia ya marehemu, Anastazia Saro (56), mama mzazi wa mwanadishi na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro, baada ya msafara uliokuwa umeubeba mwili wake kuwasili nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi.

Msafara huo ulipokewa kwa majonzi yalioambatana na vilio kutoka kwa jamaa, ndugu, marafiki wa familia hiyo na waombolezaji waliokusanyika katika kijiji cha Shari, tarafa ya Machame, wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Wakati mwili huo ukiwasili kijijini hapo, jana alfajiri, waombolezaji kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro, walionekana kwa nyakati tofauti wakijifariji kwa sala huku baadhi ya ndugu wa marehemu kutoka Manyara wakiangua vilio kwa saa kadhaa wakisema kwamba Mwenyenzi Mungu ndiye analijua kusudio la aliyetenda unyama huo kwa kuwa ndugu yao hakustahili adhabu hiyo kama alivyotekeleza muuaji.

Anastazia aliyeuawa wakati akisuluhisha ugomvi kati ya Ufoo na mzazi mwenzie, Anthery Mushi, alikutwa na risasi tano katika sehemu kadhaa za mwili wake.
Mushi mbali na kumuua Anastazia, pia alimujeruhi kwa risasi Ufoo kisha kujilipua mwenyewe na kufa papo hapo.

Kutokana na majeraha makubwa ya risasi aliyopata Ufoo, hakuweza kusafi kumzika mama yake na amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Afya yake inaendelea kuimarika siku baada ya siku.

Baadhi ya waombolezaji wakilia na kupoteza fahamu baada ya kudondoka chini kutokana na mshituko uliotokana na kuuona mwili wa Anastazia aliyeuawa alfajiri ya Jumapili ya iliyopita.

“Ee Mungu wangu, wewe ndiye unayejua Anthery alipanga nini kabla ya kutekeleza unyama huu kwa kuwa ndugu yetu hakustahili adhabu aliyopewa. Nenda katende muujiza katika familia hii ambayo imebaki na ukiwa, tena likiumiza familia ya Saro na kuliacha taifa katika majonzi makubwa,” alisema Winfrida Nkya.

Haikuwa kazi rahisi kwa kiongozi wa msafara uliousafirisha mwili wa marehemu Anastazia, kutokea Jijini Dar es Salaam kuwatuliza waombolezaji nyumbani kwa marehemu, hata wakati ulipopelekwa katika Usharika wa Uraa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa ajili ya ibada ya maziko kutokana na mamia ya waombolezaji kujikusanya na kujitenga katika makundi wakijadili tukio hilo la mauaji ya kikatili.

Akisoma wasifu wa marehemu baada ya kufikishwa katika Kanisa la Uraa lililopo chini ya Jimbo la Hai katika Dayosisi ya Kaskazini, msemaji wa familia, Allelio Swai, alisema marehemu Anastazia alifikwa na mauti hayo baada ya kupigwa risasi na mkwewe Anthery Mushi ambaye alikwenda nyumbani kwa mama huyo eneo la Kibamba CCM, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Taarifa ya madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inaonyesha kuwa Anastazia Saro alifariki dunia baada ya kushambuliwa kwa risasi tano katika mwili wake, lakini tunamshukuru Mungu, juzi Polisi na madaktari hao waliufanyia uchunguzi mwili wake na tukapewa kibali cha kuusafirisha kuja kuuzika hapa Uraa,” alisema Swai.

Baba mdogo wa Ufoo Saro, Eshikaeli Saro, akizungumza katika ibada ya mazishi kanisani hapo, alisema kuwa familia hiyo licha ya kufikwa na msiba mkubwa, inatoa shukrani kwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Regnald Mengi, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Redio One, Joyce Mhavile pamoja na wafanyakazi wa IPP kwa kuifanya familia hiyo iweze kuufikisha mwili wa marehemu Machame na kuzikwa katika makaburi ya kanisa.

“Hatuna cha kumlipa Dk. Mengi, Mkurugenzi wa ITV/Redio One, wafanyakazi wa IPP wala ndugu na jamaa waliotusindikiza hadi tunampumzisha Anastazia hapa Uraa. Mungu ndiye atawalipa,” alisema Eshikaeli.

Hata hivyo, katika mazishi hayo, Mkuu wa Jimbo la Hai la KKKT, Mchungaji Aminirabi Swai, alisema kifo cha Anastazia kinafungua ukurasa mpya kwa jamii kumtanguliza Mungu kabla ya kutenda jambo.

“Tunamzika mama yetu, lakini jamii, inapaswa kujua kwamba iko haja ya kumtanguliza Mungu kabla ya kila jambo kwa kuwa yeye anao uwezo wa kubadili kila anachopanga mtu kabla ya kumshirikisha.
Inaumiza, lakini hatujui kila mtu ataitwa mbinguni kwa njia gani na kila mtu lazima atatangulia kwa staili yake,” alisema Mchungaji huyo na kuwataka waliohudhuria kumuombea Ufoo Saro apone.

Mazishi hayo yalihudhuriwa pia viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga, Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya hiyo, makachero wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro na Viongozi wa vyama vya Siasa akiwemo Gavana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, Basil Lema.

MUSHI KUZIKWA KESHO
Wakati huo huo, Anthery Mushi anatarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji cha Ongoma eneo la Uru , Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) imetuma ujumbe wa watu wanne kwenda mkoani Kilimanjaro katika mazishi hayo. Mushi alikuwa mfanyakazi wa UN nchini Sudan.
 
Chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment