Polisi kwa kushirikiana na wananchi wakiwamo walinzi wa jadi Sungusungu katika kijiji cha Zawa, kata ya Mwang’honoli, wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, wamefanya kazi ya ziada kufukua kaburi la mama mmoja aliyeuawa Septemba 28 mwaka huu na kuzikwa nyuma ya ukuta wa nyumba yake aliyokuwa akiishi.
Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Antonia Sado Jitinde (50), inadaiwa ailiuwa na mchugaji wa mifugo yake pia mkazi wa kijiji cha Zawa kwa kushirikiana na wenzake wawili kwa kupigwa na shoka na jembe kichwani usiku wa manane na kasha kuzikwa ndani ya kaburi fupi kando ya ukuta wa nyumba yake kijijini hapo.
Akisimulia mauaji hayo ya kusikitisha, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwang’honoli, Jilaba Mwigulu aliiambia NIPASHE kuwa, kuuawa kwa mwanamke huyo kuligundulika Oktoba 30 mwaka huu saa 7 mchana, baada ya wananchi na majirani wa zake kumuliza mchugaji huyo wapi aliko mama huyo baada ya kutoonekana nyumbani hapo kwa kipindi kirefu huku yeye akiuza baadhi ya ng’ombe wa mama huyo jambo lililo wastua wanakijiji wenzake.
Afisa huyo alisema wananchi hao walimbana mchungaji huyo aliyekuwa ameajiriwa na mama huyo kumchungia ng’ombe wake 30 kwa vile alikuwa akikabiliwa na uzee na alikuwa akiishi na mtoto wa ndugu yake mwenye umri mdogo wa miaka minane ambaye isingekuwa rahisi kumudu kuchunga ng’ombe hao badala ya kwenda shule.
Alisema baada ya kubanwa kwa maswali na majirani ni wapi aliko mama huyo na ni kwanini anauza mifugo ya tajiri yake wakati hawamwoni, mchungaji huyo alidai mama huyo alikuwa safarini Bulyanhulu wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga akisaka dawa ya kuzindika mifugo yake isiibiwe na watu wasio wema na kwamba alikuwa amemwagiza auze ng’ombe na amtumie fedha kwa jili ya kununua dawa hiyo kwa mganga.
Taarifa hizo zilitolewa kwa viongozi wa Sungusungu ambao nao walimhoji na ndipo alipo toboa siri ya kumuua mama huyo kwa kushirikiana na wenzake wawili wote wakazi wa kijiji cha Zawa.
Alisema wananchi walishangaa kuona jinsi walivyo mzika kwani kaburi lake lilikuwa fupi na kusababisha kuwa na tuta kubwa kando ya nyumba ya mama huyo na kuonekana kama ni tuta la kuchoma mkaa na walipofukua kaburi waliukuta mwili ukiwa umeviringishwa katika shuka maarufu kwa jina la shuka za Kimasai au za Kimbulu.
Mwigulu alisema baada ya kutoa shuka hizo waliukuta mwili wa marehemu ukiwa umeoza na ghafla kichwa kilikatika jambo lililoamsha kilio na huzuni kwa wananchi walishirikiana na polisi na madaktari kutoka mjini Maswa waliofanya uchuguzi na kubaini kuwa alipigwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Alisema baada ya uchuguzi wa kidaktari polisi waliaruhu mabaki ya mwili huo kuchukuliwa na ndugu wa marehemu na kwenda kuzikwa upya na kwa heshima katika kijiji cha Mahaha wilaya ya Magu mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi Salum Msagi amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba watuhumiwa wote watatu wanashikiriwa na polisi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamailika.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment