Saturday 9 November 2013

Mwalimu aelezea jinsi alivyopewa mkong'oto na wanafunzi Kigoma

Jumanne ya Septemba 24, 2013 haikuwa siku nzuri kwa Mwalimu Method Lugakila Zakaria wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Masanga, iliyopo katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji mkoani Kigoma.

Miongoni mwa wanafunzi wa shule yake walimgeuka. Wakamfanyia kile anachokielezea kuwa ni udhalilishaji mkubwa dhidi yake binafsi na pia taaluma yake ya ualimu.

Ni kwamba, wanafunzi hao walimzomea, wakampiga mwereka na baada ya kuwa chini, wakamshushia kipigo kilichoambatana na ngumi na mateke.
Mkasa huo ulijiri shuleni kwake mishale ya saa 4:00 asubuhi huku wanafunzi wengine wakishuhudia. Wengine wakapiga kelele za kumuombea msaada, wengine wakamlilia na wachache walibaki wakishangilia na kupiga miluzi.

Tukio hilo lililozua gumzo kubwa Masanga limeshatua kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai na watuhumiwa wawili wameshatiwa mbaroni. 
"Siwezi kuisahau siku hii... niliumia sana kimwili na kisaikolojia," anasema Mwalimu Zakaria.

"Nilivamiwa na baadhi ya wanafunzi, nikapigwa mwereka mpaka chini... kisha wanafunzi hao wakaanza kunishambulia mwilini kwa kunipiga ngumi na mateke. Shati langu lilichanika, damu ikanitoka. Nimepatwa na maumivu makali," anasema Mwalimu Zakaria, ambaye ni msimamizi mkuu wa nidhamu katika shule hiyo.

Kwa maelezo yake, Mwalimu Zakaria anasema kuwa maeneo aliyoumizwa na kupata maumivu makali zaidi siku hiyo ni shingoni, puani na mdomoni.

Anasema baada ya kukumbwa na mkasa huo, wanafunzi wema walimuokoa na baadaye akawahishwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Maweni ambako alipewa mapumziko ya siku nne kabla ya kupata nafuu. "Walionifanyia yote haya ni baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne C," anasema Mwalimu Zakaria.

CHANZO CHA KUPIGWA
Mwalimu Zakaria anasema kuwa wanafunzi waliomvamia na kumpiga walitoka katika darasa la kidato cha nne C, wakiwa ni miongoni mwa watano aliotoka kuwacharaza bakora mbili kila mmoja kwa kosa la kupiga kelele na kumzomea wakati yeye akiendelea kufundisha katika darasa jingine la kidato cha pili.

“Najua sababu za kuchukiwa na baadhi ya wanafunzi hawa... mimi ni mwalimu wa nidhamu. Na siku zote huwa nasimamia sheria za shule bila kuzipindisha. Sheria inavyosema, mimi ndivyo ninavyofanya. 

“Ila nadhani baadhi ya wanafunzi wameharibikiwa maadili muda mrefu,” anasema Mwalimu Zakaria, babamwenye mke na watoto wanne.

"Najihisi kudhalilika. Hata hivyo, sijaanza mchakato wowote wa uhamisho. Ni kwa sababu kesi hii bado iko polisi... haijafikishwa mahakamani," anasema mwalimu huyo ambaye aliajiriwa miaka 12 iliyopita na kuwahi kufundisha pia katika Shule ya Msingi Kigoma, Shule ya Msingi Kibirizi, Shule ya Sekondari Bushabani na mwaka 2012 ndipo akahamishiwa katika shule aliyopo sasa ya sekondari ya kata ya Masanga.

"Nina miaka mitatu sasa tangu nianze kufundisha hapa," anasema Mwalimu Zakaria, huku akiwataja wanafunzi watatu anaodai kuwa ndiyo waliompiga (majina tunayahifadhi).

"Na hawa ndiyo niliowashtaki polisi... serikali iangalie pia namna ya kuwalinda walimu wanaokumbana na vituko vya wanafunzi wa aina hii wawapo kazini," anasema.

Akieleza zaidi, anasema kuwa awali, mwanafunzi mmojawapo kati ya waliompiga alisimamishwa kwa siku 21 kutokana na utovu wa nidhamu. Mwanafunzi huyo alitakiwa kufika shuleni akiwa na mzazi wake. 

Hata hivyo, katika siku hiyo (Septemba 24), mwanafunzi huyo alifika peke yake na kuungana na wenzake (wa kidato cha nne C) kupiga kelele. Anasema baada ya kuwaadhibu wanafunzi watano kwa kosa la kupiga kelele, akamtaka huyo aliyetakiwa kufika na mzazi wake kufanya hivyo.

Anasema kuwa baadaye, mwanafunzi huyo akamleta kweli mzazi wake. Wakati huo yeye alikuwa akiendelea kufundisha somo la Fizikia katika darasa la kidato cha pili.
Wakati akiendelea kufundisha, ndipo akafika mwanafunzi huyo na kumtaka yeye (mwalimu) atoke darasani kwani tayari alishafika na mzazi wake kama alivyoagizwa. 

Licha ya Mwalimu Zakaria kumjibu kuwa asubiri hadi amalize kipindi, bado mwanafunzi huyo alirejea tena na kugonga mlango huku akiwa na mzazi wake.

Mwalimu Zakaria akalazimika kutoka tena na kuanza kuzungumza na mzazi huyo. Ghafla, mwanafunzi huyo aliyeonekana kukerwa na mazungumzo ya mwalimu (Zakaria) na mzazi wake akamvamia (Mwalimu Zakaria) na kuanza kumpiga, tena mbele ya mzazi. 

Mara, wakaongezeka wanafunzi wengine wawili kati ya wale aliowaadhibu kwa fimbo na  kumchangia kwa kipigo.

"Siwezi kuelezea zaidi. Bodi ya Shule imeshafanya uamuzi wake na Polisi wanaendelea na upelelezi wao," alisema Mwalimu Zakaria.

Bodi ya shule hiyo iliamua kuwafukuza shule wanafunzi wawili, mmoja akaadhibiwa kwa kucharazwa bakora tatu mbele ya wanafunzi wote na wawili walisimamishwa shule hadi siku ilipoanza mitihani ya kidato cha nne. Wawili waliofukuzwa walikamatwa na polisi na kushikiliwa katika mahabusu ya Kituo cha Polisi Kati Kigoma/Ujiji. 

YALIYOJIFICHA

Mwalimu Zakaria hufundisha somo moja tu la Fizikia. Anasema kuwa mara zote hupata wakati mgumu katika kulifanya somo hilo lipendwe na wanafunzi na hatimaye wafanye vizuri kutokana na changamoto nyingi zilizopo shuleni kwao.   

"Hakuna vitabu vya kutosha wala vya maabara. Hata viwanja vya michezo kwa ajili ya wanafunzi hakuna. Na pia wanafunzi wengi ni watoro," anasema Zakaria.

Mwalimu Zakaria anasema kuwa tatizo jingine linalochangia utovu mkubwa wa nidhamu shuleni kwao ni aina ya wanafunzi walio nao, ambao wengi hawapati uangalizi mzuri wa wazazi wao kwavile wanaishi peke yao katika maeneo ya jirani na shule.

"Wanafunzi wanatoka katika maeneo tofauti na wengi wanaishi bila wazazi. Hili pia ni tatizo," anasema Zakaria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walikiri kuwa wenzao waliomfanyia vurugu Mwalimu Zakaria ni wakorofi.
Hata hivyo, wanamlaumu pia Mwalimu Zakaria kwa kusema kuwa anapenda sana kuchapa. 

"Mwalimu (Zakaria) naye ni mkali sana. Tungependa ahamishwe tu kwa sababu anapenda sana kutoa adhabu kali kali. Kwake kila kosa ni fimbo au kurukishwa kichurachura. Ukisalimika anakwambia kamlete mzazi wako, na akija unafukuzwa shule. Ndiyo maana wengine walishangilia baada ya kuona akipigwa," alisema mmoja wa wanafunzi.    

"Hata mwaka jana kuna mwanafunzi alifukuzwa shule kwa sababu ya mwalimu huyu... anapenda sana kuchapa na ndiyo maana wengine anagombana nao," mwingine anaongeza.  

Yapo pia madai kwamba wanafunzi wana malalamiko mengi ambayo hadi sasa hayajapatiwa majibu, baadhi yakiwa ni kuchangishwa Sh. 10,000 kila mmoja kwa ajili ya kuletewa walimu wa masomo ya sayansi ambao hata hivyo hawapo (ukimuondoa Mwalimu Zakaria wa somo la Fizikia), mchango wa madebe ya unga na maharage ili wapikiwe chakula ambacho hadi wakati wakizungumza na NIPASHE, walikuwa bado hawajawahi kupatiwa. 

Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Komba, anasema wanafunzi kumpiga mwalimu ni kosa kubwa sana kwani ni sawa na mtoto kumpiga mzazi wake. 

Anasema baadhi ya wanafunzi shuleni kwao wameunda kundi hatari linalojihusisha na utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na kukiuka maelekezo ya walimu.

"Ukiangalia Mwalimu Zakaria ni wa nidhamu. Anakutana na vijana hawa kila siku na huwapa adhabu kwa makosa mbalimbali, hasa ya uchelewaji, kuchomekea shati na usafi wa nywele. Matokeo yake wanafunzi wanamuona kuwa mkorofi, hawafai," anasema Mwalimu Komba.

Mwaka jana, shule hiyo ya sekondari Masanga ilipata matokeo mabaya ya kukosa daraja la kwanza na la pili, daraja la tatu mwanafunzi mmoja, daraja la nne wanafunzi 37 na wanafunzi 245 walipata daraja sifuri.

AFISA ELIMU
Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Bruno Sangwa anasema maamuzi ya kikao cha bodi yalikuwa sahihi kwani yalizingatia sheria ya elimu namba 25 ya mwaka 1978 na marekebisho yake ya mwaka 2002, pamoja na waraka wa elimu namba 4 wa mwaka 2012.

Analaani tukio hilo la kupigwa kwa mwalimu na kuitaka jamii, hasa wazazi kushirikiana kwa pamoja katika kuwalea vyema vijana.  

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai alithibitisha kuwashikilia wanafunzi wawili na kuiambia NIPASHE kuwa wangefikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Naibu Waziri wa Elimu, Philip Mulugo alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alielezea kusikitishwa kwake; lakini akaongeza kuwa hawezi kulizungumzia zaidi kwavile halijaletwa kwake na hivyo hajui undani wake.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment