Saturday 2 November 2013

Malengo ni ufunguo wa mafanikio yako.


Inawezekana katika kuhakikisha unapata mafanikio wakati mwingine ilikulazimu kulala muda mfupi zaidi, kuhatarisha maisha yako katika safari mbalimbali nakadhalika, sasa jiulize unafanya hayo yote kwa ajili ya kutaka kufikia malengo yapi hasa uliyojiwekea? 

Wengi wameingia kwenye ujasiriamali kwa ajili ya kutafuta mafanikio, na kilele cha mafanikio hupimwa kwa fedha na mali wanazopata, je umewahi kujiuliza ni kiasi gani cha kipato au mali unahitaji kupata na utapataje? Ni nini hasa ungependa kiwe kipimo cha mafanikio yako?

Umewahi kujiuliza kwanini baadhi ya wajasiriamali wanashindwa kufikia ndoto zao? Umeshawahi kujiuliza kwanini kuna wajasiriamali waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa? Hawa waliofanikiwa wamewezaje kupata mafanikio waliyonayo na wengine wameshindwa?

Amka ndugu mjasiriamali, malengo ni silaha ya kukupeleka kule unakotaka. Acha kufanya mambo kimazoea kwa kuwa tu unapata hela ya kula na kulipa ada, elewa kuwa malengo yenye kufaa yanaweza kukupeleka mbali zaidi kuliko pale ambapo umebaki muda mrefu.

Wajasiriamali wengi hasa wa chini, hawajagundua nguvu iliyopo katika malengo ya biashara, ndiyo maana wengi wao wanabaki katika hali ya kawaida kwa kile wanachofanya. Ukiwauliza watakwambia mitaji ni shida, hichi ni kilio cha wengi!

Yafaa kuelewa tunapozungumzia malengo tunamaanisha nini zaidi. Ndugu mjasiriamali elewa kwa kifupi kuwa malengo ni hali ya kupanga, kuamua na kujiwekea kitu unachotaka kufanya na matokeo tarajiwa katika muda fulani. Malengo ni ndoto ya kweli unayotaka kuipata.

Kwa mfano mpaka sasa mwezi wa 11 tunaelekea mwishoni mwa mwaka, je ulijiwekea malengo gani katika biashara yako? Chukua kalamu na karatasi jikumbushe yale malengo uliyojiwekea na jiulize yapi umefanikiwa au hujafanikiwa na kwa kiasi gani. 

Elewa ndugu mjasiriamali malengo yamegawanyika katika sehemu mbili, yapo malengo ya muda mfupi, haya ni malengo yanayowekwa katika kipindi kifupi cha muda kama siku, wiki au mwezi, malengo yasiozidi mwaka mmoja. Je, umekuwa na malengo gani ya muda mfupi?

Vilevile kuna malengo ya muda mrefu, haya ni malengo yanayowekwa kwa kipindi zaidi ya mwaka mmoja. Kwa kawaida malengo ya muda mrefu hufikiwa kwa msaada wa malengo ya muda mfupi. Safari moja hutengeneza safari nzima, je malengo yako ya muda mrefu ni yapi?

Wajasiriamali wengi huegemea katika kupata kesho au keshokutwa huku wakisahau kuwa kupata mafanikio sio jambo la kulala na kuamka. Wengi hufikiria kupiga ‘mabao’ ya haraka na si kujijenga. Unahitaji ujijengee msingi mzuri wa mafanikio unayotamani kuyapata.

Yafaa kukumbuka kuwa malengo katika biashara lazima yapangwe kwa kuhusisha muda mrefu na mfupi, mfano kuongeza faida, kuboresha bidhaa, kubuni bidhaa mpya, kupanua wigo wa soko lako nakadhalika yote haya yanagitaji muda na namna bora ya kuyafikia.

Kutokuwa na malengo kwa wajasiriamali wengi ndiko kunakopelekea watu wengi kufanya biashara zilezile wanazofanya wengine. Watu wengi wanafanya mambo kwa kuiga, malengo yatakusaidia kufanya vitu tofauti na kuwa mbunifu.

Kuwa na biashara au mawazo ya biashara bila malengo mahsusi ni kama vile kuanza safari bila mwelekeo, hujui uanzie wapi uishie wapi. Malengo ni jambo ambalo linapaswa kuwatofautisha wajasiriamali kwani ni vigumu kuwa na malengo yenye kufanana.

Fikiria wajasiriamali waliofanikiwa nchini kwetu, wapo wenye majina makubwa na madogo, ukiwauliza moja ya siri ya mafanikio yao watakwambia ni pamoja na kujiwekea malengo, kuyasimamia na kupata matokeo tarajiwa. 

Kama hawa waliweka malengo yao na kupata mafanikio, ni kitu gani kinakuzuia kujiwekea malengo yako, uyahangaikie na hatimaye upate matunda unayotamani? Je umeashau msemo mbuyu ulianza kama mchicha, kila kitu kinawezekana kwa hatua!

Malengo ni muhimu kwa wajasiriamali, ni kama vile ramani mkononi mwa mtalii ambayo inatoa mwelekeo wa safari, wapi aanze, wapi apumzike, wapi na lini asimame. Bila malengo ya safari maana yake mtalii ataishia kuzunguka tu.

Kama ilivyo ramani, mjasiriamali ukiwa na malengo yenye kufaa itakusaidia  kujua hali halisi ya biashara yako, mbinu za kuziingiza katika biashara, na njia za kutumia ili kuweza kufikia mafanikio unayotamani kila siku.

Kutokana na umuhimu wa malengo ulivyo katika kutafuta mafanikio, mjasiriamali lazima ‘ulale macho’ ili kuhakikisha unafikia ndoto zako. Itakulazimu kufahamu uanzie wapi, wapi upumzike, na wapi uongeze bidii na wapi upambane.

Malengo ni muhimu katika biashara yako kwasababu yatakusaidia kupima maendeleo yako ili kujua kipi umefanikiwa kukifanya katika kitu chochote ambacho umedhamiria kukifanya, pia yatakusaidia mjasiriamali kujiamini na kusonga mbele.

Pamoja na umuhimu wa malengo kama tulivyoona hapo juu, kuna baadhi ya vitu vya kukumbuka kila mara unapokaa chini ili kujiwekea malengo yako. Baadhi ya mambo ya kukumbuka ni kama yafuatayo;

Jambo la kwanza ni kujiwekea malengo yenye kueleweka. Elewa kile unachotaka kufanya na kile ambacho biashara yako inataka, ni vigumu kufikia malengo ambayo wewe mwenyewe hujui nini kinatakiwa kufikiwa, kaa chini na changanua nini hasa unakihitaji.

Jambo la pili la kuzingatia ni kuwa jiwekee malengo ambao yanaweza kufanyika na yenye kutoa matokeo. Jiwekee lengo lenye mshiko na si lengo la kufikirika, usiweke malengo ambayo ni mlima kama vile ni usiku unaota! 

Jambo la tatu ni kuweka kwenye maandishi malengo ambayo ungependa kuyafikia na namna ya kuyafikia. Kwa kuweka kwenye maandishi inakusaidia siyo tu kujenga nidhamu, bali pia kufanya kitu hicho kuwa kweli na kujipima badala ya kufikiria tu.

Jambo la nne ni kuzingatiaa muda wa malengo uliojiwekea. Elewa kuwa muda ni kama kipimo cha ulichoweza na ambacho hujaweza. Malengo mazuri lazima yapimwe na muda husika. Mpira wa miguu kwa kawaida huchezwa dakika 90 na baada ya hapo matokeo hufahamika! 

Ndivyo ilivyo katika malengo, kushindwa kufikia kile ulichopanga katika muda fulani isiwe sababu ya wewe kukata tamaa, unaposhindwa kufikia malengo jipange tena kwa wakati mwingine na kwa jambo lingine utafanikiwa tu.

Kukumbuka wakati unajiwekea malengo yako ni muhimu kuanza na malengo madogo yatakayo kupeleka kwenye malengo makubwa. Malengo madogo yatakuhamasisha kuyafikia haraka na hatimaye kufikiria makubwa.

Kujiwekea malengo madogo isimaanishe kujiwekea malengo ya chini. Kujiwekea malengo madogo kusikufanye ufikirie kwa upeo mdogo au kushusha uwezo wako. Mara zote kumbuka safari ni hatua.

Kumbuka kuwa na malengo madogo itakusaidia kujua matatizo ya mwanzo na kuwa na mpango mzuri wa kuyatatua. Na wakati unaendelea utaelewa nini cha kufanya na nini cha kuacha katika kufikia malengo makubwa ya baadaye.

Je, ndugu mjasiriamali jaribu kujiuliza mpaka sasa tunapomaliza mwezi wa kumi na ikiwa imebaki miezi miwii mwaka uishe ulijiwekea malengo gani kama ufunguo wa kukupeleka kwenye mafanikio? Je, ni njia gani umezitumia ili kuweza kuyafikia malengo hayo?
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment